Wednesday, November 30, 2016

WIZARA YA MAJI KUJENGA MTAMBO WA MAJITAKA UTAKAOGHARIMU BILIONI 200

madini
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akitoa hotuba ya uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa kutathmini maendeleo ya sekta ya maji uliowashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi. Mkutano huo umefanyika leo katika ukumbi wa arnautoglo uliopo maeneo ya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.
madini-1
Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya wadau wa maendeleo wa sekta ya maji walioshiriki katika Mkutano Mkuu wa kutathmini maendeleo ya sekta hiyo uliofanyika leo katika ukumbi wa arnautoglo uliopo maeneo ya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.

Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO

Wizara ya Maji na Umwagiliaji imejipanga kuanza ujenzi wa mtambo mkubwa wa majitaka katika maeneo ya Ilala Jijini Dar es Salaam ili kuzuia uchafuzi wa mazingira nchini.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Mhandisi Gerson Lwenge alipokuwa akizindua Mkutano Mkuu wa kutathmini maendeleo ya sekta ya maji unaolenga kutatua changamoto zinazozuia upatikanaji wa maji salama na uondoshaji wa majitaka nchini.

Mhandisi Lwenge amesema kuwa fedha za mradi huo zimetoka Serikali ya Korea Kusini ambapo kwa sasa wizara hiyo ipo katika mchakato wa kumtafuta Mhandisi mshauri ambaye atafanya mapitio sanifu ya manunuzi ya vifaa na baada ya hapo juhudi za kumtafuta mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa mitambo hiyo zitaendelea.

“Mtambo huo utajengwa katika wilaya ya Ilala na mabomba yake kutandazwa katika maeneo yaliyopo katikati ya jiji, Magomeni pamoja na Kurasini ili kuhakikisha maji machafu yanapata sehemu ya kuelekea na kuacha jiji likiwa safi siku zote,” alisema Mhandisi Lwenge.

Mhandisi Lwenge aliongeza kuwa baada ya mtambo huo kukamilika maji yatakayopatikana yatasafishwa na kutumika kwa matumizi mengine yakiwemo ya nyumbani, ufugaji, kilimo cha umwagiliaji au kupelekwa moja kwa moja katika bahari ya Hindi.

Naye Mwakilishi kutoka Asasi za Kiaraia, Josephine Lemoyan amesema kuwa uchafuzi wa mazingira unachangiwa na kutokuwa na miundombinu mizuri ya kupitisha maji machafu hivyo mkutano huo uliofunguliwa leo utajadili mambo mbalimbali ikiwemo njia za  uondoshaji wa majitaka ambayo kwa kiasi kikubwa unaathiri mazingira yanayotuzunguka.

“Katika kila sekta mapungufu huwa hayakosekani hivyo kwa kupitia mikutano ya wadau kama hii inatusaidia kupata mawazo ya kutatua baadhi ya changamoto zinazozuia uendelevu wa miradi mbalimbali ya majisafi na majitaka,”alisema Bi. Josephine.

Bi. Josephine amefafanua kuwa hadi kufikia mwezi Juni 2016 Tanzania imejitahidi kuondoa majitaka kwa asilimia 52.6 na ifikapo mwaka 2020 Tanzania inategemewa kufikia asilimia 75 katika suala zima la uondoaji wa majitaka.

Mkutano huo wa siku mbili ambao umewashirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi unafanyika katika ukumbi wa arnautoglo uliopo maeneo ya Mnazi Mmoja, Jijini Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment