Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo imeanza kusimamia zoezi la ushushaji wa Mabango ambayo hayajalipiwa katika maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa.
Akizungumza wakati wa Oparesheni ya kushusha Mabango Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi Kayombo alisema kuwa Leo June 29, 2017 amesimamia zoezi hilo la ushujaji wa Mabango ambayo hayajalipiwa yaliyopo katika maeneo mbalimbali ndani ya Manispaa ya Ubungo lengo ikiwa ni kuwakumbusha kwa njia ya vitendo wadaiwa hao ambao wamefunga masikio kwa kipindi kirefu.
MD Kayombo alisema kuwa ofisi yake ilishapeleka madai hayo kwa zaidi ya mara moja huku kesi zikifikishwa mahakamani ambapo baadaye zilitolewa kwa ajili ya mazungumzo ya maridhiano kufanyika ambapo hata hivyo pomoja na mazungumzo hayo lakini kampuni hizo hazijalipa Kodi hiyo.
Alisema kuwa Zaidi ya mabango 25 yatashushwa ambapo tayari mabango Tisa yameshushwa ambayo yapo chini ya kampuni tatu ambazo ni Kampuni ya A1 Outdoor, Masoko Agency na kampuni ya Apple Media.
Kampuni zingine zinazodaiwa Kodi ni pamoja na M1 Outdoor, SkyOutdoor, Brooklyn Media, Loft Media, Lable Promotion, EF Outdoor, Milestone International, JCD Decaux, Spark Venture, Brand Active, Global System, na TBL Tanzania Ltd.
Kampuni zingine ni Goba Petrol Station, Oil Link, Lake Oil, Camel Oil, CRDB Bank PLC, Access Bank, Tanzania Distillers, Sadoline, UDART, na Equity Bank Tanzania LTD.
Mkurugenzi Kayombo alisema kuwa Jumla ya Shilingi 644.428.994.00 zinadaiwa kutoka katika kampuni hizo huku mdaiwa wa Deni kubwa ikiwa ni kampuni ya A1 Outdoor inayodaiwa Jumla ya Shilingi 273,000,000.00
Alisema kuwa Mabango yote yanayoshushwa yatahifadhiwa katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo na wamiliki watatakiwa kulipa gharama wanazodaiwa za Mabango sambamba na gharama ya ushushaji wa Mabango hayo.
Mkurugenzi Kayombo alisema kuwa katika kipindi hiki Cha serikali ya Awamu ya tano inayoongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ni wakati wa kazi sio wakati wa kucheza na kukwepa Kodi za serikali.
Aidha, ametoa Rai kwa wadaiwa wote kulipa Kodi ili kuendelea na huduma za kujitangaza kupitia Mabango yao.
IMETOLEWA NA;
KITENGO CHA HABARI NA UHUSIANO
HALAMASHAURI YA MANISPAA YA UBUNGO
No comments:
Post a Comment