Thursday, December 8, 2016

MWAKYEMBE – KUNA HAJA YA KUWA NA MIKAKATI YA KUZUIA MAUAJI YA KIMBARI

WAZIRI wa Mambo ya Katiba na Sheria, Dk Harrison Mwakyembe amewataka wajumbe wa Kamati ya Kimataifa inayojishughulisha na kuzuia mauaji ya kimbari katika nchi za ukanda wa Maziwa Makuu, kuangalia upya mikakati ya kuondoa vitendo vya mauaji ya kimbari na ukiukwaji wa haki za binadamu katika ukanda huo.

Amesema Ukanda wa Maziwa Makuu umekuwa ukishuhudia vitendo vya mauaji ya kimbari vikishamiri licha ya kwamba kila nchi imekuwa ikichukua jitihada mbalimbali na kusaini makubaliano ya kikanda na kimataifa ya kuzuia vitendo hivyo.mwakyem

Alisema wakati umefika wa kujiangalia ni kwa nini vitendo hivyo vimekuwa vikishamiri pamoja na jitihada zote ambazo kila nchi imekuwa ikizichukua ili kukomesha vitendo hivyo.

Dk Mwakyembe aliyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya kuwajengea uwezo na kubadilisha uzoefu na wajumbe wa kamati hiyo kwa nchi za Maziwa Makuu yanayofanyika jijini Dar es Salaam.

Mafunzo hayo yanajumuisha wajumbe kutoka nchi za Zambia, Rwanda, Burundi, Kenya, Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Sudan Kusini na wenyeji Tanzania.

“Ni wazi kuwa siku hizi mwelekeo wa matukio ya kihalifu umebadilika, zimeibuka njia nyingi mpya zinazosababisha mauaji ya kimbari na hata ukiukwaji wa haki za binadamu, kutokana na hali hiyo kuna haja ya kuboresha mikakati yenu ili kuzuia kuendelea kutokea kwa mauaji ya kimbari na ukiukwaji wa haki za binadamu,” alisema.

Aidha, amewaambia wajumbe wa kamati hiyo kuwa ni jukumu lao kuangalia namna ya kukabiliana changamoto ambazo zimekuwa zikijitokeza na hivyo kufanya vitendo hivyo kuendelea kuwepo miongoni mwa nchi za maziwa makuu.

Amewataka wataalamu hao kwenda mbali zaidi na kubainisha hatua za kisera, kisheria na kiutawala zitakazofaa kuchukuliwa ili kukabiliana na changamoto ya kuendelea kuwepo kwa vitendo hivyo, lengo likiwa kuvikomesha ndani ya nchi za ukanda wa maziwa makuu

No comments:

Post a Comment