Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe(kulia) akimpongeza Balozi
wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking wakati alipowasili kwa ajili
ya kushiriki hafla ya kumuaga balozi huyo iliyofanyika katika mgahawa wa
Great Wall Jijini Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe akiongea na wageni
waalikwa pamoja na Viongozi mbalimbali waliohudhulia hafla ya kumuaga
balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking iliyofanyika katika
mgahawa wa Great Wall Jijini Dar es Salaam.
Balozi wa China nchini Tanzania,
Mhe. Lu Youking akiongea na wageni waalikwa pamoja na Viongozi
mbalimbali waliohudhulia hafla ya kuagwa kwake iliyofanyika katika
mgahawa wa Great Wall Jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Chama cha
Ushirikiano wa Urafiki baina ya Tanzania na China, Dkt. Salim Ahmed
Salim (kushoto) akimpongeza Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu
Youking mara baada ya kumalizika kwa hafla ya kumuaga balozi huyo
iliyofanyika katika mgahawa wa Great Wall Jijini Dar es Salaam.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-WHUSM)
…………………………………………………………………………………..
Na. Benedict Liwenga-WHUSM
Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt. Harrison Mwakyembe ametoa pongezi za dhati
kwa Balozi wa China nchini Tanzania, Mhe. Lu Youking kutokana na
utendaji kazi wake uliotukuka katika kudumisha ushirikiano baina ya
Tanzania na China hususani katika nyanja za masuala ya habari,
utamaduni, sanaa na michezo.
Pongezi hizo amezitoa hivi
karibuni wakati wa hafla ya kumuaga balozi huyo iliyowakutanisha baadhi
ya Viongozi wa Chama cha Ushirikiano wa Rafiki wa Tanzania na China
wakiwemo Waandishi wa habari.
Moja ya mambo makubwa muhimu
yaliyofanyika chini wakati wa kipindi cha Balozi Lu Youking ni tukio la
utiaji saini mwezi Machi mwaka huu ambapo Serikali ya Tanzania na China
zilitiliana saini Mkataba wa Ushirikiano wa Kiutamaduni wa Miaka mitatu
ambao utawapa fursa vijana 200 kutoka Tanzania kila mmoja kwenda China
kwa ajili ya kupata mafunzo katika nyanja mbalimbali za habari, sanaa na
utamaduni.
“Balozi Lu Youking umetuachia
zawadi kubwa sana sisi Wanahabari wa Tanzania, sasa hivi mimi na
wenzangiu Wizarani tunakamilisha utaratibu wa utekelezaji wa Mkataba huu
ili tuanze kuutekeleza mapema iwezekenavyo”, alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliongeza kuwa, Balozi Lu Youking
hivi karibuni ameshirikiana na Balozi wa Tanzania nchini China, Mhe.
Balozi Mbelwa Kairuki katika kuhakikisha kwamba Waandishi wa habari 10
kutoka Tanzania wanaondoka mwezi ujao kuelekea nchini China kwa ajili ya
kubadilishana uzoefu katika masuala ya habari.
Kwa upande wake Balozi Lu Youking
alisema kwamba, urafiki kati ya Tanzania na China umekuwa wa afya na
imara zaidi ya nusu karne akikumbushia kuwa, Baba wa Taifa Mwalimu
Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake aliwahi kusema kwamba,
Tanzania ina marafiki wengi, lakini China ni zaidi ndiyo maana Rais wa
China, Mhe. Xi Jinping alichagua Tanzania kuwa kituo chake cha kwanza
Afrika wakati wa ziara yake ya kwanza nje ya nchi tangu kuwa mkuu wa
nchi.
Aliongeza kuwa, kila mwaka zaidi
ya Wanafunzi 700 kutoka Tanzania huenda China kwa ajili ya masomo zaidi
na kutokana na hilo, matokeo ya ushirikiano wa China na Tanzania umekuwa
wa manufaa katika maeneo yote ya uchumi wa Tanzania na maendeleo ya
jamii na kwa kila maisha ya Mtanzania.
“Uhusiano wa China na Tanzania
umetoa mwongozo kwa Ushirikiano wa Kusini na Kusini yaani South-South
Cooperation, hivyo kutokana na maendeleo ya ushirikiano huu katika uwezo
wa uzalishaji kati ya China na Tanzania na mpango wa Ukanda mmoja njia
moja, tunaamini ushirikiano huu utakuwa na matunda zaidi”, alisema
Balozi Youking.
Urafiki baina ya Tanzania na
China ulianzishwa na Waasisi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Kikomunisti cha
China, Bw. Mao Tse-Tung (Mao Zedong) ambapo uhusiano baina wa nchi
hizi mbili kwa sasa umekuwa kwa kasi na kuleta maendeleo baina ya pande
zote mbili.
No comments:
Post a Comment