TIMU ya Mpira wa Kikapu ya Savio
imekuwa mabingwa wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam kwa upande wa
wanaume (Dar e Salaam Stertimes RBA) kwa mwaka 2017 baada ya kuwachapa
mabingwa watetezi JKT Mgulani kwa pointi 88 dhidi ya 81 katika fainali
iliyopigwa jana kwenye uwanja wa ndani wa Taifa.
Fainali hiyo ilikuwa ni ya
shindano la 33 ambapo bingwa huyo mpya alikabidhiwa zawadi ya sh.
700,000 na Medali za Dhahabu huku JKT ambaye ni mshindi wa pili
akipatiwa sh. 500,000 na medali.
Aidha kwa upande wa kina dada
bingwa amekuwa ni Timu ya Vijana Queens. Imetwaa ubingwa huo baada ya
kuichapa Timu ya Donbosco kwa pointi 72 dhidi ya 69.
Kwa huo Vijana Queens pia
wamekabidhiwa kitita cha sh.700,000 na medali za Dhahabu huku Donbosco
wakikabidhiwa sh. 500,000 na medali.
Washindi wa tatu kwa pande zote
wamepatiwa sh.300,000 kila mmoja ambapo kwa wanaume ni Vijana City Bulls
huku kwa wanawake ikiwa ni JKT Stars.
Akizungumza katika hafla ya
kukabidhi zawadi kwa washindi Makamu wa Rais wa Kampuni ya StarTimes
nchini Zuhura Hanif, amesema kupitia udhamini wa RBA ni mwanzo wa kuwa
karibu na jamii kwa kuwapa vijana ajira kupitia michezo.
“Huu ni mwanzo wa kuwa karibu na
jamii, lakini pia kuwapa vijana ajira pamoja na kuwapa nafasi ya
kuonyesha vipaji vyao,” amesema Hanif.
Aidha ametoa wito kwa kampuni
nyingine ambazo zipo tayari kusaidia maendeleo ya mpira wa kikapu nchini
kujitokeza ili kusaidia vijana kupata ajira pamoja na kuonyesha vipaji
vyao.
Kwa upande wa ligi ya kikapu
daraja la kwanza Timu ya Kigamboni ndiyo mabingwa na kutokana na ubingwa
huo wamepanda katika Ligi ya Mkoa ya RBA katika msimu ujao.
No comments:
Post a Comment