Waziri mkuu -Majaliwa
*Aagiza kuimarishwa kwa ukaguzi wa watu, magari na mizigo mipakani
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Tanzania siyo lango la kupitishia dawa za kulevya kwenda nchi za nje
hivyo ameagiza ulinzi uimarishwe katika mipaka yote.
Amesema kunatabia ya baadhi ya watu
wasiokuwa waaminifu kutumia Tanzania kama njia ya kupitisha dawa za
kulevya kwa ajili ya kupeleka nchi za Afrika ya Kusini, Malawi na
Zambia.
Alitoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi,
Julai 29, 2017) alipozungumza na watumishi wa kituo cha forodha cha
Kasumulu kilicho katika mpaka wa Tanzania na Malawi wilayani Kyela.
Waziri Mkuu alisema ili kuhakikisha
jambo hilo linadhibitiwa ni vema ukaguzi wa watu wanaopita kwenye maeneo
hayo pamoja na mizigo ukaimarishwa.
“Endeleeni kufanya upekuzi wa kina wa
magari, watu na mizigo yote yote katika mipaka yetu. Tanzania siyo lango
la kupitishia dawa za kulevya na Serikali haitakubaliana na jambo
hilo.”
Pia aliwataka viongozi hao kuhakikisha
biashara zote za magendo zinazifanyika mipakani, zikiwemo za kubadilisha
fedha zinadhibitiwa kwa kuwa zinaikosesha Serikali mapato.
Alisema ni vema yakawepo maduka ya
kubadilishia fedha katika maeneo hayo ili kudhibiti biashara hiyo ambayo
kwa sasa inafanywa kimagendo huku Serikali ikikosa kodi.
“Biashara za magendo zidhibitiwe katika
maeneo haya na yaanzishwe maduka ya kubadilishia fedha ili biashara hiyo
ifanyike kihalali. Pia imarisheni vyanzo vya mapato.”
Pia Waziri Mkuu aliwataka Maofisa wa
Uhamiaji katika mikoa hiyo ya mipakani kuhakikisha wanadhibiti uingiaji
holela wa raia wa kigeni kwa lengo la kuimarisha ulinzi nchini.
Waziri Mkuu alisema katika baadhi ya
maeneo kwa sasa zimeanza kuonekana silaha ambazo hapo awali hazikuwepo
na ndizo zinazosadikiwa kutumika katika matukio ya kihalifu.
Awali, Bw. Taniel Magwaza ambaye
ni Afisa Mfawidhi wa Uhamiaji alisema watahakikisha wanafanya kazi kwa
weledi katika kupambana na biashara za magendo kwenye mpaka huo.
Alisema mbali na kupambana na biashara
za magendo pia watadhibiti uingiaji wa wahamiaji haramu kwa kushirikiana
na watumishi idara zote waliopo katika mpaka huo wa Kasumulu.
Bw. Magwaza alisema katika doria
zilizofanywa mwaka 2016/2017 jumla ya wahamiaji haramu 87 walikamatwa na
kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
Alisema wahamiaji hao walitokea nchi za
Malawi (30), Ethiopia (47), Burundi (6) Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo
(DRC) (4), ambapo baadhi walirudishwa makwao na wengine walifungwa
katika Gereza la mkoa wa Mbeya.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, JULAI 30, 2017
No comments:
Post a Comment