Hivi
karibuni kumekuwepo na taarifa katika baadhi ya vyombo mbalimbali vya
habari vya ndani na nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na mitandao ya kijamii
vikizungumzia hali ya dawa nchini hasa kufuatia taarifa zilizotolewa na
taasisi ya kiraia na baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa.
Taarifa
hizo zilidai kwamba katika kipindi hiki kuna upungufu mkubwa wa dawa
katika bohari kuu ya dawa , Hivyo, kusababisha kukosekana kwa dawa
katika vituo vya kutolea huduma za Afya.
Taarifa
hizi si sahihi na zinalenga kupotosha umma na kuwatia wananchi
wasiwasi. Napenda kuwathibitishia wananchi kuwa Afya ni suala la
kipaumbele kwa Serikali ya Awamu ya Tano. Hivyo, ningependa kutoa
ufafanuzi kwa wananchi katika masuala yafuatayo; –
Hali ya Upatikanaji wa dawa
Hali
ya upatikanaji wa dawa kwa sasa iko vizuri. Dawa muhimu zinazohitajika
sana nchini zinapatikana kwenye maghala ya Bohari ya Dawa (MSD). Mfano
kwa upande wa dawa za antibiotics tuna Amoxycillin, Ciprofloxacin,
Cotrimoxazole na Doxycycline. Kwa upande wa dawa za maumivu – tunazo za
kutosha kama vile paracetamol, asprin na diclofenac.
Pia
tuna dawa za kutosha za malaria, Kifua Kikuu, ukoma na dawa za kufubaza
makali ya UKIMWI (ARVs). Kwa upande wa chanjo za watoto na wajawazito,
ni kweli kulikuwa na uhaba nchini kwa kipindi cha miezi miwili
iliyopita.
Hata
hivyo, wiki iliyopita Serikali imenunua na kupokea dozi milioni 2 za
chanjo ya Kifua Kikuu (BCG), dozi milioni 1.2 za Polio na dozi milioni
za Polio. Chanjo hizi zinasambazwa katika vituo vya afya nchini.
Dawa
nyingine zitaendelea kupatikana katika Bohari kuu ya Dawa kwa kuwa
tumeagiza dawa za kutosha kutoka kwa wazalishaji wa ndani na nje ya
nchi.
Aidha,
kiasi kikubwa cha dawa zinazowasili Bohari kuu ya Dawa zikifika
zinapelekwa kwenye Kanda nane za MSD pamoja na vituo viwili vya Mauzo
kwa ajili ya kuwasambazia wateja walioagiza.
Hivyo,
kipimo cha upatikanaji wa dawa si kuangalia katika maghala ya Bohari ya
Dawa peke yake bali pia katika vituo vya kutolea huduma za afya.
Ili
kuondoa mlolongo wa manunuzi ya dawa, tunapenda kuwataarifu kuwa Bohari
kuu ya Dawa imepanua wigo wa upatikanaji wa dawa kwa sasa kwa kutumia
mikataba ya muda mrefu (miaka miwili) na washitiri wa ziada wa ndani
(Prime Vendors) ili kuhakikisha dawa zinapokosekana MSD zinapatikana kwa
haraka kwa Washitiri wa ndani waliothibitishwa katika kila mkoa.
Katika
muktadha huo huo, Bohari ya Dawa imefungua maduka ya ziada kwa ajili ya
kuongeza upatikanaji wa dawa zaidi ya aina 600 kupitia mfumo wa maduka
katika mahospitali kama vile Muhimbili, Mbeya na Arusha.
Bajeti ya dharura kwa ajili ya dawa
Ni
muhimu wananchi wakajua kuwa fedha zilizotengwa kwa ajili ya manunuzi
ya dawa katika mwaka wa fedha 2016/17 zinatosha kuhudumia mahitaji ya
dawa kwa mwaka mzima. Hivyo hakuna sababu ya kuwa na bajeti ya dharura.
Niwakumbushe
bajeti zilizotengwa kwa ajili ya kununulia dawa na vifaa tiba katika
miaka michache iliyopita mpaka hivi sasa, kama ifuatavyo: -.
Mwaka 2011/2012 bajeti iliyotengwa ilikuwa shilingi Bilioni 23.7
Mwaka 2012/2013 bajeti ilikuwa shilingi Bilioni 34
Mwaka 2013/2014 ilikuwa shilingi Bilioni 34
Mwaka 2014/2015 ilikuwa shilingi Bilioni 60
Mwaka 2015/2016 ni shilingi Bilioni 30
Na mwaka huu 2016/17 ni shilingi Bilioni 251.5
Mkakati wa Wizara kwa sasa ni kuhakikisha kuwa fedha hizo zinapatikana kwa wakati kutoka Hazina kulingana na makusanyo ya nchi.
Vilevile
ieleweke kwamba tayari serikali imeshatoa kiasi cha shilingi bilioni 20
katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2016/17, kwenda
Bohari kuu ya Dawa kwa ajili ya ununuzi wa dawa na chanjo. Hali hii
inathibitisha kuwa suala la upatikanaji wa dawa ni la kipaumbele kwa
Serikali ya Awamu ya tano.
Kulipa Deni la Bohari ya Dawa (MSD)
Napenda
kuwafahamisha kuwa Serikali imedhamiria kulipa deni lote la Bohari ya
Dawa (MSD) ambapo katika mwaka huu wa fedha 2016/17 tayari Bilioni 85
imekwishatenga kwa ajili ya kulipa deni hilo.Jambo ambalo halijawahi
kutokea huko nyuma. Kulipwa kwa deni hilo kutasaidia kuhuisha mtaji wa
MSD (revolving fund) na hivyo kuiwezesha MSD kuwa na dawa na vifaa tiba
kwa kiwango kikubwa.
