Monday, August 14, 2017

WAUGUZI ZANZIBAR WATAKIWA KUJIENDELEZA KIELIMU NA KUZIDISHA JUHUDI KATIKA KAZI ZAO

01
Mkuu wa Skuli ya Uunguzi  na Ukunga Chuo Kikuu cha Aga Mjini Nairobi Kenya Khan Prof. Sharon Brownie akizungumza na viongozi wa wauguzi na wakunguga wa Hospitali Kuu ya Mnazimmoja akisisitiza juu ya kuinua na kuimarisha kada hiyo kupitia Jumuia zao.
02 03
Mwenyekiti wa Jumuia ya Wauguzi na Wakunga Zanzibar Bi. Amina Abdulkadir akitoa ufafanuzi kuhusu Jumuia hiyo inavyofanyakazi na kusisitiza umuhimu wa wafanyakazi wa kada hiyo kujiendeleza katika mkutano huo uliofanyika Hospitali Kuu ya Mnazimmoja.
04
Mmoja wa viongozi wa wauguzi Bi. Salama Rashid Haroub akitoa mchango wake juu ya kuikuza kada ya uuguzi na ukunga Zanzibar.
05
Baadhi ya viongozi wa Wauguzi na Wakunga wakifuatilia mkutano mkutano huo uliohutubiwa na Mkuu wa Skuli ya wakunga na wauguzi kutoka chuo Kikuu cha Aga Khan Mjini Nairobi Kenya.
06
Picha ya pamoja ya viongozi wa wauguzi na wakunga wakiwa pamoja na Mwenyekiti wa Jumuia ya Wauguzi Zanzibar na wageni wao kutoka Chuo Kikuu cha Aga Khan Nairobi Kenya ambapo wamekuja Zanzibar kuinua kada ya wakunga na wauguzi.
Picha na Makame Mshenga.     

Na Miza Kona Maelezo-Zanzibar

Wauguzi na Wakunga nchini wamesisitizwa kuongeza bidii katika kuongeza taaluma  katika fani yao  kwa lengo la kutoa huduma kwa ufanisi wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Hayo yameelezwa leo huko Hospitali ya Mnazi Mmoja na Mkuu wa Skuli ya Wauguzi na Wakunga wa Chuo Kikuu cha Aga Khan nchini Kenya Profesa Sharon Brownie alipokuwa akizungumza na wasimamizi wa wauguzi  na wakunga wa Hospitali hiyo.

Prof. Sharon amesema wauguzi wana nafasi muhimu kwa jamii hivyo ni vyema kutafuta ujuzi kupitia sehemu nyengine kwa lengo la kukuza fani hiyo.

 “Asilimia 90 ya wauguzi duniani ni wanawake, wauguzi mnatakiwa kuangalia mitandao ya wauguzi ambayo inatoa taaluma ya uuguzi  kufanya hivyo mtaweza kubadilika kifanisi katika kazi hii ya uuguzi,” alieleza Profesa Sharon

Alifahamisha kuwa fani ya uuguzi inatakiwa kufanyakazi kwa kujituma na mashirikiano katika utendaji na utoaji huduma na kuweza kuinua afya kwa jamii.
 
Alieleza lengo la ziara hiyo ni kuinua na kuboresha Wauguzi pamoja na Jumuiya za Wauguzi kwa dhamira ya kuendeleza kitaaluma na kutekeleza majukumu ya kazi hiyo kwa ubora pamoja na kuimarisha afya kwa jamii.

Nae Mwenyekiti wa Baraza la Wakunga na Wauguzi Bi Amina Abdulkadir amewataka wasimamizi pamoja na wauguzi kufanya kazi kwa kujiamini, kujiheshimu pamoja na kubadilika kifanisi na kujua majukumu ili kuweza kutekeleza majukumu yao bila ya katawaliwa na kudharauliwa na wengine.

“Muuguzi anatakiwa  kufanya kazi kwa kujiamini, awe smati, ajiheshimu pia anatakiwa kubadilika kielimu sio awe regerege awe ni mwenye kufanya maamuzi  ndio mfanyakazi mwengine nae atamuheshimu, sisi tunataka wauguzi muwe juu zaidi katika fani hii,” alifahamisha Bi Amina.   

Aidha Bi Amina amewasisistiza wauguzi hao kuipenda kazi yao kwa lengo la kutoa huduma iliyo bora kwa jamii ili kuepukana na usumbu na malalamiko yanayotolewa na jamii.

Nao wauguzi hao walisema wanafanyakazi katika mazingira magumu hivyo  wanahitaji kupatiwa elimu na vifaa vya afya ili waweze kujiimarisha zaidi na kutoa huduma bora kwa jamii.

Aidha wauguzi hao walisisitiza kufanya utafiti katika kazi zao ili kuweza kujua na kupata sababu zinazoikumba jamii wakati wa utoaji huduma kwa lengo la kuimarisha afya na kuepukana na changamoto zinanajitokeza.

No comments:

Post a Comment