Thursday, August 31, 2017

DKT ANGELINE MABULA AVITAKA VIKUNDI VYA WANAWAKE NA VIJANA KUTUMIA VIZURI MIKOPO WANAYOIPATA

Mbunge wa Jimbo la Ilemela na Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe Dkt Angeline Mabula amevitaka Vikundi vya Vijana na Wanawake ndani ya Jimbo hilo kutumia vizuri fedha za mikopo wanazopewa ikiwemo kufanya shughuli za uzalishaji

Mhe Dkt Angeline Mabula ameyasema hayo mapema leo wakati wa zoezi la ugawaji hundi kwa vikundi vya kina mama na vijana zoezi lililofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya manispaa ya Ilemela na kushuhudiwa na kamati ya fedha ya manispaa hiyo ambapo amesema

‘…Ndugu zangu hiki kidogo mnachopewa mkifanye kama mbegu maana mbegu huwezi kupewa gunia zima utapewa kidogo ili ukazalishe, Sasa ukizalisha vizuri maanake ukija tena kurudia utapewa zaidi, Hivyo nawaomba hii mbegu mkazalishe vizuri msiende mkaiweka ikaoza , usiende ukaweka ikaharibika na usiende badala ya kuweka kwenye shamba lenye rutuba wewe ukapanda kwenye miamba nawaomba mkazitumie vizuri fedha hizi …’
Aidha Mhe Angeline Mabula amempongeza mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe Renatus Mulunga kwa namna anavyoisimamia manispaa yake katika kuhakikisha inatenga na kutoa mikopo hiyo kwa makundi ya Vijana na Wanawake.

Nae mwakilishi wa kikundi cha wanawake cha Agano Joshoni kutoka kata ya Buswelu Bi Jopines Bakebura amemshukuru Mbunge wa Ilemela Dkt Angeline Mabula na Uongozi wote wa Manispaa hiyo kwa kutekeleza lengo la Serikali katika kuwakwamua wananchi wake na kuahidi kuzitumia vizuri fedha hizo za mkopo sambamba na kurejesha kwa wakati.

Akihitimisha zoezi hilo Mkurugenzi wa Manispaa Ilemela John Wanga amemuhakikishia Mbunge huyo na wananchi wote kuwa ataendelea kutenga fedha hizo huku akiwaasa kurejesha mkopo kwa wakati ili kutoa fursa na kwa wengine kuweza kunufaika.

Vikundi vya Mshikamano kata Bugogwa, Tuinuane group kata Nyasaka, Muungano Kangaye A kata Nyakato, Wanakazi kata Nyamhongolo, Umoja ni nguvu kata Kitangiri, Twins Busenga kata Buswelu, Urafiki group kata Buzuruga, Umoja wa matawi kata Ilemela, Alfa na Omega kata Kahama, Amsha amsha Nzengo A kata Mecco na Agano Joshoni kutoka kata ya Buswelu vimenufaika na mkopo huo

‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga ’

Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
31.08.2017

No comments:

Post a Comment