Aidha
serikali imekwisha kuviagiza vituo vyote vinavyotoa huduma za Afya
kupitia Halmashauri zao, kuhakikisha zinakuwa na fedha ya mzunguko kwa
ajili ya kununulia dawa (revolving fund) na hivyo kupata dawa kwa kulipa
fedha taslimu kutoka Bohari ya Dawa badala ya kukopa.
Fedha
hizo zitapatika kutoka kwenye vyanzo vyao vingine vya mapato kama vile
Bima ya Afya (NHIF, CHF) na gharama wanazochangia wananchi katika kupata
huduma. Hii itawezesha kutoendelea kukuza deni kutoka Bohari ya Dawa na
kuhakikisha dawa zinapatikana kwa wakati wote.
MSD Kupata Mshindani
Katika
mwaka 2015, Serikali ilimpa kazi mshauri mwelekezi wa kampuni ya
ushauri iliyobobea kimataifa ya Deloitte ya kulitazama jambo hili kwa
ajili ya kuifanyia tathmini MSD pamoja na mambo mengine ikiwemo
kuangalia suala ya kutafutiwa mshindani katika manunuzi na usambazaji wa
dawa.
Napenda
kuwajulisha kuwa tathmini hiyo ilionyesha kuwa MSD kutafutiwa mshindani
itakuwa ni kuongeza gharama kubwa kwa serikali kutokana na kurudufisha
(duplication) majukumu.
Pia
ilibainika kuwa suala la dawa ni muhimu, hivyo Serikali haiwezi
kuliacha kwenye mikono ya watu binafsi.Jambo ambalo lilipendekezwa ni
kuifanyia maboresha makubwa MSD ili iweze kutekeleza majukumu yake
ipasavyo. Utekelezaji wa mapendekezo hayo tayari umeshaanza.
Nchi ambazo zinaiuzia dawa na vifaa tiba MSD
MSD
inaagiza dawa na vifaa tiba nje ya nchi zaidi ya asilimia 80 kwa sababu
viwanda vilivyoko ndani ya nchi havikidhi mahitaji ya nchi kwa ubora na
kiasi. Hivyo, MSD hununua dawa na vifaa tiba kutoka nchi za India,
China, Kenya, Uganda, Afrika Kusini, Ujerumani, Marekani, Ufaransa na
sehemu nyingine duniani.
Kwa
mfano, tuna dawa zaidi ya aina nne ambazo zinanunuliwa kutoka Kenya
(Dawa ya kutibu malaria kwa akina mama wajawazito ijulikanayo kama
Sulfadoxine Pyrimethamine (SP), dawa ya kutibu magonjwa ya maambukizi ya
Cotrimoxazole ya watu wazima na watoto pamoja, Amoxicilline na
Paracetamol ya maji kwa ajili ya watoto.
Ikumbukwe
kuwa MSD hununua dawa hizi kupitia mchakato wa zabuni, ikiwa baadhi ya
vigezo ni kuangalia usajili wa dawa nchini pamoja na ushindani wa bei.
Hata hivyo, ili kukuza viwanda vya ndani, watengenezaji wa dawa wa ndani
hupewa hadi 15% ya upendeleo katika mchakato wa tathmini ya zabuni
dhidi ya dawa zinazotoka nje ya nchi (Domestic preference).
Kwa
upande mwingine mkakati wa serikali sio kuendelea kutegemea dawa kutoka
nje ya nchi, kwani kwa kufanya hivi uchumi wa nchi hautakuwa. hivyo
basi serikali iko katika hatua za mwisho za utaratibu wa kuwakaribisha
wawekezaji wa viwanda vya kuzalisha dawa kuwekeza nchini kwa mpango wa
kuwashirikisha wadau wengine katika masuala ya dawa (PPP).
Hitimisho
Wizara
ya afya inapenda kuwahakikishia wananchi kuwa itasimammia ipasavyo
utapatinaji wa dawa, vifaa na vifaa tiba nchini kwa wakati na kwa bei
nafuu kwa kuwa Sera ya afya inawataka wananchi kuchangia huduma.
Aidha
vituo vya kutolea huduma za Afya vinahimizwa kupeleka mahitaji na
maoteo yao ya dawa kwa wakati badala ya kusubiri hadi dawa zote muhimu
zimeisha kabisa katika vituo vyao. Pia wanakumbusha kulipa madeni
wanayodai na bohari ya dawa sambamba na kuhakikisha fedha inayopatikana
katika shughuli za utoaji huduma inatumika kwa ajili ya dawa, vifaa na
vifaa tiba.
Ili
kuondoa vikwazo kwa wananchi katika kupata dawa na huduma za afya kwa
ujumla wananchi wanahimizwa kujiunga na mifuko ya Bima ya Afya kwani
hakuna anayejua leo hama kesho ataugua na Magonjwa hayapigi hodi na
wakati mwingine yanakukuta hauna akiba ya fedha, ila ukiwa na bima
wakati wowote unapata matibabu.
Mwisho,
Wizara itaendelea kuhakikisha kuwa kuna dawa, vifaa tiba na
vitendanishi vya maabara vya kutosha kwenye vituo vya umma vya kutolea
huduma za Afya nchini
No comments:
Post a Comment