VIJIJI 19 vilivyopo katika Wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro
vimefanikiwa kumaliza migogoro ya kugombea mipaka baada ya Mradi wa
Uwezeshaji Umilikishaji Ardhi (LTSP) kupitia wataalamu wa ardhi kuweka
alama za upimaji.
Vijiji hivyo vilikuwa na migogoro ya mipaka kwa zaidi ya miaka 10 kwa
kijiji kimoja kuingilia kingine na kwamba baada ya kupimiwa ardhi yao,
waliwekewa alama za upimaji (bikoni). Ofisa Ardhi Mteule wa Wilaya ya
Ulanga, Valence Huruma alisema haya wakati akizungumzia utekelezaji wa
mradi huo wa LTPS.
Alisema walibadili mfumo wa upimaji ardhi kutoka ule wa kuweka alama
bikoni kila baada ya kilometa tano hadi 10, na kuweka bikoni kwa kila
mita 50 ya mpaka ambazo ni ndefu zisizoweza kupoteza alama ya mpaka.
“Awali tulifanya upembuzi wa kupata taarifa za msingi kujua hali ya
umiliki ardhi na baada ya mradi kuisha utasaidiaje. Tulipima vijiji 19
hivi vilikuwa na mgogoro kwa muda mrefu na baada ya kuweka mipaka hakuna
migogoro tena,” alisema Huruma na kuongeza kuwa alama za upimaji
wanazoweka katika mipaka ni za kisasa ambazo haziwezi kupoteza alama ya
mpaka kwa hali yoyote.
Alisema kutatuliwa kwa migogoro ya mipaka kwa vijiji hivyo
kumechangiwa na ushirikishwaji wa wananchi ambapo katika uwekaji wa
alama za mipaka, viongozi kutoka vijiji viwili vinavyogombana husaini
kwa pamoja na kuridhia kuwekewa mipaka.
Alisema hii ni tofauti na awali ambapo upande mmoja wa kijiji chenye
mgogoro ndio uliosaini ili kuwekewa alama za mipaka hali iliyokuwa
ikisababisha migogoro inapotokea kushindwa kutatuliwa kwa urahisi.
Alisisitiza uwepo kwa migogoro hiyo unachangiwa na mfumo usiokuwa rasmi
wa kuanzisha vijiji bila ya kupanga maeneo ya matumizi.

No comments:
Post a Comment