Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga,
akizungumza na wahandisi (hawapo pichani), wakati wa kufunga Mkutano wa
15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.
Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa
Wahandisi nchini (ERB), Mhandisi, Profesa Ninatubu Lema, akisisitiza
jambo wakati wa kufunga Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika
leo mjini Dodoma.
Kaimu Msajili wa Bodi ya Usajili
wa Wahandisi nchini (ERB), Mhandisi Patrick Barozi, akisoma maazimio
yaliyofikiwa katika Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika
mjini Dodoma.
Baadhi ya wahandisi wakimsikiliza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya
Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga (hayupo pichani), wakati wa kufunga
Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi uliofanyika leo mjini Dodoma.
Katibu Mkuu wa wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph
Nyamhanga, akimkabidhi cheti mmoja wa watoa huduma aliyefanya vizuri
katika utoaji wahuduma bora kwenye Mkutano wa 15 wa mwaka wa wahandisi
uliofanyika leo mjini Dodoma. Wa tatu kulia ni Mkurugenzi wa Barabara
kutoka Sekta hiyo Mhandisi Ven Ndyamukama, akishuhudia tukio hilo.
…………………….
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph Nyamhanga,
amezungumzia umuhimu wa Wizara, Taasisi na Idara za Serikali kutumia
vifungu vilivyopo kwenye sheria ya ununuzi wa umma ya mwaka 2011 na
kanuni za ununuzi wa umma za mwaka 2013 na marekebisho yake ya mwaka
2016.
Sheria hiyo inawapa fursa
makandarasi wazalendo, watalamu washauri, wa zabuni na watoa huduma
mbalimbali kupata fursa nyingi katika miradi mbalimbali ya ujenzi hapa
nchini.
Akifunga maadhimisho ya 15 ya
Wahandisi mjini Dodoma, Mhandisi Nyamhanga, amesema chini ya sheria ya
sasa miradi isiyozidi bilioni 10 imewekewa utaratibu mzuri wa
kutekelezwa na makandarasi wazalendo na hivyo kuwawezesha kukuza uwezo
wa kitaaluma na kiuchumi.
“Hakikisheni mnapopata miradi hii
mnafanya kazi kwa weledi kwa kuzingatia muda na thamani ya fedha ili
kuongeza tija katika miradi yenyewe na kutoa fursa kwa miradi mikubwa
kupewa makandarasi wazalendo”, amesema Mhandisi Nyamhanga.
Amewataka wahandisi kutumia
maadhimisho ya 15 kama somo la kukabiliana na changamoto mbalimbali
zinazolikabili Taifa ili kufikia malengo ya kuifanya Tanzania kuwa nchi
ya uchumi wa kati yenye viwanda na rasilimali watu wenye weledi wa
kisasa.
Aidha, ametoa wito kwa Bodi ya Usajili ya Wahandisi (ERB),
kutoa kipaumbele kwa wanafunzi waliohitimu katika kozi ya kihandisi kwa
kugharamia mafunzo kwa vitendo kwa kutumia fedha zinazotolewa na
Serikali na zile za wafadhili ili kuweza kuendeleza taaluma kwa
Wahandisi.
“Wizara itaendelea na mkakati wake
wa kufadhili mafunzo kwa vitendo na kuhakikisha wahitimu wa vyuo
mbalimbali vya wahandisi nchini wanakidhi mahitaji soko la ajira ndani
na nje ya nchi”, amesisitiza Mhandisi Nyamhanga.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi
ya ERB, Mhandisi Profesa Ninatubu Lema, amewapongeza watoa mada wote
walioshiriki katika maadhimisho ya 15 na kuahidi bodi hiyo itayafanyia
kazi mafunzo hayo na kuhakikisha kila mhandisi ananufaika na mafunzo
hayo.
katika maadhimisho hayo wahandisi
wamepata fursa ya kujifunza maswala ya utafiti na maendeleo, ubunifu,
masoko na ujasiriamali, maendeleo ya viwanda na utunzaji wa mazingira,
na uharakishaji wa Teknolojia, habari na mawasiliano kijamii, kiuchumi
na kimaendeleo.
Naye Kaimu Msajili wa Bodi ya ERB,
Mhandisi Patrick Barozi, amesema bodi hiyo imejipanga kikamilifu
kuhakikisha wahandisi wanapata mazingira mazuri ya kufanya kazi ndani na
nje ya nchi kwa kuzingatia weledi, uadilifu na ubora unaopimika.
Maadhimisho ya 15 ya Wahandisi
yaliyofunguliwa jana na Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi Balozi John
Kijazi na kufungwa leo na Katibu Mkuu (Sekta ya Ujenzi), Mhandisi Joseph
Nyamhanga yamelenga kuwakutanisha wahandisi kujadili kwa pamoja “Jukumu
la Sayansi, Teknolojia, Uhandisi na Hisabati katika Kukuza Viwanda kwa
Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi”,
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
No comments:
Post a Comment