Tuesday, October 24, 2017

KAYA ZAIDI YA 7000 GOGONI KIBAMBA KUPATA NEEMA YA MAJI

Halmashauri ya Ubungo inayongozwa na Ndg John Lipesi Kayombo imejidhatiti kutoa huduma kwa wananchi wake.

Hayo yamebainishwa leo na Kaimu Mhandisi wa Maji wa Manispaa ya Ubungo ndg Ramadhani Mabula wakati wa kutembelea  kisima cha maji eneo la Mtaa wa Gogoni Kata ya Kibamba.

Mabula amesema kisima hicho ni cha kipekee kwa mkoa wa Dar es Salaam ambacho kinauwezo wa kutoa maji lita elfu kumi na nane (lita 18,000 ) kwa saa bila ya kutumia pampu.

Kisima kimechimbwa mwaka 2014 kina urefu wa mita 100 kwenda chini na maji yake hayana chumvi ni maji mazuri kwa matumizi ya binadamu.

Mhadisi Mabula amesema kwa mwaka huu wa fedha Manispaa imetenga tsh milioni 100 kwa ajili ya kutengeneza miundo mbinu ya maji kwa lengo la kusambaza maji hayo katika jamii inayozunguka kisima hicho.

Licha ya kuwa mradi huu ili ukamilike unahitaji fedha takribani milioni 280, kwa fedha  ambazo zimetengwa mwaka huu wa fedha zitatumika kujenga fensi ,kulaza mabomba ya maji na kuweka tanki la maji lenye ujazo wa lita elfu 90 hiyo ni awamu ya kwanza.

Awamu ya pili itakuwa ni kuhakikisha maji hayo yanafika kila kaya inayozunguka kisima hicho na kuunda jumuiya za maji ambazo zitakuwa zinasimamia huduma hiyo.

Mhandisi Mabula  amewaomba wananchi wa eneo hilo kuzingatia sheria ya utunzaji wa vyanzo vya maji ikiwemo pamoja na kutojenga nyumba umbali wa mita 60 na pia kupanda miti ambayo ni rafiki wa maji.

Maji ni uhai , Kwa pamoja tutaijenga Ubungo yetu

No comments:

Post a Comment