Monday, August 7, 2017

Dc Mtaturu azishauri Benki Kubuni Bidhaa Zitakazo Wavuta Masikini

unnamed
Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Miraji Mtaturu akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi tawi la NMB Ikungi.

MKUU wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Miraji Mtaturu ameyashauri mabenki ikiwemo NMB kubuni bidhaa zitakazowanufaisha Watanzania maskini ili kuondoa dhana inayowabaguzi ya kuwa “‘maskini sio rafiki wa taasisi za kifedha”. Mtaturu ametoa wito huo juzi wakati akifungua rasmi Tawi la Benki ya NMB Ikungi. Alisema kuendelea kuamini kwamba maskini sio rafiki wa mabenki, kundi hilo la Watanzania litaendelea kudidimia ndani ya lindi la umaskini.

“Kaeni muangalie kundi hili la watu maskini litanufaikaje na huduma zinazotolewa na mabenki ikiwemo ninyi NMB. Kundi hili la Watanzania maskini ili liweze kujikomboa kiuchumi, basi mabenki badala ya kutoa mikopo ya fedha taslimu, toeni mikopo ya mizinga ya nyuki, mabwawa ya kufungia samaki au kuku kwa ajili ya kufunga kibiashara”, alishauri Mtaturu.

Akisisitiza,mkuu huyo wa wilaya, alisema ili Mtanzania akiwemo maskini aweze kupata maendekeo ya kweli ni lazima ajiongeze kwa kupata mikopo kutoka kwenye taasisi za kifedha.

“NMB ninyi mnakwenda vizuri na mnakwenda na wakati. Mmeendelea kubuni bidhaa/huduma mbalimbali ambazo zimepelekea kuvutia Watanzania zaidi ya milioni mbili kufungua akaunti kwenye matawi yenu nchini kote”, alisema na kuongeza; “Sasa mmebuni akaunti ya FANIKIWA, ambayo inawalenga wajasiriamali wadogo wakiwemo baba/mama lishe na wauza chips. Hongereni sana”.
Meneja wa NMB kanda ya Kati, Straton Chilongola (wa tano kushoto) akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Ikungi vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi milioni tano vilivyotolewa na NMB.
Meneja wa Benki ya NMB Kanda ya Kati, Straton Chilongola akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi rasmi wa tawi la NMB Ikungi.

Mtaturu alisema sasa umefika wakati wa kuliangalia upya kundi la Watanzania maskini,ili na lenyewe liweze kushiriki kikamilifu kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati. Aidha, Mtaturu ametumia fursa hiyo kuwaalika wakazi wa wilaya ya Ikungi wahakikishe wananufaika kikamilifu na huduma mbalimbali zinazotolewa na tawi la NMB Ikungi.

“Najua wazi wakazi wengi wa wilaya yetu wameshindwa kunufaika na huduma za kibenki ikiwemo mikopo, kutokana na benki zote kuwa Singida mjini umbali wa kilometa 45. Sasa NMB imesongeza huduma karibu, tuitumie fursa hii kwa kupata mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji na kupanua kilimo kikiwemo cha alizeti”, alisema.

Katika hatua nyingine, mkuu huyo wa wilaya huyo,ametumia nafasi hiyo kuipongeza na kuishukuru benki ya NMB, kwa msaada wake wa vifaa tiba kwa kituo cha afya Ikungi vyenye thamani ya shilingi milioni tano.

“Naagiza vitanda hivi vitatu vya kujifungulia, vifaa vya kujifungulia, vitanda na magodoro mawili ya kupumzikia wagonjwa na mizani mbili, vitunzwe vizuri viweze kutumika kwa kipindi kirefu”, alisema.

Awali meneja NMB kanda ya kati, Straton Chilongola, alisema msaada huo wa vifaa tiba, ni mwendelezo wa NMB kuunga mkono serikali ya awamu ya tano katika kuboresha sekta ya afya. Alisema benki hiyo imeendelea kubuni bidhaa mbalimbali na zenye kuzingatia mahitaji halisi ya soko kwa wakati husika.

“Moja ya bidhaa hizo ni kampeni ya ‘FANIKIWA’ akaunti ambayo ni mahususi kabisa kwa wajasiriamali wadogo wadogo.Wajasiriamali hao ni pamoja na baba/mama lishe, wauza chipis, wenye maduka ya biashara yakiwemo ya nguo”, alifafanua Chilongola.

Akifafanua zaidi, alisema akaunti hiyo inampa fursa mteja kupata mkopo wa shilingi laki tano hadi shilingi 30 milioni. Pia meneja huyo, alisema wanayo akaunti nyingine ya ‘Wajibu’ ambayo ni mahususi kwa ajili ya watoto wenye umri wa miaka 0-18.

“Kwa upande wa teknolojia tuna akaunti ya ‘Chap Chap’. Akaunti hii mteja anaweza kufungua akaunti kwa muda mfupi na papo hapo kupata kadi yake ya ATM, na kuanza kufanya miamala wo wote”, alisema Chilongola.

Benki ya NMB, ina matawi zaidi ya 200 na mashine za kutolea fedha zaidi ya 700 nchi nzima. Ina wateja zaidi ya milioni mbili jambo linaloifanya kuwa benki pekee nchini yenye hazina ya wateja wengi kuliko benki zingine zilizopo nchini.

No comments:

Post a Comment