Kanisa
Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, limekataa kuendesha misa ya maziko ya
mfanyabiashara bilionea Faustine Mrema kwa madai hakuwa na Sakramenti ya
ndoa na mke wake wala kipaimara.
Paroko
Msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Theresia, Mtoto Yesu, Jimbo Kuu la
Arusha Padri Festus Mangwangi amekiri suala hilo na kuongeza kuwa
marehemu enzi za uhai wake hakuweka heshima na kanisa.
“Marehemu
ni mkatoliki wa kuzaliwa, lakini hakuwahi kuwa na sakramenti ya ndoa na
mke aliyezaa naye watoto wala kupata Kipaimara. Kanisa haliwezi kumzika
kabisa, kawaida mazishi ya Kanisa Katoliki ni heshima inayotolewa kwa
mhusika kama anastahili.
“Huyu
hakuwahi kufunga ndoa kanisani, alijitenga na kanisa kwa hiyo kusema
tumemtenga si kweli, yeye ndiyo alijikataa hakutaka kutafuta heshima
yake na kanisa akiwa hai,” alisema Padri Mangwangi.
Kuhusu
kutokwenda kwenye Misa za Jumuiya ambayo nayo ni moja ya taratibu
muhimu inayowataka waumini wa kikatoliki kushiriki ibada za nyumba kwa
nyumba Padri Mangwangi amesema, hata ibada hizo nazo pia marehemu
alikuwa hashiriki.
“Jumuiya
ni utaratibu wa kanisa unaowataka waumini wawe na ushirika wa karibu
ikiwamo kufahamiana marehemu pia alikuwa hashiriki kabisa sasa unaanzaje
kumzika mtu kwa heshima za Kanisa Katoliki?” amehoji Padri Mangwangi.
Wakati
Kanisa hilo likijivua kushiriki Misa ya heshima ya maziko ya marehemu
Mrema hiyo jana, Askofu Dk. Eliud Issangya wa Kanisa la Kimataifa la
Kiinjili, alilazimika kuongoza Ibada hiyo ya maziko iliyofanyika Hoteli
ya Ngurdoto, wilayani Arumeru.
No comments:
Post a Comment