Na Mwandishi Wetu, Tunduru
Halmashauri ya wilaya ya Tunduru imetekeleza agizo la Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama Samia Suluhu Hassan la kila Halmashauri nchini kuanzisha jukwaa la uwekezaji wanawake kiuchumi,jukwaa hili litaunganisha wanawake kutoka kada tofauti tofauti na kutoa fursa za Uchumi, Biashara,upatikanaji wa mitaji, na kupitia sheria za nchi katika masuala ya Uchumi na jinsia ya kujitegemea kiuchumi.
Akizungumza na wanajukwaa mkuu wa wilaya ya Tunduru ambaye pia alikuwa mgeni katika uzinduzi wa jukwaa hilo Mh.Juma Zuberi Homera alisema jukwaa hili litawasaidia wananwake kujikwamua kiuchumi kwa watapata sehemu ya kusemea matatizo yao yanayowakabili na changamoto mbali mbali, pia jukwaa hili litawasaidia katika kupata mikopo ya asilimia tano kutoka halmashari kwani watapata sehemu ya kuweza kukutana na kupanga mipango ya uchumi, biashara na njia za kuweza kupata mikopo na kuongeza kipato kwa kimama.
Vilevile jukwaa la uwekezaji wanawake kiuchumi wilaya litakuwa na tija kwa kina mama kwa sababu litaongeza wigo wa kuweza kupata wakufunzi wa kutoa elimu ya ujasiriamali kwa kuwa watakuwa na chombo cha kuwaunganisha niwaombe viongozi wa jukwaa hili mtumie nafasi zenu katika kuleta mabadiliko katika wilaya ya Tunduru
Mh. Homera alisema kuwa "ili jukwaa hili liweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi linatakiwa kuwa mambo yafuatayo ikiwa ni pamoja na kufungua akaunti ya wanajukwaa, kuwa ofisi maalum ambayo shughuli zote za wanawake zitakuwa zinafanyika, kuwa na ushirikiano na halmashauri kupitia idara ya maendeleo ya jamii na kuwa na katiba au muongozo utakaozimamia utekelezaji wa shughuli zote za jukwaa".
Aidha aliwataka wanajukwaa kuwa na ushirikiano wa karibu na uongozi wa wilaya na wasisite kuomba ushauri kwani viongozi wako kwa ajili ya kuhakikisha wananchi wake wanafanikiwa kiuchumi na kufikia malengo ya serikali ya awamu ya tano ya kila mtanzania kuwa na maisha bora hadi ifikapo 2025, hivyo bila ya ushirikiano na kuwasaidia wananchi kujua na kuzifahamu fursa mbali mbali za kiuchumi serikali haitaweza kufikia malengo.
"Nimeanza kufanya mawasiliano na shirika la viwanda vidogo (SIDO) kuona uwezekano wa upatikanaji wa mashine za kurahisisha kazi kama kubangua korosho, kupukuchua nafaka kama mahindi, mbaazi, na ufuta kwa njia rahisi na kuepukana na utumiaji wa njia za asili ambapo mkulima anatumia nguvu na muda mwingi angali angeweza kufanya kazi nyingine za uzalishaji na kuongeza kipato"
Na kwa upande wa mbunge wa tunduru kusini Mh. Daimu Iddi Mpakate allisema kuwa umakini wa familia lazima uanze kwa mama kama akiwa legelege ataeweza kumsimamia mumewe hivyo kuwaomba kina mama kusimama imara katika jukwaa walilolianzsha na kuwa chanzo cha kuimarisha uchumi katika familia zao na kuongoza wanaume zao kwani serikali haitegemei mwanamke kuchukua mkopo na kwenda kumpa mumewe kuongeza mke mdogo bali kuanzisha biashara ambayo itawasaidia kujikwamua kiuchumi na kuondokana na hali ngumu ya maisha.
Alisema "sisi wabunge tuko tayari kuwaunga mkono na kwa kuanza tutahakikisha ofisi inapatikana pamoja na samani zake ili kuwezeshwa jukwaa hili kufanya kazi kwa wakati katika halmshauri yetu na niko tayari kwa kikundi chochote cha wanawake kitakachofika kuomba ushauri bila ya kujali wanatoka sehemu gani, naomba masuala ya kubaguana huyu wa huku na huyu wa kule tuyaache wanawake tuungane tuwe kitu kimoja"
Nao viongozi wa jukwaa la wanawake wakiongozwa na mwenyekiti mama Fatima Rajabu Mkina waliushukuru uongozi wa wilaya kuzindua rasmi jukwaa hilo kwani ni muda mrefu sana wamesubiri chombo hicho kwa kitambo sasa hivyo kuanzishwa kwake kutaongeza hamasa kwa wanawake kushiriki katika shughuli za uchumi, biashara, upatikanaji wa mitaji, na kupitia sheria za nchi katika masuala ya Uchumi na jinsia ya kujitegemea kiuchumi.
No comments:
Post a Comment