Na Mathias Canal, Dodoma
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Majaliwa K. Majaliwa Leo Julai 2, 2017 amezindua Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini uliofanyika Kwenye Ukumbi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliopo katika Chuo Cha Mipango Mjini Dodoma.
Katika Mkutano huo Waziri Mkuu amesema kuwa Baada ya kuanzishwa kwa TARURA hoja ya kutazama upya sheria ya Mfuko wa Barabara ambayo ilielekeza mgawanyo wa Asilimia 70 ya fedha za mfuko huo kwenda TANROADS na asilimia 30 kwenda kwenye Halmshauri sasa inajadilika hivyo zitumike taratibu zilizopo ili maamuzi yaweze kufanyika.
Amesema kuwa wakati taratibu hizo zikiendelea kusubiriwa Wakurugenzi wa Mamlaka za serikali za Mitaa kote nchini kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa utaratibu uliopo kwani tatizo yawezekana ikawa sio fedha Bali namna fedha kidogo iliyopo kutumika vibaya.
Mhe Mjaliwa alisema kuwa Uanzishwaji wa Wakala wa Barabara nchini ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015 iliyopo katika ukurasa wa 54 inayoielekeza serikali kuanzisha Wakala/Taasisi itakayosimamia kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za Halmashauri, Miji, na Majiji ambazo zipo chini ya TAMISEMI ifikapo mwaka 2020.
Amezitaja changamoto mbalimbali zinazozikabili mamlaka za serikali za Mitaa katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya miundombinu ya Barabara ambazo ni pamoja na Miradi kutekelezwa kwa viwango duni, Ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi kutokana na mipango isiyoridhisha, na Kandarasi kutolewa bila kuzingatia vigezo, uwezo na sifa.
Changamoto zingine ni pamoja na kutokuwepo kwa viwango vinavyoshabihiana vya ubora wa barabara Kati ya Halmashauri Moja na nyingine, Fedha zilizopangwa kutekeleza miradi ya barabara kutotumika kutokana na urasimu wa viongozi wa Halmashauti, Rushwa iliyokithiri katika utoaji wa zabuni, Mgongano wa maslahi na usimamizi hafifu wa mikataba ya ujenzi.
Mhe Waziri Mkuu alisema kuwa wakati serikali ikiendelea kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha TARURA inasimama imara na kutekeleza majukumu yake ni lazima pia menejimenti kujipanga vizuri ili nayo itekeleze wajibu wake kikamilifu
Alisema, Wakala huo utasaidia kuimarisha mtandao wa barabara za vijijini na hivyo kuwawezesha wananchi wengi zaidi kusafiri na kusafirisha bidhaa za mashambani kwa urahisi.
Katika Mkutano huo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Majaliwa K. Majaliwa alieleza manufaa yatakayopatikana kutokana na kuwa na Barabara za Vijijini na Mijini kuwa ni pamoja na kuongeza chachu ya uzalishaji Mali mashambani kutokana na urahisi wa kufikisha mazao sokoni, Kushusha bei ya vyakula mijini kutokana na gharama za kusafirisha mazao kutoka mashambani kupungua.
Mengine ni kuboresha na kubadili hali za kimaisha na kiuchumi kwa wananchi, kufanya maeneo mengi zaidi ya nchi kufikika kwa urahisi na hivyo kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na Kutoa ajira kwa vijana katika maeneo ambayo ujenzi au ukarabati wa miundombinu utakapokuwa unafanyika.
Mhe Majaliwa ametoa Rai kwa wadau wote wa barabara hususani waheshimiwa Wabunge na Madiwani kuusoma mpango huo, ili kuepusha malalamiko yasiyo na lazima kwa wakala huo mpya.
Aliongeza kuwa ni vyema Mipango kazi ya Wakala ikawa inapata mchango kutoka kwenye Halmashauri husika, ili matengenezo na Ukarabati uzingatie pia vipaumbele vya Halmashauri.
Imeandikwa na Mathias Canal, Mhariri Wazo Huru Blog, anapatikana kwa simu namba 0756413465
No comments:
Post a Comment