Na Mwandishi Wetu, Dar Es Salam
Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) umesema jumuiya ya Kimataifa haiwezi kumsikiliza Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad ili Tanzania inyimwe misaada ya kibinadamu kwasababu ya tamaa na udikteta wa kiongozi huyo anayekivuruga chama chake kwa kupigania maslahi binafsi.
Aidha Umoja huo umesisitiza kuwa ugomvi wa cuf hadi kufukuzana na kuvuana nyadhifa hakuna uhusiano wowote na serikali wala jumuiya ya kimataifa huku ukikitaka chama hicho kuheshimu katiba yake badala ya kumtafuta mchawi na kupiga ramli.
Msimamo huo umetolewa jana na kaimu Katibu Mkuu Shaka Hamdu Shaka ofisi kwake Upaga jijiiji Dar es saalam siku moja baada ya kumaliza ziara katika Mikoa ya Kigoma na Mwanza ilichukua takriban wiki mbili .
Shaka alisema Maalim Seif anapohusisha mtafaruku unaorindima ndani ya chama chake na serikali au jumuiya za kimataifa, ndivyo anavyozidi kuuthibitishia ulimwengu jinsi kiongozi huyo alivyo mwanasiasa mzandiki na msaliti kwa Taifa na maendeleo ya wananchi .
Alisema imekuwa ada na kawaida ya kiongozi huyo toka akiwa ndani ya SMZ na CCM kuichonganisha Tanzania na jumuiya za kimataifa ili aweze kuyafikia kirahisi malengo yake kisiasa hasa kwa kutamani kwake aukwae urais wa Zanzibar kwa gharama yoyote hata ikibidi watu kufa .
"Vitimbi na kedi za Maalim Seif si mpya za kutaka Tanzania inyimwe misaada, kama ni nyimbo basi anachokiimba sasa ni zilipendwa, amewahi kuzishawishi jumuiya za kimataifa ziinyime Zanzibar dawa na chanjo kwa watoto wachanga na kina mama wajawazito mwaka 1995, sasa anaiparamia serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kwa Rais Magufuli huyu atakwama "Alisema Shaka
Alisema si jumuiya ya kimataifa, serikali ya Jamhuri ya muungano au smz iliompa maelekezo Maalim Seif agombane na Mwenyekiti wake Profesa Ibrahim Lipumba hadi washindwe kutafuta muafaka na wala haijatoa agizo wafukuzane na kuvuana nyadhifa.
"Kama Maalim seif anataka jumuiya ya kimataifa iinyime misaada Tanzania kwa dai la kukosekana demokrasia, cuf ilipewa tunzo ipi ya zawadi kwa ukandamizaji wa haki na demokrasia unaoendelea ndani ya chama hicho, kama sababu Profesa Lipumba amewavua wabunge nyadhifa, Maalim Seif ametangaza nini kuhusu mbunge Magdalen Sakaya na wenzake "Alihoji Shaka
Pia kaimu katibu mkuu UVCCM alizishauri jumuiya ya kimataifa na nchi wahisani kumuuliza Maalim Seif wako wapi wenziwe alioanzisha nao chama tokea mwaka 1993 na kwanini abaki yeye peke yake madarakani huku akiwa mgombea wa kudumu wa chamaa hicho kwa miongo mitano bila kuwapisha wenzake.
Hata hivyo amewataka viongozi wa cuf kuacha maneno ya uzushi na utapitapi badala yake njia pekee sahihi kwao ni kuheshimu katiba yao kama ambavyo Msajili wa vyama vya siasa nchini anavyokishauri kiungwana chama hicho mara kadhaa .
"Hata kama watu wote Bara na Zanzibar watakufa kwa njaa, Maalim seif hana nafasi tena ya kuchaguliwa na wazanzibar awe Rais kwasababu si kiongozi kiungo na mfano bora wa aina ya uongozi unaofaa kwa wananchi wanaotamani kuishi kwa amani, usawa, haki na umoja "Alisema Shaka.
Vile vile mtendaji huyo mkuu wa UVCCM alieleza kuwa rekodi ya Maalim seif kisiasa na kiuongozi tokea akiwa smz na ccm, imejiandika kwa wino mbaya usiofutika, hivyo amejidhihirisha si mtu anayeweza kujenga mazingira ya umoja bali anaonekana kama kiongozi aliyejibebesha agenda hatari ya kuvuruga mustakabali wa ustawi wa amani kitaifa na kikanda .
"Maalim seif hawezi kutulia kama hajawa juu ya wenzake, hata kama atapewa utukufu wa kuishi kwenye mawingu hatakubali mpaka awe Rais wa Zanzibar, urais haupatikani kwa ndoto bila kuchaguliwa kwa kura , utachaguliwa vipi kama unakizuia chama chako kisishiriki uchaguzi "Alisema Shaka
Source: Uhuru
No comments:
Post a Comment