Ndugu Waandishi wa habari;
Kwa mara nyingine tena
tunawakaribisha kwa mikono miwili katika mkutano huu muhimu. Karibuni sana huku
nikiwaomba mjione mko huru na mko nyumbani .
Dhana ya Demokrasia ni jambo muhimu
linalohitaji kuheshimiwa na kuenziwa ndani ya Chama na Jumuiya zake. Kiongozi
wa UVCCM mahali popote pale huchaguliwa kwa kufanyika uchaguzi huru na wa
haki unaozingatia Kanuni na Taratibu za Uchaguzi kama zilivyoagizwa na
vikao husika bila ya kukiuka, kupuuzwa au kuvunjwa.
Nia ya UVCCM ni kujenga na kudumisha
haiba njema ya kuendelea kuheshimu misingi ya demorasia ya kweli , yenye
kuchunga adabu na kufuata nidhamu, miiko na maadili kwa kila mwanachama
anayetaka kutumia haki ya kuchagua au kuchaguliwa.
April Mwaka 2017 Chama Cha Mapinduzi
kilianza mchakato wa Uchaguzi ndani ya Chama na Jumuiya zake. Kufuatia
mabadiliko ya Kanuni ya UVCCM yaliyofanyika mwezi Machi, 2017 tulianza Uchaguzi
katika ngazi za Matawi ambapo hadi leo jumla ya Matawi 23,529 sawa na Asilimia 99.4% kati ya Matawi 23,670
sawa na Asilimia 0.59% yamekamilisha uchaguzi.
Ngazi za Kata 3,913
sawa na Asilimia 96.59% kati ya Kata 4,051 sawa na asilimia 3.4% zimekamilisha
uchaguzi .Kwa upande wa majimbo ya Zanzibar majimbo 54 sawa na Asilimia
100%, wamekamilisha uchaguzi.
Ngazi ya Wilaya na Mkoa mchakato wa uchujaji wa majina kwa
Vijana waliomba nafasi mbali mbali ndani ya Jumuiya yetu , umeanza na
unaendelea vizuri huku jumla ya Vijana 7,606 wamejitokeza kuchuka fomu za
kugombea nafasi mbali mbali katka Jumuiya yetu, hali inayoonyesha kumekupo kwa
mabadiliko na msisimko wa kisiasa ukilinganisha na chaguzi zilizopita.
Kwa upande wa ngazi ya Taifa Vijana
350 wamejitokeza kuomba nafasi za uongozi ndani ya UVCCM kama ifuatavyo:-
(i)
|
Nafasi ya Mwenyekiti
|
113
|
Walioomba
|
(ii)
|
Nafasi ya Makamu Mwenyekiti Taifa
|
24
|
Walioomba
|
(iii)
|
Nafasi 5 za Wajumbe wa H/Kuu
|
103
|
Walioomba
|
(iv)
|
Nafasi 5 za Wajumbe wa B/Kuu Taifa
|
81
|
Walioomba
|
(v)
|
Nafasi 1 Wawakilishi UWT
|
14
|
Walioomba
|
(vi)
|
Nafasi 1 Wawakilishi Wazazi
|
15
|
Walioomba
|
Maandalizi kwa ajili ya Mikutano
Mikuu ya Wilaya hadi Taifa yanaendelea vyema ambapo chaguzi zote ndani ya UVCCM
zinategemewa kukamilika Novemba 2017.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi tunaendelea kusisitiza kuwa sifa na wasifu wa kila mgombea aliyeomba
kuteuliwa kwa kadri alivyojaza kwenye fomu yake, utaandaliwa na kuandikwa
vizuri katika kitabu maalum cha wagombea wote ambacho watapatiwa wajumbe wa
Mkutano siku ya uchaguzi husika.
Kila mgombea atapata nafasi ya
kujieleza na kutoa wasifu wake, kutaja dhamira na malengo yake mbele ya wajumbe
wa Mkutano Mkuu husika baada ya taratibu za vikao vya uteuzi kukamilika si
kinyume na hivyo.
Tunaendelea kuwakumbusha kuwa ni
mwiko kwa mgombea kuanza kampeni mapema au wapambe wake kufanya ushabiki
wa kisiasa kumnadi, kumpigia debe, au kujipitisha na kuelezea nafasi
anayogombea. Ukiukaji huo wa Kanuni na taratibu utampotezea sifa za kuteuliwa.
Aidha tunaendelea kuwasisitiza kuwa
ni marufuku na hairuhusiwi kabisa walioomba nafasi mbali mbali kuanza kufanya
kampeni za kihuni , kutumia lugha chafu, siasa za maji taka kuchafuana, matusi,
dharau kinyume na ubinadamu.
Kuyaacha hayo yote yafanyike bila ya
kuyadhibiti, kuyaasa na kuyakemea ni mwanzo wa kukaribisha mvurugano,
mgawanyiko hatimaye kujipenyeza kwa adui rushwa. Hivyo basi
tunaendelea kuwaagiza watendaji wote wa ngazi husika kusimamia matakwa ya
Kimaadili, Kikanuni na Kikatiba.
Aidha tunaendelea kuviomba
vyombo vinavyohusika katika ngazi zote hasa TAKUKURU kuendelea na
kufuatilia kwa karibu nyendo za wagombea na wapiga kura ili kubaini kuwadhibiti
na kuwachukulia hatua za kisheria. Mgombea au mpiga kura yoyote atakayethibitika
kutoa au kupokea Rushwa, hatua za kimaadili na kisheria tunaelekeza zichukuliwe
ili kulinda heshima ya taasisi yetu.
