Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula leo amefanya ziara ya kiutendaji kufuatilia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali juu ya masuala ya Ardhi, kutembelea mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zinazojengwa na shirika la nyumba nchini NHC kata ya Buswelu, kuzungumza na wataalamu wa ardhi wa wilayani humo na kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero za Wananchi juu ya Ardhi katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya Sekondari Bwiru
Akizungumza katika ziara hiyo Mhe Dkt Angeline Mabula ameitaka Manispaa ya Ilemela kuwachukulia hatua watu wote wasiofanya maendelezo ya ardhi na kuongeza kasi katika ukusanyaji wa kodi huku akiwaasa wananchi kuhakikisha hawabweteki tu na zoezi la urasimishaji bali wanapata hati miliki za maeneo waliyonayo sanjari na kumuunga mkono kwa vitendo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt John Magufuli kwa kutekeleza maagizo yake, kufichua na kuvipinga vitendo vyote viovu
'Mhe Rais Magufuli kazi anayoifanya ni kubwa katika mambo yote anayoyafanya hatutakiwi kuishia kusema mdomoni tunatakiwa kumuunga mkono kwa kutekeleza yale yote anayoyasema hakuna vita mbaya kama ya kiuchum,i Sisi Ilemela tuna rasilimali ya Ziwa alafu tunaruhusu watu wanavua kwa sumu, kwa baruti tunanyamaza tu, Vita hii inahitaji watu wote tuwe pamoja, Najua zipo jitihada na hatua zinazochukuliwa lakini niwaombe wafichueni wote wanaofanya maovu yale yanayoendelea kibiti tutayasikia kwenye maeneo yetu kama tutaendelea kukaa kimya’ Alisema
Kwa upande wake Kaimu mkuu wa wilaya ya Ilemela Mhe Mwalimu Hadija Nyembo amemshukuru Naibu Waziri huyo kwa kufanya ziara ya kikazi katika wilaya yake mbali na kuwa Mbunge wa Jimbo hilo na kumhakikishia kuyasimamia na kuyatekeleza maelekezo yote aliyoyatoa kupitia ziara hiyo.
Aidha Ziara hiyo pia imehusisha wataalamu wa ardhi kutoka Wizara ya Ardhi, Ofisi ya ardhi kanda Ziwa, Shirika la Nyumba la Taifa Mkoa Mwanza, Msaidi wa Katibu Tawala Mkoa Mwanza, Mstahiki Meya Renatus Mulunga na Mkurugenzi wake wa Manispaa ya Ilemela John Wanga
‘ Ilemela ni yetu, tushirikiane kuijenga’
Imetolewa na
Ofisi ya Mbunge
Jimbo la Ilemela
26.07.2017
No comments:
Post a Comment