Sabodo akisisitiza jambo
Mfanyabiashara
maarufu nchini, Jaffar Sabodo (73), amemshauri Rais John Magufuli
abadilishe fedha ili kubana wafanyabiashara wakwepa kodi na kuficha
fedha majumbani.
Aidha,
amesema kutokana na utendaji wa Rais, haoni sababu za vyama vya upinzani
kuendelea kumpinga, na badala yake waache siasa na waungane naye
kujenga Tanzania mpya.
Kauli ya
mfanyabiashara huyo iliungwa mkono na wachumi waliozungumza na gazeti
hili kubainisha kuwa njia nzuri zaidi ni Benki Kuu ya Tanzania (BoT)
kupunguza masharti kwa benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye
benki iwe kubwa jambo ambalo litafanya watu wakiweka fedha benki wapate
faida.
Sabodo
alitoa ushauri huo jana alipozungumza na JAMBO LEO katika mahojiano
maalumu nyumbani kwake Dar es Salaam, ambapo alisema licha ya hatua
nzuri za Serikali ya Rais Magufuli kiuchumi na kwenye mapambano dhidi ya
rushwa, ubadhirifu na ufisadi, wapo walioficha mabilioni ya fedha
nyumbani badala ya benki ili kukwepa kodi.
“Rais
anafanya kazi nzuri, lakini ni wengi walioficha fedha nyumbani.
Watanzania wanakufa njaa, wengine wameficha fedha. Hapo nashauri Rais
abadilishe fedha hasa noti za Sh 5,000 na Sh 10,000. Hatua hiyo
itasaidia kukabili ubadhirifu unaofanywa na watu wenye nia mbaya, lakini
pia inaweza kuokoa uchumi na kufikia ndoto ya kuwa na Tanzania Mpya,”
alisema Sabodo.
Aliongeza:
“Kwa maoni yangu, hatua hiyo ya kubadilisha fedha ichukue kati ya mwezi
mmoja na mmoja na nusu, watabainika wengi walioficha fedha nyumbani na
hali ya uchumi itabadilika.”
Akifafanua,
Sabodo ambaye ni mzaliwa wa Lindi, alisema India, Pakistan na Venezuela
ziliwahi kukumbwa na hali kama iliyopo sasa nchini, lakini hatua ya
kubadilisha noti ilizisaidia kuimarisha uchumi na bajeti zao.
“Watu
wanaiba fedha nyingi, wanazificha chini ya magodoro, ili kumaliza hali
hiyo ni muhimu noti zikabadilishwa hali itakayomlazimisha kila
aliyeficha fedha kuzitoa, hapo wapo watakaokimbia nchi,” alisema Sabodo
huku akitaja baadhi ya watakaokimbia hatua hiyo ikichukuliwa.
Sabodo
alitoa kauli hiyo wakati Rais Magufuli ameshatoa kauli kuwataka
walioficha fedha majumbani kuziacha ziingie kwenye mzunguko huku akionya
wasipofanya hivyo anaweza kuamua kuzibadili ili wakose mahali pa
kuzipeleka.
Magufuli
alitoa kauli hiyo Septemba kwenye mkutano wa 14 wa mwaka wa wahandisi
ambapo alisema watu hao wamekuwa na utaratibu wa kutoa fedha zao benki
na kuzificha kwa kuogopa kuwa atabaini kiasi walichonacho.
Wachumi
Akizungumzia
suala hilo, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (Sua),
Profesa Damian Gabagambi alisema: “Kuendesha uchumi hakutakiwi nguvu
sana. Uchumi unajengwa kwa imani, mtu yeyote anayeendesha uchumi
anatakiwa kuijenga hiyo imani na ikuzwe.
“Chochote
kinachofanyika na kuua imani kinavuruga uchumi, ukiona watu wanaficha
fedha hilo si tatizo, ni kwamba kuna kitu ambacho ni tatizo, kuficha
fedha ndio kujihami kwao.”
Alisema
njia nzuri ya kufanya watu walioficha fedha kuzitoa, ni BoT kupunguza
masharti inayowekea benki, hasa viwango vya riba, ili riba kwenye benki
iwe kubwa, jambo ambalo litafawanya watu kutoficha fedha kwa maelezo
kuwa wakipeleka fedha kwenye benki hizo, watapata faida.
Alisema
riba inayotozwa kwenye benki inapangwa na BoT na kuitaka benki hiyo
kufanya marekebisho ili kusaidia wanaoweka fedha kwenye benki kupata
faida.
“Ila kama
wana hakika fedha zimefichwa na wahusika hawawezi kuzitoa, njia pekee
ni kutishia kuchapisha, ingawa hiyo ni njia ya haraka sana. Pamoja na
hayo, muhimu ni kuhakikisha chanzo cha watu kuficha fedha kinajulikana,”
alisema
Mhahidhi
Mwandamizi wa Chuo Kikuu Dar es Salaam (UDSM), Dk Haji Semboja alisema:
“Katika uchumi ambao unakwenda vizuri na mamlaka zinazohusika na
usimamizi wa fedha zinafanya kazi, suala hilo (kuficha fedha) haliwezi
kujitokeza kwa maana mwenye fedha atajua jinsi ya kuziweka.
“Katika
uchumi ambao watu wamekaa na kuhodhi fedha majumbani mwao ukitaka fedha
hizo ziingie kwenye mzunguko basi unazibadilisha. Watu watazileta kwa
nguvu maana hawatakuwa na ujanja. Ila kubadili fedha kuna sababu
nyingi.”
Alisema
sababu nyingine ni kutaka kubadili fedha ili kuwa na mwonekano mpya,
pamoja na ubora wake ikiwa za awali zilikuwa zikichakaa mapema.
No comments:
Post a Comment