Tunaendelea kusisitiza kuwa uchaguzi
wa UVCCM katika ngazi zilizobakia zitafanyika kwa misingi ile ile ya uhuru na
uwazi huku kila mgombea akipitishwa na vikao vya kikanuni na kikatiba baada ya
kukidhi mashariti ya uchaguzi kwa mujiba kanuni na katiba.
Ndugu Waandishi wa Habari.
Katika siku za hivi karibuni
kumekuwa na malumbano yenye kupandikiza chuki na kupalilia mifarakano isio na
ulazima huku baadhi wa watu wakiwachafua wenzao kwenye mitandao ya kijamii na
wakati mwingine wapo wanaothubutu kuwatukana wenzao matusi ya nguoni kinyume na
ustaarabu, ubinadamu na misingi na Maadili ya Chama Cha Mapinduzi.
Wapo baadhi yao hujivika kofia ya
Jumuiya wakitumia njia hatari na batili, wamekuwa wakikebehi, kutuhumu
wenzao kinyume na utaratibu huku baadhi yao hata kufikia kutoa madai
yanayovuka mipaka na kubeba taswira ya Jinai au
madai.
Umoja wa Vijana wa Chama Cha
Mapinduzi umestushwa na hali hiyo inayoonekana kutaka kuibua migogoro na
kujenga mazingira yanayotaka kuonyesha kana kwamba ndani ya Jumuiya kuna
mvurugano au kuporomoka kwa mshikamano wetu wakati mambo nayo
hayapo.
Kimsingi yote yanayofanyika ni
kinyume na utamaduni wa Chama Cha Mapinduzi Kikatiba na Kikanuni na Kimaadili.
CCM si genge la wahuni bali ni Chama makini cha Siasa kinacho heshimu utu wa mtu, taratibu na miongozo iliyojiwekea
katika kushughulikia mambo yake.
Kwa miaka yote wanajumuiya na
viongozi wamekuwa wakiishi kwa kuzingatia misingi ya Umoja, Upendo, mashauriano
na kudumisha Maelewano.
Jumuiya yetu imekuwa ikifanya kazi
zake kwa uwazi na umakini mkubwa. Tusingependa kuona ikitiwa nyufa au kukumbwa
na athari za kutengenezwa na watu wachache. Nasema tena hatutasita kuchukua
hatua stahili kwa mujibu wa kanuni Katiba ya Chama na ikibidi hata kisheria ili
kukomesha vitendo hivyo vyenye nia ya kuondosha haiba nzuri ya Chama na Jumuiya
katika kufanya mambo yake ya msingi.
Tumeanza kuwafatilia kwa karibu mno
na kuanza kuwatambua wote ambao wanafanya au kushiriki vitendo hivyo vya aibu
aidha iwe kwenye Jumuiya au ndani ya Chama chetu
Chama Cha Mapinduzi na Jumuiya
zake hujadili mambo yake aidha yakiwa magumu au mepesi kwa mujibu
wa ajenda na njia za majadiliano kupitia vikao halali hatimaye
maamuzi hutolewa baada ya kujiridhisha.
Kimsingi utaratibu wa kushughulikia
mambo mbali mbali ndani ya chama na Jumuiya zake uko wazi.
Yeyote mwenye madai, tuhuma au
shutuma anatakiwa atumie vikao halali vya kikanuni na kikatiba ama
kuyafikisha kwa viongozi husika kwa kufuata utaratibu si kinyume na
hivyo.
Kwa kila mwana jumuiya muadilifu,
msemakweli, mpenda Umoja na Mshikamano, siku zote huheshimu kanuni, taratibu,
katiba na maelekezo yanayotolewa na viongozi wetu.
Ndugu Waandishi wa habari.
Nachukua nafasi hii kuwaasa na
kuwonya wale wote ambao pengine watakuwa wameteleza na kujikuta wakijielekeza
katika kushiriki vitendo hivyo vyenye muoneekano wa uasi , tunawataka
wajiepushe navyo hasa kipindi hiki ambacho tunaelekea katika Demokrasia ya
kweli ndani ya Jumuiya.
Narejea tena wapo tunaowajua
wakishiriki kufanya vitendo hivyo na kadri itakavyothibitika kwa
kukusanya ushahidi na vielelezo , hatua za kikanuni, kikatiba na pale
itakapobidi hatutasita kuchukua hatua za kisheria ili liwe funzo kwa wengine.
Tusingependa kuona watu wanajitwika
na kubeba agenda binafsi au kufikiria kumchafua mtu ndio kupata cheo ndani ya
Jumuiya yetu hakuna utamaduni huo haki na usawa itasimamiwa muda wote . Mtu
yeyote atayendeleza kufanya hivyo kwa kisingizio cha Uchaguzi wa Chama na
Jumuiya zake, mambo hayo hayakubaliki na hayatavumiliwa tena.
Ndugu waandishi Habari
Uchaguzi ni kipimo cha kupevuka na kielelezo
cha ukomavu wa demokrasia ya kweli bila mizengwe au hila ndani ya chama na
Jumuiya kwa lengo la kusimamia shabaha na misingi sahihi itokanayo na miongozo,
maelekezo na kuheshimu utaratibu unaohimizwa na Chama Cha Mapinduzi .
Ili kuonyesha kutii na kufuata
maelekezo yanayotolewa mara kwa mara na Mwenyekiti wetu wa CCM na Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Magufuli kila mwanachama
anapaswa kujitambua, kujiheshimu, kufuata misingi ya katiba na kulinda kwa
nguvu zake zote heshima ya Chama Cha Mapinduzi.
Ahsanteni sana na kila la heri.
KIDUMU CHAMA CHA MAPINDUZI
Shaka Hamdu
Shaka (MNEC)
KAIMU KATIBU MKUU
No comments:
Post a Comment