Wednesday, July 5, 2017

MHE PAUL MAKONDA AKABIDHIWA ZAWADI YA GARI DOUBLE CABIN WINGLE 5

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe. Paul Makonda leo asubuhi amekabidhiwa zawadi ya gari aina ya Double Cabin Wingle 5 kutoka kwa kampuni ya watengenezaji wa magari ya Great Wall Motor ya Afrika Kusini ikishirikiana na kampuni ya wauzaji wa magari ya Kifaru Motors ya Tanzania. 

Akiongea katika makabidhiano hayo Mkurugenzi wa Great Wall Motor Company ukanda wa kusini mwa Afrika Bwana Jianguo Liu alisema kuwa zawadi hiyo ni ishara ya kampuni hiyo kutambua jitihada mbalimbali za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na watumishi wake wanazofanya katika kutumikia wananchi na kusaidia kuboresha utendaji kazi. 

Katika salamu za shukrani Mhe. Paul Makonda aliushukuru Uongozi mzima wa  Kampuni ya Great Wall Motor ukishirikiana na wauzaji wa magari ya Kifaru Motors kwa kutambua jitihada za Ofisi yake na kuahidi kuendelea kuwatumikia wananchi wa Mkoa wa Dar es Salam kwa moyo na kutimiza falsafa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli ya “HAPA KAZI TU”. 

Mkuu wa Mkoa ameahidi kuwa gari hilo litatumika ipasavyo katika kuwahudumia wananchi wa Dar es Salaam na kutumiwa na Idara itakayoonekana kuwa ndio mtoa huduma bora katika Mkoa wa Dar es Salaam. 

“Naomba kuitoa hii gari kama zawadi kwa Idara inayohudumia vizuri wananchi wangu na ili nitoe kwa Idara hiyo naomba wananchi wenyewe watutumie kwa ujumbe mfupi kupitia namba tutakayoitangaza. Kazi ya wananchi ni kusema tu Idara hii inawahudumia vizuri wanapofika kwenye ofisi zao,kama ni Afya,Elimu,Ardhi,Biashara,na Mahakama”. Aliongeza Mhe. Paul Makonda. 

Kwa mfano kama ulienda Idara ya Elimu, Ardhi, Afya, au Biashara ukapewa huduma nzuri katika eneo mojawapo kati ya hayo unachotakiwa kufanya ni kutuma mesesji fupi inayoonyesha Idara hiyo ili wapewe zawadi hiyo ya Gari kama motisha ili waendelee kutoa huduma nzuri. 

Utaratibu wa kutuma ujumbe huo wa kuchagua Idara bora katika utendaji utatolewa kupitia namba maalum ambayo itatolewa hapo baadae. 

Imetolewa na:-
Kitengo cha Habari na Uhusiano
OFISI YA MKUU WA MKOA
 DAR ES SALAAM
05/07/2017

No comments:

Post a Comment