Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na
Rais wa Jamhuri ya Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni jana tarehe 05
Agosti, 2017 wameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa bomba la
mafuta ghafi la Afrika Mashariki kutoka Hoima nchini Uganda hadi bandari
ya Tanga nchini Tanzania.
Sherehe
za uwekaji jiwe la msingi la mradi huo zilifanyika katika Kijiji cha
Chongoleani Wilayani Tanga na kuhudhuriwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia
Suluhu Hassan, Mke wa Rais Mhe. Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, Naibu wa
Pili wa Waziri Mkuu wa Uganda Mhe. Dkt. Ali Kirunda Kivejinja, Mawaziri,
Makatibu Wakuu, Wabunge na viongozi wa taasisi za Serikali za Tanzania
na Uganda pamoja na wakuu wa mikoa ya Tanzania.
Bomba
la kusafirisha mafuta hayo lenye urefu wa kilometa 1,445 ambapo
kilometa 1,115 kati yake zitajengwa Tanzania, litakuwa na uwezo wa
kusafirisha mapipa 216,000 kwa siku na ujenzi wake umepangwa kukamilika
mwaka 2020 kwa gharama ya takribani Shilingi Trilioni 8 za Kitanzania.
Bomba
hili litajengwa na kuendeshwa na kampuni za TOTAL ya Ufaransa, CNOOC ya
China na TULLOW ya Uingereza, kwa ubia na Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya
Uganda (UNOC) na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC).
Akizungumza
kabla ya kuweka jiwe la msingi Mhe. Rais Magufuli alimshukuru Mhe. Rais
Museveni na Serikali yake kwa kufanikisha mradi huo na amemhakikishia
kuwa Tanzania imejipanga kutoa ushirikiano wa kutosha pamoja na kuilinda
miundombinu ya mradi huo.
Mhe.
Rais Magufuli aliwataka wananchi watakaonufaika na ajira zaidi ya
30,000 zitakazozalishwa na mradi huo kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na
uaminifu na pia ametoa wito kwa wananchi wa Tanga na mikoa yote
itakayopitiwa na mradi huo kujipanga kunufaika na fursa mbalimbali za
biashara zitakazotokana na mradi huo.
Aidha,
Mhe. Rais Magufuli amekubali ombi la Mhe. Rais Museveni la Tanzania
kujenga bomba la kusafirisha gesi kwenda nchini Uganda kwa ajili ya
kusaidia uzalishaji wa chuma, na pia amemshukuru kwa kukubali kutoa
wataalamu waliogundua mafuta nchini Uganda kuja kushirikiana na
wataalamu wa Tanzania kwa ajili ya kufanya utafiti wa mafuta katika ziwa
Tanganyika na ziwa Eyasi magharibi mwa Tanzania.
"Kutoka
Msimbati Mtwara mpaka Uganda kuna kilomita 1422, kwa hiyo kuweka bomba
ambalo litapitisha gesi wakati hili lingine linapitisha mafuta,
inashindikana nini? Napenda kumuhakikishia muheshimiwa haya
yanawezakana, bomba la gesi lipite hapa kwenda Uganda, Kama wao
wametukubalia kwa nini sisi tushindwe, huu ndio ushirikiano wa Afrika
Mashariki , Tuwapelekee gesi wakafufue viwanda vyao vya chuma kule", alisema Rais Magufuli.
Kwa
upande wake Mhe. Rais Museveni amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa
utayari wake wa kutekeleza mradi huo, na amesisitiza kuwa Tanzania na
Uganda zinapaswa kushirikiana katika fursa zake mbalimbali ili kujenga
uchumi imara na kuboresha maisha ya watu wake.
Mhe.
Rais Museveni alitolea mfano wa mradi wa bomba la mafuta ghafi
litakalojengwa na kueleza kuwa mafuta yatakayozalishwa yataziwezesha
nchi hizi na nyingine za Afrika Mashariki kupata mafuta kwa gharama
nafuu na hivyo kuimarisha huduma za usafirishaji na viwanda, na pia
alisisitiza kuwa Tanzania iliyogundua gesi nyingi itaiuzia Uganda ili
iitumie kuzalisha chuma kingi na kukiuza Tanzania.
Mhe.
Rais Museveni pia alitoa wito kwa nchi za Afrika Mashariki kushirikiana
zaidi na kujipanga kukabiliana na changamoto ya uwiano wa kibiashara
usio na manufaa kwake, kutokana na takwimu kuonesha kuwa Jumuiya ya
Afrika Mashariki inauza kiasi kidogo cha bidhaa ikilinganishwa na bidhaa
zinazoingia kutoka nje.
Mhe.
Rais Museveni amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku 2 hapa nchini na
amerejea nchini Uganda, na Mhe. Rais Magufuli leo anaendelea na ziara
yake ya siku 5 hapa Mkoani Tanga ambapo atazindua kiwanda cha saruji cha
Kilimanjaro, ataweka jiwe la msingi la upanuzi wa kiwanda cha maziwa
cha Tanga (Tanga Fresh) na ataweka jiwe la msingi la ujenzi wa matanki
ya kuhifadhia mafuta katika eneo la Raskazone hapa Mjini Tanga
No comments:
Post a Comment