Tuesday, September 12, 2017

WAZIRI LUKUVI ATOA MSAADA WA AMBULANCE JIMBONI KWAKE

Waziri wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi na mbunge wa jimbo la ismani Williamu Lukuvi akiwa kwenye gari la wagonjwa aina ya Toyota Land Cruiser alilokabidhi kwa halmashauri ya wilaya ya Iringa vijijini ambalo ni rafiki na mazingira kwa tarafa ya pawaga mkoani Iringa.
Waziri wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi na mbunge wa jimbo la ismani Williamu Lukuvi akiwa na mkuu wa mkoa wa Iringa Amina Masenza sambamba na mkuu wa wilaya ya Iringa Richard Kasesela wakitafakari jambo wakati wakukabidhi gari la wagonjwa kwa viongizi wa halmashuri ya wilaya ya Iringa vijijini
Huu ndio muonekano wa gari la kubebea wagonjwa lililokabidhiwa na waziri Lukuvi kwa ajili ya mahitaji ya kituo cha afya cha Idodi

Na Fredy Mgunda, Iringa

Waziri wa ardhi,nyumba na maendeleo ya makazi na mbunge wa jimbo la ismani Williamu Lukuvi ameendelea kuboresha sekta ya afya katika tarafa ya idodi kwa kuwapa gari la kisasa la kubebea wagonjwa linaloendana na mazingira ya tarafa hivyo kwa ajili ya matumizi ya kituo cha afya cha Idodi.

Gari hilo aina ya Toyota Land Cruiser lilikabidhiwa kwa uongozi wa halmashauri ya Iringa vijijini inayosimamia uendeshaji wa kituo cha afya cha Idodi katika mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Idodi tarafa ya Idodi.
Akikabidhi msaada huo Lukuvi alisema; “napenda ifahamike kwamba gari hilo limenunuliwa na familia ya Karimjee Jivanjee kwa ajili ya kuwasaidia wananchi wa tarafa ya Idodi na hiyo yote imetokana na uadilifu na uaminifu kwa serilikali ndio umetufanya tushirikiane vyema katika mambo mengi kwa faida ya wananchi wa jimbo langu la Ismani.”

Alisema gari hilo la wagonjwa ni rafiki kwa wagonjwa na wajawazito kwa kuwa lina vifaa tiba vinavyoweza kutumika kutolea huduma wakati wakipelekwa hospitalini.

Baada ya kukabidhi gari hilo, lukuvi ambaye ni mbunge wa jimbo la Ismani, mkoani Iringa alikumbusha vipaumbele vyake kwa wapiga kura wake kuwa ni kuhakikisha jimbo hilo linapata huduma bora ya maji, elimu, afya na miundombinu ya barabara.
MH Lukuvi aliwataka wananchi na viongozi kulitunza gari hilo ili litumike kwa muda mrefu kwa wamanufaa ya wagonjwa.

“Jamani gari hili ni rafiki na mazingira yetu hivyo naombeni tulitunze hili gari kadri tuwezavyo maana magari ya kubebea wagonjwa ni gharama kubwa sana hivyo ni lazima tuwe na uchungu wa vitu tunavyopewa kwa msaada”alisema Lukuvi

Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa iringa Amina Masenza alimshukuru waziri Lukuvi kwa kijihada anazozifanya kuboresha sekta ya afya katika jimbo la Ismani.
“Tuna wabunge wengi hapa nchi ila ni wabunge wachache sana ambao wanaokumbuka wananchi wao hivyo niendelee kumpongeza mheshimiwa waziri kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuleta maendeleo katika jimbo la Ismani na Iringa kwa ujumla” alisema Masenza

Akishukuru kwa msaada huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Iringa vijijini, Stephen Mhapa alisema kabla ya msaada huo, kituo hicho cha afya kilikuwa kina gari moja ambalo nalo lilikuwa limeharibia kutokana na kutokuwa na mazingira rafiki na barabara za tarafa hiyo.

Alisema kupatikana kwa gari hilo jipya kutasaidia kuboresha huduma hiyo kwa kuokoa maisha ya wagonjwa na maisha ya mama na mtoto ambayo ni kipaumbele katika utoaji wa huduma za afya.
Naye diwani wa kata ya Idodi Onesmo Mtatifikolo alisema atahakikisha inatekeleza ahadi mbalimbali zilizotolewa na Chama cha Mapinduzi (CCM), Rais Dk John Magufuli, mbunge na madiwani ili kuboresha huduma ya afya wananchi wa tarafa ya Idodi.
Nao baadhi ya wanachi wa tarafa ya Idodi walimpongeza waziri Lukuvi kwa msaada wa gari la wagonjwa pamoja na kuanza kutatua tatizo la wafugaji na wakulima kwa vitendo.

No comments:

Post a Comment