Friday, June 23, 2017

UMOJA WA WAZEE MFUKO WA MAENDELEO KATA YA NYAMUSWA WAMPA HEKO RAIS MAGUFULI

UTANGULIZI

Kata ya Nyamuswa ipo katika Mkoa wa Mara  Wilaya ya Bunda Tarafa ya Chamuriho.

Nyamuswa ipo upande wa Mashariki mwa ziwa Vikitoria na Magharibi mwa mbuga ya Serengeti. Imepakana na Wilaya ya Butiama upande wa kasikazini na upande wa kusini imepakana na kata ya Nyamang’uta.

Umoja wa Wazee Mfuko wa  Maendeleo Kata ya Nyamuswa,  ulianzishwa mwaka 2011 Ukiwa na wanachama 50, Umesajiliwa kisheria na kutambuliwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, pia una  akiba maalumu benki.  Umoja huu umetokana na chimbuko la umoja wa watu wa eneo la Ikizu uliokuwapo zamani  wakati huo likitawaliwa na  Chief Mohamed Makongoro kabla ya uhuru mwaka 1961.

Umoja huu umesimama na kufanya kazi zake vizuri  zinazohusu Maendeleo ya eneo la Ikizu na wilaya yote baada ya vijana na Wazee wa eneo hili kukaa na kuona umuhimu wa kufufua umoja huu, waliazimia  kuchangia maendeleo na kusimamia maadili katika eneo letu,Ikumbukwe eneo letu la Nyamuswa linabeba taswira kubwa ya eneo la Ikizu, hivyo tunawajibika kuisaidia jamii kuenzi historia ya eneo hili.  

Lengo kubwa la Umoja huu ni kuchangia Maendeleo na ustawi wa jamii,Tumekuwa msitari wa mbele katika kuishauri jamii kuhusu maendeleo na maadili ya kuwatumikia watu katika Kata, Tarafa, Wilaya,Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Umoja huu kwa kushirikiana na wadau mbalimbali tumefanikiwa kutatua baadhi ya changamoto katika Kata, Tarafa na Wilaya.  Mathalani mwaka 2011 tulitengeneza madawati 260 yenye thamani ya million kumi na nane (18,000,000)  na kuyagawa shule zote za msingi katika kata ili kuchangia jitihada za serikali katika Elimu kama wadau muhimu na wazazi, Mwaka 2014 tulinunua Motor ya Maji yenye thamani ya sh million kumi na nne (14,000,000/=) kwa ajili ya kutoa maji katani, Mwaka 2015 tulifanikiwa kusimika jokofu la kuhifadhia maiti(mortury) lenye thamani ya sh Million ishirini na sita (26,000,000/=)  na tulilikabidhi serikali katika kituo cha Afya Ikizu – Nyamuswa na Mwaka 2016 tulichangia Harambee zaidi ya sh Million ishirini (20,000,000/=) kwa ajili ya uanzishwaji wa Makongoro High School.

*TAMKO RASMI LA KUMPONGEZA MH. RAIS JOHN POMBE JOSEPH MAGUFULI KWA HATUA YA UJASIRI YA KULINDA RASILIMALI ZA NCHI YETU.*

Sisi Umoja wa Wazee kata ya Nyamuswa, tukiwawakilisha Wazee wa Ikizu tunakupongeza Mheshimiwa Rais John Pombe Joseph  Magufuli kwa ujasiri wa uamzi mkubwa na mgumu wa kujitoa mhanga kutetea Rasilimali za nchi hasa *Madini.*

Tunatambua kuwa, haikuwa kazi rahisi kufikiri na kuamua kuchukua hatua ya kuzuia usafirishaji wa Makontena ya *Makinikia* yaliyokuwa yakisombwa  kiholela na kinyemela na wezi wa nje ya nchi kwa jina la wawekezaji huku wakisaidiwa na watanzania wachache wasio waadilifu.

Tunatambua kuwa haikuwa kazi rahisi ya kuchukua uamuzi wa kuunda Kamati ya Wataalam wa Miamba na Madini na Kamati ya Uchumi na Sheria ili kupata ukweli.
Sisi Wazee wa Ikizu tunatambua kuwa vita hii uliyoianzisha wewe Mheshimiwa Rais hapa Tanzania sio ndogo dhidi ya Mabepali wa kiuchumi duniani. Tunajua vita hii  ni vita ya ukombozi wa pili wa Nchi yetu ili kujikwamua kiuchumi.

