Saturday, August 5, 2017

Kampeni za uchaguzi Kenya zatamatishwa kwa kishindo

media
Wafuasi wa vyama vya siasa nchini Kenya wakishangilia kwenye moja ya mikutano.

Kampeni za kuwania kiti cha urais nchini Kenya zimetamatika rasmi siku ya Jumamosi Agosti 5 kwa wagombea wa kiti hicho kumaliza kampeni zao wakiwataka wananchi wa wachague kuhudumu katika Serikali ijayo.

Vinara wawili wanaochuana vikali kwenye uchaguzi wa mwaka huu waziri mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga na rais wa sasa wa Kenya Uhuru Kenyatta, walimaliza kampeni zao katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto walimaliza kampeni zao kwenye kaunti ya Nakuru, eneo ambako wagombea hawa walikutana kwa mara ya kwanza na kukubaliana kuunda chama cha Jubilee, baada ya mwaka 2013 kuingia madarakani chini ya muungano wa vyama vya TNA na URP ambavyo baadae vimezaa Jubilee.

Wakiwa Nakuru vinara hawa waliwasihi wananchi wa wape nafasi nyingine ya kuongoza kwa kipindi cha miaka mitano wakijivunia rekodi nzuri ya hatua za kimaendeleo walizowaletea wakenya toka wameingia madarakani.

Rais Uhuru Kenya akiwa na mgombea mwenza wake William Ruto, Nakuru 5 Agosti 2017
Viongozi hawa wanasema ujenzi wa reli ya kisasa na uboreshaji wa bandari na kuimarisha miundombinu mingine kama barabara na mifumo ya elimu kunatosha kuwafanya wananchi kuwarejesha madarakani kwa miaka mitano.

Kwa upande wao muungano wa upinzani wa NASA wenyewe ulihitimisha kampeni zake jijini Nairobi ambapo vinara wa muungano huo wamewataka wafuasi wao kujitokeza kwa wingi siku ya Jumanne na kuwachagua ili walete mabadiliko kwenye taifa lao.

Kinara wa muungano huo Raila Odinga, amesema lengo lake ni kutaka kupambana na ufisadi na kuleta ahueni ya maisha kwa raia wa Kenya ambao wengi amesema wameendelea kutaabika kwa sababu ya Serikali ya Jubilee.

Vinara wa muungano wa upinzanik nchini Kenya, NASA, Raila Odinga na mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, Nairobi, 5 Agosti 2017

NASA inakituhumu chama tawala kwa kuiba fedha za uma na kujilimbikizia mali, huku wakitoa mifano kadhaa ikiwemo sakata la rushwa kwenye mradi wa vijana nchini Kenya NYS.

Wagombea wengine nao kama vile Mohamed Abduba Dida, John Ekuru Longoggy Aukot, Shakhalaga Khwa Jirongo, Japhet Kavinga Kaluyu, Michael Wainaina Mwaura na Joseph William Nthiga Nyagah, wamekuwa na kampeni za chini kwa chini wakiwashawishi wananchi wawachague wao badala ya Raila Odinga na Uhuru Kenyatta.

Uchaguzi wa mwaka huu unatazamwa kwa jicho pana na wananchi wa Kenya, nchi jirani na Jumuiya ya Kimataifa, ambapo baadhi yao wamekuwa na hofu ya kutokea machafuko licha ya Serikali kuwahakikishia wananchi kutakuwa na usalama wa kutosha.

Mwaka 2007 nchi ya Kenya ilitumbukia katika vurugu za mara baada ya uchaguzi ambapo maelfu ya wananchi walipoteza maisha baada ya Raila Odinga kukataa kutambua matokeo.

Chanzo:RFI

No comments:

Post a Comment