Thursday, September 7, 2017

SHAKA AZINDUA PROGRAMU YA USHIRIKISHWAJI KWA VIJANA DODOMA

Na Mathias Canal, Dodoma

Kaimu Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa CCM)  Shaka Hamdu Shaka (MNEC)  Septemba 7, 2017 Amezindua Programu maalumu kwa Vijana wa CCM katika ushiriki wa shughuli za miradi ya Kimaendeleo, Kiuchumi na Kijamii katika ukumbi wa CCM (NEC) Mjini Dodoma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Shaka alisema Wazo hilo limeibuliwa wakati muafaka huku serikali ya CCM awamu ya tano chini ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Pombe Magufuli ikiweka mkazo na vipaumbele kadhaa vinavyomtaka kila mtanzania hususani vijana kujituma, kufanya kazi kwa bidii na kuzalisha Mali.

Alisema dhana ya kufanya kazi kwa bidii, malengo na shabaha si ngeni lakini kwa wakati huu inahubiriwa kwa nguvu kulingana na changamoto nyingi zilizopo, fursa, ushirikishwaji kwa kuzingatia mahitaji halisi kutokana na mabadiliko ya dunia Kiuchumi na Kimaendeleo.

Aliwasisitiza Vijana kutambua wajibu wa kukuza shughuli za kazi na maisha zikiongozwa na nguvu ya uzalendo, kujali utaifa na kutambua dhamana iliyopo ya kudumisha amani, Umoja, Mshikamano na Maendeleo.

"Ili kusihi yote hayo hatimaye Vijana waweze kuyafanikisha tunapaswa kuwa na mioyo isiyopwaya au kukosa rutuba ya kutodumisha uzalendo, tunalazimika kwa pamoja kutambua mpango wowote wa kuyafikia maendeleo ya kweli utabaki ni hadithi na ndoto Kama hatutaongozwa na shime ya uzalendo au kutothamini utaifa wetu Kama ambavyo viongozi wanatuhimiza siku Hadi siku" Alisema Shaka

Shaka aliwaeleza Vijana kuwa pamoja na kuwepo juhudi kubwa za mara kwa mara kuchukuliwa na serikali, mashirika hiari ya Kijamii na yasiyokuwa ya kiserikali, kuelimisha juu ya dhana ya ushirikishwaji na ushiriki wa Vijana katika miradi ya Kiuchumi na Kijamii wanapaswa kuwa na utayari, uthubutu, uzalendo, na Utaifa.

Alisema kuwa Vijana wanapaswa kukubali kujadiliana na wenzao juu ya mpango wa maendeleo na hatma ya Taifa na mustakabali wake kwani ndiyo njia pekee ya kukuza uzalendo kwa Taifa.

Alisema mataifa yaliyoendelea yametokana na watu wake kukubali kufanya kazi kwani Ndiko kuliko yakomboa mataifa hayo yaliyoendelea kutoka katika uchumi duni na kuhamia katika uchumi wa Kati na Sasa wakionekana kuwa na uchumi wa maendeleo ya viwanda.

"Mafanikio hayakuja Kama zawadi kwenye kisahani Cha Chai ama kutokea kwa bahati mbaya Kama mtende unavyoota jangwani ni lazima kukubali kwa pamoja kufanya kazi ili kupambana na adui umasikini" 

"Wakati huu ambao serikali imebeba mzigo wa kutoa elimu bure toka msingi Hadi sekondari ni lazima Vijana tuwe na muktadha mmoja wa kujenga mtazamo wa pamoja kwa kujitambua na kukubali kufanya kazi bila kusukumwa" Alisema Shaka
 
Aliongeza kuwa kazi ya Vijana siku zote na kila wakati inapaswa kuwa ni kufikiri, kupambanua, kubuni na kujadiliana ili kumaliza changamoto, vikwazo, fursa na matumizi ya nafasi husika katika Jamii.

Aidha, kupitia kusanyiko hilo aliwaagiza na kuwataka makatibu wote wa Umoja wa Vijana wa CCM wa mikoa na Wilaya nchini kila mmoja kuhakikisha programu hiyo inaanzishwa katika mikoa na Wilaya zake na kusisitiza kuhitajika matokeo makubwa kwani ataandaa utaratibu wa kuthamini programu hiyo kila kipindi Cha robo mwaka.

Sambamba na hayo pia Kaimu  Katibu Mkuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi Ndg Shaka Hamdu Shaka alishiriki ujenzi wa shule ya Msingi Mizengo Pinda iliyopo katika Kijiji Cha Chinangali 2 Kata ya Bwigili Wilayani Chamwino.

Pamoja na kushiriki shughuli ya uchimbaji msingi, ufyatuaji tofali na matengenezo ya tungilizi kwa ajili ya upauaji wa majengo ya shule hiyo pia Shaka alichangia mifiko 20 ya saruji kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za wananchi walizozianza kwa kujitolea nguvu, muda na rasilimali zao.

MWISHO

No comments:

Post a Comment