Wasimamizi wa miradi ya kutoa ajira za muda kwa wanufaika wa mpango wa Tasaf kutoka halmashauri na manispaa ya Singida wakimsikiliza kwa makini Mkuu wa Mkoa wa Singida (hayupo pichani) wakati akifungua mafunzo ya uwezeshaji wa kusimamia miradi hiyo. Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Singida Patrick Girigo Kasango akiwa na Afisa Ufuatiliaji kutoka Tasaf Sinith Haule wakifurahia jambo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uwezeshaji wa kusimamia miradi ya ajira za muda kwa wasimamizi wa kutoka halmashauri na manispaa ya Singida. Ramadhani Alute kutoka kata ya Minga manispaa ya Singida akiandika baadhi ya mambo katika mafunzo ya uwezeshaji wa kusimamia miradi ya ajira za muda kwa wasimamizi wa kutoka halmashauri na manispaa ya Singida.
Wanufaika wa mpango
wa Kunusuru kaya masikini Tasaf, Mkoa wa Singida wametakiwa kupanda mikorosho
ili waweze kutunza mazingira pamoja na kujiongezea kipato kutokana na zao la
korosho.
Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dkt Rehema Nchimbi ametoa rai hiyo wakati akifungua mafunzo ya
uwezeshaji kwa wasimamizi 67 wa miradi ya kutoa ajira za muda kwa wanufaika wa
mpango wa Tasaf kutoka halmashauri na manispaa ya Singida.
Dkt Nchimbi amesema
kutokana na kuwa ajira za muda kwa awamu hii zimelenga katika utunzaji wa
mazingira kwa kupanda miti hivyo amewataka Tasaf mkoa wa Singida kuwasiliana na
Bodi ya Korosho waweze kupatiwa mbegu ili isipandwe miti mingine bali
mikorosho.
Amesema kwa kufanya
hivyo mkoa wa Singida utaweza kuwa mzalishaji mkubwa wa Korosho huku ajira hiyo
ya muda ya kutunza mazingira kwa kupanda mikorosho, ikiwa imewatengenezea
wanufaika hao ajira yao ya kudumu.
“Tukiweza kupanda
mikorosho kwa zoezi hili la ajira za muda baada ya muda wanufaika hawa wataweza
kuwa na kipato kikubwa kwa kuweza kuuza korosho zao, hii itakuwa ndio maana
halisi ya mpango wa kunusuru kaya masikini ambapo zinatakiwa pia zishiriki
katika kukuza uchumi”, amesema na kuongeza kuwa,
“Katika kuelekea Tanzania
ya uchumi wa kati wa viwanda haimaanishi kila mtu afungue kiwanda bali kila
mwananchi asiachwe nyuma katika kufanikisha uwepo wa viwanda, kwa maana hiyo
hawa wanufaika watasaidia uwepo wa viwanda kutokana na malighafi ya korosho
watakayoilima”, amefafanua.
Dkt Nchimbi ameongeza
kuwa miradi ya ajira za muda itafanikiwa endapo itaweza kuwajengea uwezo
wanufaika hao wa kutambua fursa za kujiajiri na sio kupokea fedha na kuzitumia
kisha kurudi katika umasikini ule ule.
Aidha amewataka
watumishi wa umma wasiwafundishe wanufaika hao kulalamika kuwa fedha ni ndogo
kama ambavyo wao wamekuwa wakilalamikia mishahara, bali wajifunze kwa wanufaika
ambao wameweza kuanzisha miradi kama ufugaji kuku, kilimo cha bustani kutokana
na fedha ndogo wanayopata.
Kwa upande wake
Mratibu wa Tasaf Mkoa wa Singida Patrick Girigo Kasango amesema mpango wa ajira
za muda kupitia Tasaf unafanyika katika halmashauri nne kati ya saba kwa Mkoa
wa Singida ambazo ni halmashauri ya Singida, manispaa ya Singida, Malakama na
Iramba.
Kasango amesema kwa
awamu hii ajira za muda zimelenga katika kutunza mazingira kwa kupanda miti,
kutengeneza mabwawa ya maji na kuzuia mmomonyoko wa udongo.
Ameongeza kuwa ajira
hizo hufanyika kipindi ambacho si cha kilimo pia wanufaika hao watafanya kazi
kwa muda wa masaa manne kwa muda wa siku sitini ambapo watakuwa wanalipwa kiasi
cha shilingi 2300 kwa masaa hayo.
Girigo amesema wasimamizi
27 kwa Manispaa ya Singida, 40 halmashauri ya Singida, 41 Mkalama na 42 Iramba
watapewa mafunzo kwa siku sita pamoja na mafunzo kwa vitendo yatakayowawezesha
kusimamia vema ajira za muda.
Naye mmoja wa
washiriki amesema mara baada ya mafunzo hayo wasimamizi hao wakatoe mafunzo kwa
wanufaika waweze kutumia fursa ya ajira za muda na fedha watazopata kwa
kujiendeleza kiuchumi.
Ramadhani Alute
kutoka kata ya Minga manispaa ya Singida amesema watajitahidi kuwaelekeza
vizuri wanufaika hao ili wasizitumie vibaya fedha hizo bali wawekeze hicho
watakachopata kwa manufaa ya baadaye.
No comments:
Post a Comment