Na.Samuel Samuel
Mwezi juni mwakani kwa mara nyingine tena dunia itashuhudia michuano mikubwa zaidi kisoka iliyoanza zaidi ya miaka 80 iliyopita . Hii ni michuano ya kombe la dunia ambayo hufanyika kila baada ya miaka minne . Mwakani itafanyikia nchini Urusi .
Barani Ulaya, Latin America na Asia tayari wameanza kupata baadhi ya wawakilishi wao baada ya baadhi ya nchi kufuzu katika makundi yao tayari kwa michuano hiyo mwakani. Latin ni Brazil na Mexico tayari wamekata tiketi huku barani Ulaya ni Ubelgiji na wenyeji Urusi . Asia ni Iran .
Barani Afrika bado ni vita kali kuelekea michuano hiyo . Mwisho wa juma zimepigwa mechi mbalimbali katika harakati za kutafuta nafasi za kwenda Urusi.
Kundi A; Libya walifanikiwa kupata ushindi wao wa kwanza dhidi ya Guinea katika uwanja wao wa nyumbani wa Stade Mustapha Ben Jannet.
Waliwatandika Guinea 1-0 na kufanikiwa kupata alama tatu ingawa bado wanaburuza mkia kundi A wakiwa na alama hizo tatu huku Tunisia wakiwa kileleni na alama 9, DRC wanashika nafasi ya pili wakiwa na alama 6 lakini wakicheza mechi mbili tofauti na Tunisia waliocheza mechi tatu. Guinea nafasi ya tatu wakiwa na alama 3 sawa na Libya mkiani.
Mabingwa wa Afrika Cameroon baada yakula kichapo cha 4-0 jijini Lagos dhidi ya Nigeria ‘ super Eagles ‘ , jumatatu walijitutumua na kutoka sare ya 1-1 jijini Younde katika harakati hizo za kwenda Urusi.
Cameroon wanashika nafasi ya tatu kundi B wakiwa na alama 3 huku Nigeria wakiwa kileleni na alama 10 wakiwa na mechi mbili tu kukata tiketi ya Urusi. Wamebakiza mechi dhidi ya Zambia walio nafasi ya pili na alama 4 pia dhidi ya Algeria wanaoburuza mkia kundi lao wakiwa na alama 1. Kundi hili njia nyeupe kwa Nigeria kwenda Urusi.
Kundi C kuna Ivory coast waliopo kileleni na alama 7 huku Morocco wakishika nafasi ya pili kwa alama 5. Gabon wapo nafasi ya tatu wakiwa na alama 2 huku Mali wakiburuza mkia kwa alama 1. Timu zote zimecheza mechi tatu . Mchuano mkali hapa ni Ivory coast dhidi ya Morocco.
Kundi D linaongozwa na Burkinafaso wenye alama 5 kileleni , Senegal wanashika nafasi ya pili kwa alama 4, Afrika ya kusini nafasi ya tatu kwa alama 3 na Cape Verde wakiwa mkiani pia kwa alama 3. Hili kundi bado ni ngumu kwa timu zote kutokana kuwa na tofauti ya alama 1 mpaka 2 kwa aliyeko juu na mkiani sawa na mechi moja tu na timu zote zimecheza mechi tatu kila mmoja.
Kundi la mwisho ni kundi E ambalo linaongozwa na Uganda toka Afrika mashariki wakiwa na alama 7 . Misri wanashika nafasi ya pili kwa alama 6 na Ghana wakiwa nafasi ya tatu kwa alama 2. Congo-Brazaville wapo mkiani wakiwa na alama 1. Mtihani mkubwa kwa vinara wa kundi hili Uganda ni Misri ambao wanatofautiana nao kwa alama moja ingawa mafarao hao hawana rekodi nzuri ya kufuzu michuano ya kombe la dunia licha ya ubora wa soka lao Afrika nakuwa na rekodi nzuri ya kubeba kombe la AFCON . Misri wamewahi kufuzu mara mbili tu katika michuano ya kombe la dunia . Mwaka 1934 na mwaka 1990.
Huu unaweza kuwa mtaji mzuri kisaikolojia kwa Uganda kupambana vyema na kuweka rekodi yakuwa taifa la kwanza kutoka Afrika mashariki kufuzu kwa michuano hiyo mikubwa zaidi duniani. Tayari Uganda walitoa onyo kwa Misri katika mechi yao ya kundi hili baada ya kuwapiga 1-0 Nambole stadium Uganda kwa goli la Emanuel Okwi.
Bara la Afrika linatoa timu tano tu katika makundi hayo matano hivyo kila atakayemaliza wakwanza kwenye kundi ndio mwakilishi wa Afrika mwakani huko nchini Urusi.
No comments:
Post a Comment