Sunday, January 15, 2017

DC RUKIA MUWANGO AONYA WAZAZI KUWACHELEWESHA WANAFUNZI KUJIUNGA NA KIDATO CHA KWANZA MWAKA 2017


Pichani ni Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mhe Rukia Muwango
Baadhi ya wazazi na walezi wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2017 Wilayani Nachingwea wakimsikiliza kwa makini mkuu wa Wilaya hiyo Mhe Rukia Muwango

Na Mathias Canal, Lindi 
Wazazi na walezi wa wa wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2017 wametakiwa kulifanya suala la elimu kuwa Jambo la kipaumbele kwani msingi wa maendeleo ya Taifa ni pamoja na wananchi kuelimika kifikra na kuachana na mila potofu.
Hayo yamezungumzwa na Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi Mhe Rukia Muwango katika Ukumbi wa Shule ya Kutwa ya Nachingwea katika Kijiji cha Kilimahewa wakati wa kikao cha Wazazi na Walezi wa wanafunzi waliofaulu kujiunga na kidato cha kwanza kwa mwaka huu 2017.
 Kikao hicho kimejiri Mara baada ya kuripoti wanafunzi wachache katika shule za sekondari ambapo mpaka juzi Wanafunzi 450 pekee ndio walioripoti shule kati ya wanafunzi 2070 waliochaguli jambo ambalo litapelekea kudumaa kwa ukuaji wa elimu katika Wilaya hiyo ukilinganisha na maeneo mengine nchini.
Onyo hilo limetolewa na Mkuu Huyo wa Wilaya ya Nachingwea kwa wazazi na walezi wa wanafunzi hao ambapo amewaagiza wakuu wa Idara na Vitengo, Kaimu Mkuu wa Polisi Wilaya, Mdhibiti elimu Wilaya, Afisa elimu sekondari Wilaya, Afisa Taaluma Sekondari, Wakuu wa shule, Afisa Tarafa, Maafisa watendaji wa Kata na Vijiji wote kwa pamoja kuhakikisha wanafunzi hao wanajiunga na masomo haraka iwezekanavyo.
 Dc Muwango amewaagiza wazazi na walezi hao hadi kufikia tarehe 20/01/2016 wawe wamewapeleka wanafunzi kujiunga na elimu ya sekondari kabla serikali haijaingilia kati jambo hilo na kuchukua hatua stahiki kwa wazazi na walezi, ambapo pia amemuagiza Afisa elimu sekondari kukabidhi kwa mkuu wa Wilaya taarifa ya hali halisi ya kuripoti kwa wanafunzi katika shule zote 27 zilizopo Wilayani Nachingwea.
 Sambamba na hayo Wazazi na Walezi hao wamekiri kuwachelewesha watoto hao na kuomba radhi kwa jambo hilo hivyo kuahidi kuwa hadi kufikia Jumatatu tarehe 16/01/2016 tayari watoto wote watakuwa wameripoti shule.
 Hata hivyo DC Muwango amewataka Wakuu wa shule kuwapokea wanafunzi ambao hawajakamilisha baadhi ya mahitaji ya shule kama kupima afya sambamba na kuwataka wazazi kuhudhuria mikutano inayoitishwa kwa ajili ya kuimarisha ustawi wa elimu katika shule za msingi na sekondari.
 Dc Muwango pia amewaasa wananchi Wilayani humo kutumia vizuri fedha za Korosho kwa kununua chakula na kuhifadhi kwa ajili ya akiba ya njaa, kujenga nyumba bora, kuwa na vyoo bora na kuvitumia na sio kwenda kujisaidia porini kwani kufanya hivyo ni kuharibu mazingira.
Hata hivyo amewashauri wakulima wa korosho kupanda mbegu mpya za korosho zinazopatikana katika ofisi ya idara ya kilimo Wilaya ili kuimarisha zaidi ustawi wa kilimo hicho kwa kutumia mbegu bora.
MWISHO

No comments:

Post a Comment