Baadhi ya wajumbe wa kijiji cha Mkoyo pamoja na wataalam wa maji wa manispaa ya Dodoma wakati wa ziara ya kikazi ya Naibu waziri Ofisi ya Rais Tamisemi Selemani Jafo.
Naibu Waziri Ofisi ya Rasi, Tamisemi Selemani Jafo akisikiliza taarifa ya mradi wa maji Mkoyo
Jenerata ya mradi wa maji Mkoyo.
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Tamisemi Selemani Jafo amesikitishwa
na baadhi ya wakandarasi washauri wanaosimamia miradi ya maji katika
halmashauri mbalimbali hapa nchini kwa kutofanya kazi yao kwa umakini na hivyo
kuruhusu wakandarasi wa ujenzi wa miradi ya maji kujenga miradi hiyo chini ya
kiwango.
Jafo alitoa kauli hiyo alipotembelea mradi wa maji katika kijiji
cha Mkoyo ndani ya Manispaa ya Dodoma, ambapo amebaini mkandarasi mshauri wa
mradi huo O&A Co LTD hakuwa makini wakati wa utekelezaji wa mradi huo kwani
imeonekana mradi huo ukiwa na changamoto kadhaa licha fedha nyingi kutumika
zaidi ya milioni 430 kati ya milioni 480 zilizipangwa kwa mradi huo.
Amesema wakandarasi hao wamekuwa wakisababisha miradi kujengwa
chini ya kiwango na kusababisha kushindwa kuwapatia maji wananchi kama ilivyotarajiwa.
Aidha amebaini kampuni hiyo mshauri huyo ndiye yule yule
aliyesimamia mradi kijiji cha Itiso ambao
aliutembelea mradi huo mwezi Agosti mwaka huu na kukumbana na
changamoto nyingi.
Kufuatia hali hiyo, Jafo amemuagiza Mkurugenzi Msaidizi wa Ofisi
ya Rais Tamisemi Mhandisi Enock kwa shirikiana na wahandisi wa maji wa
halmashauri za mkoa wa Dodoma kufanya tathmini ya miradi yote ya maji
inayosimamiwa na mshauri huyo ili Ofisi ya Tamisemi ifanye maamuzi sahihi.
Aidha amesema serikali haitaweza kuvumilia endapo ikibainika mshauri
wa miradi hiyo ameshindwa kuisaidia serikali katika miradi ya maji anayoisimamia.
No comments:
Post a Comment