Monday, July 31, 2017

MHE MWIGULU AKEMEA SIASA ZA ULIMBUKENI

Na Friday Simbaya, Iringa

Waziri wa mambo ya ndani ya nchi, Mwigulu Lameck Nchemba amesema Tanzania bado kuna ulimbukeni wa demokrasia kwa kubaguana katika misingi ya vyama vya siasa.

Mwigulu alitoa kauli hiyo jana (JUMAPILI) wakati akitoa salamu za serikali katika ibada maalum ya kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa kanisa la kiinjili la kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Mlandege katika Manispaa ya Iringa, mkoani Iringa. 

Alisema kuwa bado anashangaa kuona watu wanabaguana kwa itikadi ya vyama pamoja na siasa ya vyama vingi nchini kudumu kwa miaka zaidi ya 20 sasa.

“Inatakiwa watu tuwe tunataniana kama tunavyotaniana kwenye mpira na ndugu yangu DC Kasesela kuhusu Singida united na Lipuli FC au mpira wa Yanga na Simba…,” alisema Mwigulu.

Mwigulu aliambatana na mwenyeji wake Richard Kasesela ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa.

Aidha, ibada hiyo iliongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Iringa Blaston Tuluwene Gaville akisaidiana na mchungaji kiongozi Rhodeni Mang'lisa. 

Pia ibada hiyo ilikwenda sambamba na changizo (harambee) kwa ajili ya ujenzi wa kanisa unaoendelea wa Usharika wa Mlandege, ambapo Mwigulu alichangia shilingi milioni tano na kuahidi kutoa bati 600 kwa kuezekia kanisa hilo.

DC Kasesela na pia alichangia pesa taslimu shilingi milioni moja kwa ajili ya ujenzi wa kanisa hilo unaondelea.

Alisema kuwa anashangaa kuona bado watu wanafanya siasa za kishamba katika misingi ya vyama vya siasa na kuongeza kuwa huku nikuonesha kwamba Tanzania demokrasia bado haijakomaa.

“Watu wanauana kwa sababu za vyama vya siasa kumbe walitakiwa kufanya kazi kwa pamoja kama ndugu wa taifa moja lakini sio kutoana roho kwa misingi ya vyama, huo ni ushamba wa kidemokrasia…,” alisema Mwigulu. 

Mwigulu alisema kuwa waumini wa madhehebu ya dini mbalimbali wanawajibu mkubwa wa kuwa pamoja na wakati wote kwa kumuombea dua na sala rais dkt John Pombe Magufuli kila siku ili aweze kufanikiwa.

Naye mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa kanisa Boas Danford alisema kuwa wanahitaji zaidi ya shilingi milioni 75 kukamilisha ujenzi huo, ambapo tayari wameshatumia shilingi milioni 78,468,000/-.

Alisema kuwa kanisa hilo litakuwa ni la ghorofa moja lenye uwezo la kubeba washarika jumla ya 1,100 pamoja na ofisi za usharika ndani yake.

Danford alisema hadi kukamilika kwa ujenzi huo litagharimu shilingi milioni 350/- na kuongeza kuwa tangu kuanza kwa ujenzi huo hakuna msaasa wowote kutoka nje isipokuwa ni michango mbalimbali kutoka kwa washarika.

Aidha, Usharika wa Kanisa la Mlandege lilianzinshwa mnano 24.10.1983 ikiwa na washarika 120 tu lakini washarika wameongeza na kufikia 1,950, ambalo kwa sasa kanisa hilo linaongozwa na mchungaji kiongozi Rhodeni Mang’ulisa.

Hadi tuanenda mitamboni mchango na ahadi ziliendelea kutoa na wageni waarikwa na waumini mbalimbali ambapo pia Askofu wa Dayasisi ya Iringa naye aliahidi kutoa shilingi milioni one na elfu ishrini.

Mwisho

No comments:

Post a Comment