Neno La Wakati Mwema
Na Mathias Canal
Tunapaswa kukumbuka kuwa msingi wa kuumbwa kwa Mwanadamu ni ibada tena kwa kauli yake mwenyewe Mwenyezi Mungu aliposema “Na Sikuwaumba wanaadamu na majini isipokuwa ni kuja kuniabudu mimi tu” Lakini maneno ya Mwenyezi Mungu yanaendelea zaidi kutuhabarisha kuwa wanadamu wote wanapaswa kushikamana pasina kutengana.
Awali ya yote hatuna budi kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba wa mbingu na ardhi na vingine vyote vilivyomo ndani yake, Mwenyezi Mungu tunayemuabudu siku zote ni mmoja na asiyeingiliwa na Mwanadamu katika maamuzi yake .
Hivi karibuni nilizuru visiwani Zanzibar katika mikoa ya Kaskazini na Kusini Pemba ambapo nikiwa huko Pemba nilifanikiwa pia kufika katika Wilaya zote nne ikiwemo Wilaya ya Wete, Mkoani, Micheweni na Chakechake ambapo huko nilituama kwa takribani siku nne hivi zilizonipa hamasa ya kufahamu hali ya siasa visiwani humo kabla ya uchaguzi mkuu 2015 ulivyokuwa na baada ya uchaguzi huo jinsi hali ya siasa ilivyokuwa na hata kudodosa ili kujua hali ya kisiasa ilivyo kwa hivi sasa.
Nilijiridhisha kuwa hali ya siasa inaendelea kuimarika kutokana na juhudi za Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dkt Ali Mohamed Shein kuendelea kuiletea maendeleo Zanzibar ukilinganisha na miaka mitano iliyopita.
Nikiwa katika maskani ya Subira Yavuta Kheri ambayo ni mojawapo ya maskani yenye kutuama vijana wengi huko Pemba na kujadili fikra chanya za mustakabali wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla niliwasikia vijana wakijadili juu ya siasa za chuki zilizoenezwa na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF aliyesimamishwa uongozi Maalim Seif Shariff Hamad.
Si tu kueneza chuki dhidi ya serikali kwa kuhubiri siasa za mgawanyiko bali pia alifikia hatua ya kuwafanya waumini wa dini ya Kiislamu kutengana kuwa na dini mbili ndani ya Uislamu ambazo ni ile ya CUF na nyingine ya wafuasi wa CCM.
Hapo kabla wanachama wa Chama Cha wananchi CUF na CCM walikuwa wakisali pamoja sambamba na tofauti zao za kisiasa ingawa baadhi ya misikiti ilishatoa tamko tokea Mwaka 2010 juu ya kukataa kwao kusali na watu wa itikadi tofauti ya chama na hivyo kufanya ubaguzi ndani ya nyumba za Mwenyezi Mungu.
Mnamo mwaka 2016 baada ya kufanyika kura ya marejeo baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Jecha Salum Jecha, la kuitisha uchaguzi wa marudio tarehe 20 Machi baada ya ule Octoba 25, 2015 kwa kugundulika kuwa na kasoro kwa masikitiko makubwa kikundi cha watu wachache kwa maagizo ya Maalim Seif Sharrif Hamad waliamua kwa wazi kabisa kumkosoa Mungu hadharani juu ya amri yake ya kuwataka watu wasali misikitini na kuanza kuwashawishi watu kutoka misikiti mingine ya pembezoni mwa kitongoji cha Kiungoni Kimango ili waunge mkono suala hilo na baada ya misuguano ya wanaotaka na wasiotaka na hatimaye wote wakaunga mkono jambo lililopelekea wanaccm kuanza kusali katika msikiti mmoja pekee ambao baadaye napo walipigwa vita na hatimaye kufukuzwa katika misikiti yote na kuanza kusali majumbani.
Kuzuiliwa kusali ilikuwa ni kipindi kilichokaribiana na mwezi wa ramadhan hivyo wafuasi hao wa CCM waliamua kujikusanya kuswali ibada za funga katika banda la MASEMP kwa muda wa mwaka mzima kwa kudhani pengine wafuasi wa CUF wangeweza kubadili mawazo na ndipo walipogundua kuwa chuki tayari ilikuwa imewajaa waliamua kutafakari kuhusu ujenzi wa msikiti wao ili kuondokana na kadhia ya namna kama hiyo hata katika uchaguzi mwingine ujao.
Ndugu zangu mtu yeyote anayepinga amri ya Mwenyezi Mungu atakuwa amekufuru na sura yake ni kuwa ameidhulumu nafsi yake, inasikitisha kwa wakazi wa mji wa Kiungoni Kimango Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba ambao ni waislamu na wafuasi wa Maalim seif Sharrif Hamad kuwafukuza waislamu wenzao misikitini kwa kisingizio cha itikadi za vyama vya siasa jambo ambalo halimo katika Uislamu.
