Friday, December 2, 2016

KINANA AONGOZA MAZISHI YA MUASISI WA TANU KHADIJA KAMBA

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara Rajab Luhwavi, akishiriki kubeba jeneza lenye mwili wa Muasisi wa TANU, Khadija Kamba, katika makaburi ya Kisutu, wakati wa mazishi yaliyofanyika Jana, Desemba 01, 2016, katika makaburi hayo mjini Dar es Salaam. (Picha na Bashir Nkoromo).

Na Bashir Nkoromo

Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ameongoza mamia ya wananchi katika maziko ya muasisi wa chama cha Tanganyika African Union (TANU) na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), Khadija Kamba, aliyefariki jana na kuzikwa Jana katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam.

Kinana ambaye alifuatana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM-Bara, Rajab Luhwavi, akitoa salam za rambirambi za Chama, alisema, CCM itamkumbuka na kuuenzi daima mchango mkubwa alioutoa hasa wakati wa harakati za ujenzi wa TANU na harakati za ukombozi wa Tanzania wakati wa uhai wake.

"Binti Kamba alikuwa ni nguzo na chachu muhimu katika kuasisiwa kwa TANU na mpambanaji aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za kutafuta Uhuru wa nchi hii, hivyo Chama kitambukumbuka na kumuenzi daima Mama huyu", alisema Kinana, wakati akitoa salam za rambirambi wakati wa maziko.

Kinana alisema, licha ya kuwa muasisi, lakini Binti Kamba kamtika maisha yake, aliendelea kuwa nwanachama na kada mwaminifu wa Chama Cha Mapinduzi na kuendelea kuwa kisima cha kuchota hekima na maarifa hadi anafariki dunia.

Alisema, kutokana na kuguswa na msiba huo, kwa nafasi yake ya Katibu Mkuu wa Chama, ameandaa hitima itakayosomwa keshokutwa katika Msikiti wa Masjid Quba, kumuombea maghfira.

Binti Kamba, ambaye amefariki akiwa na umri wa miaka 94, alifariki juzi asubuhi, nyumbani kwa mwanae wa kulea, Kamba Abdallah, jijini Dar es Salaam, kutokana na kuugua figo na moyo.

Msafara kwenda kwenye maziko Kisutu ulianzia nyumbani kwa marehemu, Ilala Bungoni, Dar es Salaam, baada ya kuswaliwa, ambako miongoni mwa waombolezaji waliokuwepo ni pamoja na Muasisi mwingine wa TANU Kingunge Ngombale-Mwiru, ambaye mwaka jana alihamia Chadema kumfuata aliyekuwa mgombea urais kwa tiketi ya Chama hicho Edward Lowassa.

No comments:

Post a Comment