Mkurugenzi
wa Kampuni ya Travel House Global, Sojan Varghese amefikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kupandishwa kizimbani akikabiliwa na
mashtaka ya kujipatia Sh 193 milioni alizopewa kwa ajili ya mahujaji
zaidi ya 119 wa Chama cha Karismatiki Katoliki Tanzania.
Varghese
alidaiwa kuchukua fedha hizo kutoka kwa John Ngotty kwa lengo la kukata
tiketi za ndege kwa mahujaji hao waliokuwa wakitaka kusafiri kuelekea
nchi za Roma, Italia na Israeli kwa ajili ya hija.
Wakili
wa Serikali, Adolf Mkini akimsomea hati ya mashtaka jana Ijumaa mbele
ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alidai kuwa Desemba 23, 2016
katika maeneo ya ofisi za kampuni hiyo zilizopo Mtaa wa Jamhuri,
Vargherse alijipatia fedha kutoka kwa Ngotty, fedha ambazo ni kwa ajili
ya nauli ya kupata tiketi ya ndege kwa Wakarismatiki 119 kutoka Dar es
Salaam kwenda Roma na Israeli.
Mkini
alidai kuwa Desemba 23, 2016 mshtakiwa huyo alijipatia kiasi kingine
cha fedha kupitia hundi namba 000005 kutoka kwa Ngotty kwa ajili ya
kuwakatia tiketi ya ndege mahujaji hao kwenda nchi hizo.
Alidai
kuwa Januari 11, 2017 katika maeneo ya ofisi hizo, Varghese alijipatia
Dola za Marekani 9,500 kutoka kwa Ngotty ili zitumike kununulia tiketi
za ndege kwa wanachama wa Wakarismatiki 119 kwenda hija nchi za Roma na
Israeli.
“Januari 11, 2017, alijipatia kiasi kingine cha fedha kwa hundi namba 000008 kutoka kwa Ngotty,” alisema.
Imedaiwa
kuwa Januari 31, 2017, Varghese alijipatia fedha kutoka kwa Ngotty kwa
ajili ya nauli ya tiketi ya ndege kwa wanachama 199 wa Karismatiki.
Mkini
alidai, Aprili 12, 2017, maeneo ya ofisi za kampuni yake, alijipatia
fedha kutoka kwa Ngotty kwa ajili ya kununulia tiketi kwa wanachama 119
wa Karismatiki waliokuwa wanakwenda hija nchi za Roma na Israeli.
Baada
ya mshtakiwa huyo kusomewa mashtaka hayo, alikana na upande wa mashtaka
ulieleza kuwa upelelezi haujakamilika na kwamba hawana pingamizi la
dhamana.
Hakimu
Mashauri alimtaka mshtakiwa huyo kuwasilisha fedha taslimu Sh 100
milioni ama hati ya mali yenye thamani ya kiasi hicho cha fedha pamoja
na hayo pia awe na wadhamini wawili wanaotambulika kisheria.
Pia
alimtaka mshtakiwa huyo kuwasilisha hati yake ya kusafiria na
haruhusiwi kutoka nje ya Dar es Salaam bila ya kuwa na kibali cha
mahakama.
Kesi imeahirishwa hadi Julai 6, 2017. Mshtakiwa amepelekwa rumande baada ya kushindwa kukamilisha masharti hayo ya dhamana.
No comments:
Post a Comment