Mwenyezi Mungu anatoa onyo kali katika Quran kwa wale wanao thubutu kuzuia waislamu misikitini kwa kusema “Na ni nani dhalimu mkubwa zaidi kuliko Yule anayewafukuza watu misikitini na kutajwa jina lake ndani yake” lakini pia Mwenyezi Mungu amejitangaza ndani ya Quran kuwa yeye ndiye mmiliki wa misikiti kwa kusema “Hakika ya misikiti yote ni nyumba za Mwenyezi Mungu”
Tulitafakari swala hili la udini linalozidi kuenezwa na Maalim Seif Sharrif Hamad lilivyoanza, Mchambuzi Ahmed Hussein anasema kuwa Kama kuna chanzo cha hatari kwa umoja na mshikamano wa Kitaifa nchini basi ni Siasa za Urais. Siasa za Urais ndizo zilizochokoza hisia za udini ambazo zilikuwa zimezikwa na dhana ya Utaifa kwa muda mrefu hususani miongoni mwa wananchi wa kawaida.
Siasa za kuchaguana au kukataana kwa misingi ya udini hazikuwepo kabisa katika chaguzi zote zilizofanyika chini ya Mfumo wa Chama kimoja. Na hata ukirudi nyuma hadi enzi za ushindani wa vyama vingi, TANU, UTP, hakukuwa na hisia za udini ambapo Umma wa Watanganyika Waislamu kwa Wakristo ulishiriki katika chaguzi bila hisia za udini.
Katika kipindi chote cha chaguzi za Chama kimoja baada ya vyama vingi kupigwa marufuku, Watanzania walishiriki katika chaguzi bila kujisikia kwamba wao ni Waislamu au ni Wakristo.
Kwa kifupi hadi uchaguzi wa mwisho uliokamilisha ngwe ya pili ya Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1990, hakukuwa na hisia za udini katika siasa, na kama zilikuwepo basi kwa wachache mno ambao nao walizificha kabisa.
Mlipuko wa hisia za udini katika siasa, kwa kiasi kikubwa, ulichochewa na madhila yaliyotokana na hatua ya Waislamu kuondoa uovu wa mkono pale walipovunja bucha za nguruwe baada ya serikali kushindwa kujibu malalamiko yao dhidi ya uuzaji holela wa nyama ya nguruwe.
Augustine Liyatonga Mrema, Waziri wa Mambo ya Ndani na Naibu Waziri Mkuu kipindi hicho, alilivalia njuga suala hilo na kulitumia jeshi la polisi kwa nguvu kubwa. Uhasama baina ya Mrema, kama Waziri wa Mambo ya Ndani na Waislamu ukahamia katika siasa.
Kwanza, Waislamu walionesha kuisusa CCM, ambapo waliweza hata kukusanya kadi za chama hicho kama ishara ya kukikataa. Almarhum Amir Awwalina, ndiye aliyezikusanya kadi za CCM kutoka kwa Waislamu.
Jambo hili lilianza na likamalizika lakini zaidi ya miaka 20 baadaye Babu Seif akaja na gia nyingine ya kueneza Udini tena aina hii ya udini haikuwa ni kati ya dini moja kwenda nyingine bali ilikuwa ni kwa mujibu wa dini moja kutengenezewa chuki ya ndani kwa ndani kwa utofauti wa fikra za kiasiasa.
Ndugu zangu kwa mujibu wa Dotto C. Rangimoto katika andiko lake la Tasnifu za njano5: Uhusiano kati ya dini na siasa za Tanzania alibainisha kuwa pamoja na mambo mengine, lengo la kuanzishwa dini ni kuleta maisha bora kwa jamii, na kwa kuwa maisha bora ya jamii huhitaji maamuzi ya umma juu ya mambo kadhaa ambayo kwayo umma unaona pindi yakifanywa maisha yatakuwa bora, hivyo basi dini zetu nazo hujiingiza katika siasa kwa minajili ya kuharakisha harakati za kuleta maisha bora.
Siasa ni njia ya kufanya maamuzi ya umma katika mji, au nchi au duniani haijalishi kwa maslahi ya umma huo au kwa maslahi ya watu wachache.
Kwakuwa masuala mengi yanayohusu umma kama vile ya afya, ajira, elimu, na mengi ya kufananayo yanahitaji maamuzi ya umma, na kwakuwa siasa ndio njia ya kufanya hayo maamuzi ya umma, hivyo basi mambo yote yanayohusu umma hutawaliwa na siasa.
Kwa hivyo napata uhalali wa kusema kuwa siasa ndio kila kitu kwa mustakabali wa umma na katu mwanadamu hawezi kujitenga na siasa midhali yungali ni sehemu ya umma.
Lakini Udini ni kile kitendo cha kuwabagua, kuwatenga, kuwanyanyasa na hata kuwatesa watu wa dini fulani tu huku watu wengine wakiendelea kuneemeka.
