Saturday, October 28, 2017

DKT ANGELINE MABULA AKABIDHI VIFAA VYA USAFI

Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula leo ameshiriki utekelezaji wa agizo la Mhe Rais Dkt John Magufuli la kufanya usafi kwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi zoezi lililofanyika katika soko la Kirumba wilayani Ilemela mkoa wa Mwanza na baadae kukabidhi vifaa vya kufanyia usafi kwa Vikundi mbalimbali vilivyojitokeza vinavyojihusisha na Usafi katika viwanja vya Furahisha kwa ufadhili wa shirika la mazingira la Swiss Contact

Akizungumza katika viwanja hivyo Mhe Dkt Angeline Mabula amewataka wananchi wa Ilemela kulipa kipaumbele suala la usafi na kuacha kusubiri wageni kutoka nje ya Ilemela kuja kuhimiza  ufanyaji wa Usafi sambamba na kuwakumbusha historia ya usafi wa mji wa Mwanza

‘… Wote ni mashahidi Jiji la Mwanza liliwahi kuongoza katika usafi wa nchi hii kwa miaka Tisa mfululizo na nnaposema Jiji la Mwanza ni pamoja na Ilemela lakini baada ya kutengana tu mwaka 2012 hakuna tena Usafi na kombe halipo limeenda kwengine sasa hapa tuulizane nini tunatakiwa kukifanya? Wapi tumekosea? Kipi kimeenda vibaya?, Na suala la usafi wa nyumbani sizani kama linahitaji mpaka mtu atoke nje kuja kukufundisha …’ Alisema

Aidha Mhe Dkt Angeline Mabula amevitaka Vikundi vilivyokabidhiwa vifaa vya Usafi kuvitunza vifaa hivyo sambamba na kuvitumia kwa kufuata utaratibu ili kujikinga na maradhi huku akisisitiza kuchukuliwa kwa hatua za kisheria kwa watu wote wanaochafua mazingira

Akimkaribisha mgeni rasmi mstahiki meya wa manispaa ya Ilemela Mhe Renatus Mulunga amesema kuwa manispaa yake itaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja kuwaomba wananchi na viongozi kushirikiana katika kuboresha mazingira

Kwa  upande wake muwakilishi wa taasisi ya mazingira ya Swiss Contact Ndugu Patrick mbali na kushukuru kwa ushirikiano alioupata kutoka manispaa ya Ilemela amewataka vijana wa Jimbo hilo kuiona sekta ya mazingira kama fursa katika kupambana na changamoto ya ajira itakayoajiri vijana wengi kama wataamua kujihusisha na sekta hiyo kupitia kauli mbiu yake ya ‘TAKA NI MALI’

Akihitimisha Afisa mazingira wa manispaa ya Ilemela Ndugu Daniel Batare amemuhakikishia mbunge huyo kuhakikisha wananchi wanaochafua mazingira wanachukuliwa hatua sanjari na kuwakaribisha wadau mbalimbali katika kuunga mkono jitihada za kuboresha mazingira ya mji wa Ilemela

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
28.10.2017

No comments:

Post a Comment