Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) umewataka wananchi wa Kata za Pamba na Maina zilzopo katika Manispaa ya Nyamagana kuitunza barabara inayojengwa na Serikali ili iwasaidie katika kuimarisha huduma zao za kijamii ikiwemo mawasiliano, kazi na biashara.
Pia Umoja huo umeeleza kufurshishwa kwake na ujenzi wa barabara hiyo inayotumia malighafi ya mawe toka kwenye miamba ya mawe na kuajiri vijana wengi katika ukandarasi wake Mkoani Mwanza .
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka aliposhiriki katika ujenzi wa barabara inayojengwa kwa kutumia mawe na mchanga yenye urefu wa kilomita 2.5 itakayagharimu jumla ya shilingi bilioni 1.5
Shaka alisema barabara huwaunganisha watu na kuwarahisishia upatikanaji wa mawasiliano, wepesi wa kuzifikia huduma muhimu za kijamii lakini pia hurahisha usafiri na usalama wa maisha ya watu.
Alisema Serikali za Chama Cha Mapinduzi hazitaacha kazi ya kuwatumikia na kuwahudumia wananchi wake kwasababu hilo ni sharti na jukumu la kimkataba kati ya wananchi na serikali walioiweka madarakani kikatiba na kisheria.
"Haya ndiyo mambo yanayohimizwa na Rais wetu, anataka vijana tufanye kazi, msiwe wategemezi au kushinda vijiweni, bila kufanya kazi huwezi kupata maisha bora, kazi yoyote ni kazi ilimradi iwe halali na yenye kulinda utu na heshima "Alieleza
Aidha Kaimu Katibu Mkuu aliwataka wananchi katika wilaya ya Nyamagana kuendelea kuamini Serikali yao abadan haitaacha kutimiza majukumu yake ya kimsingi kuwahuduma mahali popote.
Pia aliwakumbusha wenyeviti wa serikali za mitaa, madiwani na wabunge kuendelea kuwatumikia wananchi na kuwawakilisha vyema kwenye vikao vya baraza la madiwani ikiwa ni pamoja na kufuatilia miradi ya maendeleo.
Mbunge wa Nyamagana Stanslaus Mabula alimueleza Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM akiwa mbunge wa jimbo hilo, hataacha kutekeleza ilani ya uchaguzi ya ccm au kujitega na wajibu wa kuwatumikia wananchi.
Mabula alieleza kuwa amekuwa katika juhudi kubwa za kuharakisha utatuzi wa kero ya barabara hiyo na nyingine zinatatuka kwa uharaka ili wananchi wapate manufaa na kuweza kutumia fursa mbalimbali.
"Nimechaguliwa kuwa mbunge kwa tiketi ya ccm, walionipigia kura ni wananchi wa Nyamagana , mkataba wetu na wananchi ni kuwatumikia, kuwawakilisha na kutatua kero zinazowakabili kihuduma, kijamii na kiuchumi "Alieleza Mabula
Hata hivyo alisifu juhudi zinazofanywa na kaimu katibu mkuu wa UVCCM Shaka Hamdu Shaka katika kuuboresha na kuupa nguvu umoja huo kwa kufanya ziara nchi nzima kuwaamsha vijana na makundi mengine na kuitetea serikali kila inapobidi.
Shaka ameanza ziara katika wilaya ya Nyamagana baada ya kuhitimisha ziara yake katika halmashauri ya wilaya ya Manispaa ya Ilemela akitokea wikaya ya Ukerewe.
No comments:
Post a Comment