Pamoja na hayo siwezi kusema kuwa nchi ya Uingereza ina udini kisa tu serikali ya nchi hiyo inafuata na kutii mambo kadhaa ya kanisa la kianglikani, siwezi kusema kuwa nchi ya Italia ina udini kisa tu inatii na kufuata mambo kadhaa ya kanisa la Roma, pia siwezi kusema kuwa Saudi Arabia ina udini kisa tu inafuata na kutii mambo kadhaa ya kiislamu.
Lakini nimemua kuanisha tu kwa namna gani ambavyo Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi CUF aliyesimamishwa uongozi na chama chake Maalim Seif Shariff Hamad asivyofaa kuwa kiongozi katika Visiwa vya Zanzibar na hata pengine nchini Tanzania.
Maalim Seif si tu hana haiba ya kuwa kiongozi bali hafai kabisa kuwa kiongozi kutokana na uroho wa madaraka kwani siku zote huwa anapenda watu wawe chini yake na ndiyo maana mara kwa mara kunakuwa na kutoelewana ndani ya CUF, Lakini pia ni Mgomvi na anapenda fedha kuliko kupenda amani na mshikamano wa watu anaowaongoza.
Kwa bahati nzuri mimi ni miongoni mwa vijana zaidi ya 300 tuliopata fursa ya kushiriki Kambi ya mafunzo ya Uongozi yaliyofanyika kuanzia Agosti 23 mpaka Agosti 24, 2017 katika chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (THE MWALIMU NYERERE MEMORIAL ACADEMY-MNMA) yakiongozwa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (NEC) Itikadi na Uenezi Ndg Humphrey Polepole.
Katika kambi hiyo ya siku tatu iliyojikita zaidi kuwafundisha vijana juu ya Uongozi wetu na hatima ya Tanzania, Tulikotoka, Tulipo na Tunapokwenda Ndg Polepole alieleza kwa kina kuhusu Kiongozi na Uongozi ambapo pamoja na mambo mengine alibainisha sifa mbalimbali za kuwa kiongozi lakini mimi nitazitaja mbili.
Kiongozi lazima Ajitambue mwenyewe, Hapa alieleza kuwa Lazima kiongozi ajitambue mwenyewe ni mtu wa namna gani, ajue uwezo wake na upungufu wake na awe tayari kujiongezea maarifa kila siku, ili aweze kukabili changamoto na mabadiliko ya ulimwengu. Asome, afuatilie mambo yanavyokwenda na ajifunze kwa wenzake kuhusu kufanikisha malengo yake. Hapa tutakubaliana kwa pamoja kuwa Maalim Seif ameikosa sifa hii kwani hajitambui alipotoka, alipo na anapokwenda
Kiongozi lazimaAdhibiti msongo wa mawazo, Tunamtarajia kiongozi mzuri awe ni mtu mwenye kupunguza msongo wa mawazo, ili kuifanya akili yake ifikie maamuzi sahihi, lakini kama atakuwa mwenye kuwaza mengi, atajikuta anachanganyikiwa na kuwa mtu wa jazba katika maamuzi na hivyo kuipotosha jamii. Naamini umenielewa ni wazi kuwa Maalim Seif anawaza mambo mengi anawaza hatma ya ukatibu wake, anawaza Ruzuku wakati huo huo anaota ndoto ya kuwa Rais wa Zanzibar ilia pate burudani ya ving’ora barabarani.
HITIMISHO
Mwanafalsafa Winston Churchill aliwahi kusema "The price of greatness is responsibility." Thamani ya ukuu ni uwajibikaji.
Nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais katika serikali ya Mapinduzi Zanzibar aliyoiwahi kuipata Maalim Seif Sharrif Hamad na thamani ya ukatibu mkuu aliyoipata katika chama cha wanachi CUF pengine yawezakana kabisa alishindwa kuitumia kwa kuwajibika ipasavyo kwa maslahi ya maendeleo ya wananchi na Taifa kwa ujumla badala yake aliamua kuitumia kwa chuki za udini kwa Wanzibar ili ahatarishe amani na mshikamano wa Wazanzibar lakini kwa juhudi za Rais Dkt Shein alikwama na kuishia kugoma kumsalimu na hata kushikana mkono.
Pili, Kukosa Dhamira ya Kweli: Maalim Seif alishindwa kuwajibika kwa ukweli katika nafasi yake ya kiserikali na chama chake, Alikosa maono kama Kiongozi na kushindwa kuivusha CUF katika mgogoro iliokuwa nao badala yake alizidisha kukoleza kaa la ugomvi lililopelekea kuzidiwa nguvu na wenzake.
Naam wanaccm kuzuiwa kuswali msikitini ni matokeo ya siasa za hila zilizoongozwa na Maalim Seif Sharrif Hamad
Ni Neno La Wakati Mwema
Mathias Canal
0756413465
Dar es salaam
No comments:
Post a Comment