Tuesday, October 3, 2017

Jalada kesi ya Mpemba, wenzake lakwama kwa DPP wakituhumiwa kwa ujangili mikoa minne

By Hadija Jumanne, Mwananchi hjumanne@mwananchi.co.tz
Dar es Salaam. Jalada la kesi inayomkabili mfanyabiashara, Yusuf Ali maarufu kama Mpemba na wenzake watano bado lipo mikononi mwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Mashtaka (DPP).
Hayo yalisemwa jana na upande wa mashtaka katika kesi ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo inayomkabili mfanyabiashara huo.
Yusuf na wenzake wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara haramu ya meno ya tembo yenye thamani ya Sh785.6 milioni na tayari upelelezi wa kesi hiyo umekamilika.
Wakili wa Serikali, Elia Athanas aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba kuwa jalada hilo lipo kwa DPP kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.
Kesi hiyo jana ilifikishwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa.
Athanas alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo umeshakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Kutokana na maelezo hayo, Hakimu Simba aliahirisha kesi hiyo hadi Oktoba 17 itakapofikishwa tena kwa ajili ya kutajwa.
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni mkazi wa Mlimba mkoani Morogoro, Charles Mrutu; mkazi wa Mbagala Chamazi, Benedict Kungwa; mkazi wa Mbezi, Jumanne Chima; Ahmed Nyagongo ambaye ni dereva na Pius Kulagwa ambao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka manne ya kujihusisha na biashara ya meno ya tembo.
Inadaiwa kwamba katika tarehe tofauti kati ya Januari, 2014 na Oktoba, 2016 wakiwa Dar es Salaam, Tanga, Iringa na Mtwara walijihusisha na mtandao wa ujangili.
Katika mashtaka hayo inadaiwa walijihusisha na mtandao huo kwa kukusanya na kuuza nyara za Serikali ambazo ni vipande 50 vya meno ya tembo vyenye thamani ya Dola 180,000 za Marekani (sawa na Sh392.8 milioni) bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori nchini.
Katika shtaka la pili inadaiwa kuwa Oktoba 26, 2016 wakiwa Mbagala Zakhem jijini Dar es salaam walikutwa na vipande 10 vya meno ya tembo vyenye uzito wa kilo 13.85 vikiwa na thamani ya Dola 30,000 za Marekani (Sh 65.4 milioni).
Kwenye shtaka la tatu washtakiwa hao inadaiwa kwamba Oktoba 27, 2016 wakiwa Tabata Kisukuru walikutwa na vipande vinne vya meno hayo vikiwa na uzito wa kilo 11.1 na thamani ya Dola 15,000 za Marekani (sawa na Sh32.7 milioni).
Aidha, Oktoba 29, 2016 walikutwa na vipande 36 vya thamani ya Sh294.6 milioni bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa wanyamapori.

No comments:

Post a Comment