Sisi Wazee wa Ikizu, sehemu ya Tanzania, Tunakupongeza kwa namna ulivyo jitofautisha katika utendeji wako kwa kugusa maisha ya wanyonge katika nyaja mbalimbali tangu umekuwa Rais Oktoba 2015.
Sisi tunakuunga mkono kwa kuwa umegusa *KIU* ya Watanzania ya kulinda Rasimali zao dhidi ya majangili na waporaji wasio na aibu kwa jina la wawekezaji, Umedhihirisha kuwa wewe ni KIJANA Mzalendo wa  Nchi hii jina lako litakumbukwa Vizazi na Vizazi kama mtangulizi wa Taifa Mwalimu JULIUS KAMBARAGE NYERERE.

Sisi wazee wa Ikizu, kwa umoja wetu tunakuunga mkono kwa kazi hii uliyoianza ambayo baadhi yetu wasio na aibu walijaribu kutisha kwamba tutawekewa vikwazo Duniani na kushitakiwa katika Mahakama za Kimataifa lakini wamepatwa na aibu baada ya hao waporaji kutubu na kukubali kulipa wizi wote waliotusababishia.

Sisi Wazee wa Ikizu – Nyamuswa tunakuombea Afya, Uwezo na Hekima zako ziongezeke maradufu katika kusimamia Nchi. Hakika tunaona  *DIRA* ya Nchi kupitia wewe kwa huduma tunazopata na Dunia nzima inavyotusifu sisi kama Tanzania.

Sisi Wazee wa Ikizu tuko nawe bega kwa bega, Usiogope, Kivuli chetu kiko nyuma yako *“ Our shadow is next to yours”* na Mungu yuko juu yako atakulinda kwa kila jambo uiongoze nchi salama.

Eneo letu hili la Ikizu linakubariki na kukukaribisha ututembelee ujionee Historia ya baraka tulizozitoa kwa watangulizi wenzako enzi na enzi, Sisi wazee wa Ikizu ndiyo tuliyo msaidia Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kuanza kutengeneza katiba ya TANU kupitia *Chifu wa Waikizu Mohamed Makongoro Matutu.*

Sisi Waikizu ndiyo tuliyemtolea ushahidi Mwalimu Nyerere kwa kesi ya mkoloni ya uchochezi na uanzishwaji wa chama cha Siasa na tukashinda.

Sisi Wazee wa Ikizu ndiyo tuliochonga  *FIMBO*ya Mwalimu Nyerere aliyokuwa akitembea nayo kote Duniani,   Fimbo hii hutolewa kwa watu Maalumu walifanya mambo makubwa na uongozi unaokubalika.

Sisi Wazee wa Ikizu leo tunajivunia kukuunga mkono kwani hata waanzilishi kumi (10) wa mwanzo wa chama cha TANU wanne  walitoka eneo letu la Ikizu hao ni *Mzee  Kisung’uda Kapera, Abubakari Iranga, Suleman Kitwara na Kibiriti  Miyasi.* Hawa waliazisha TANU na kumsaidia Mwalimu Nyerere kuongoza Chama na baadaye kupata uhuru 1961.
Kupitia historia hiyo ya eneo letu la Ikizu, nasi leo tunakuunga mkono Rais wetu uendelee kupambana na wahujumu Uchumi, Mafisadi, Wala rushwa , Wavivu na wasiopenda maendeleo ya nchi yetu. Hakika tumeona utaacha historia kubwa katika PAJI la nchi yetu.

Tunakupongeza sana kwa hatua na mafanikio uliyofikia ya kulinda Rasilimali za Nchi yetu, Penya kila kona uokoe na mengine mengi ambayo kama nchi tuliyapuuza ili hali ni mambo muhimu kwa ustawi wa watu wote.

Hongera sana wewe *Rais, Makamu wa Rais, Waziri mkuu na timu yako ya kazi* kwa kasi na umakini wa uongozi, Uzalendo na ujasiri mlionao katika kuijenga nchi yetu. Endelea, Usiogope, Usirudi nyuma sisi tuliokuchagua tupo na tunakuunga mkono.

KARIBU IKIZU, Uone eneo ambalo Mwalimu Nyerere alitumia kukaa na kuandika KATIBA YA TANU, Uone wazee waliochonga fimbo ya Mwalimu Nyerere na  uone historia ya Wazee wapenda maendeleo na jitihada za kuunga juhudi za maendeleo.

Pokea zawadi ya *FIMBO* ishara ya upendo wetu na ishara ya kukubalika kwa uongozi wako.
Mungu akubariki sana Mheshimiwa Rais wetu, Akupe afya njema, Hekima na uwezo wa kuongoza Nchi salama salimini.

*IMEANDALIWA NA UMOJA WA WAZEE MFUKO WA MAENDELEO KATA YA NYAMUSWA*– *IKIZU*
*BUNDA*, *MARA.*
*23/06/2017*

No comments:

Post a Comment