Waziri wa
Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na WatotoMh. Ummy Mwalimu
akizungumza na waandishi wa habari wakati alipokuwa akitoa tamko la
serikali kuhusu Takwimu za viashiria vya Ukimwi na Maralia mwaka
2011-2012 na kiwango cha maambukizi ya Ukimwi (VVU) kushoto kwake ni
Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Mohammed Bakari Kambi.
Kwa
mujibu wa Takwimu za Viashiria vya UKIMWI na Malaria za mwaka 2011-2012,
kiwango cha maambukizi ya Virusi vya UKIMWI (VVU) nchini kinakadiriwa
kuwa ni asilimia 5.1 miongoni mwa watu wazima wenye umri kati ya miaka
15 – 49. Takwimu hizi zinaashiria kwamba, kwa kila watanzania 1000, watu
51 miongoni mwao wanaoishi na maambukizi ya VVU. Inakadiriwa kuwa, kuna
watu 1,400,000 wanaishi na VVU nchini Tanzania ambapo, watu 839,574
wanapatiwa tiba ya dawa za kupunguza makali ya VVU zinazotolewa katika
vituo 4,000 vilikuwa vinatoa huduma hiyo nchi nzima hadi kufikia mwezi
Juni mwaka huu (2016).
Serikali
ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Wadau wake imechukua
hatua za makusudi na za haraka katika kukabiliana na Maambukizi ya
Virusi vya UKIMWI na UKIMWI. Serikali imefanikiwa kuanzisha na
kutekeleza mipango mbalimbali ya kuzuia maambukizi mapya kwa kutoa
huduma za kinga, tiba na matunzo kwa walioambukizwa VVU katika ngazi ya
vituo vya huduma za afya na ngazi ya jamii. Mikakati yote hii imelenga
kuboresha afya kwa kupunguza maambukizi mapya ya VVU na kutokomeza
kabisa UKIMWI.
Mbali na
Mipango mikakati na mbinu madhubuti ambazo zimetekelezwa bado takwimu
zinaonesha kuwa kiwango cha maambukizi miongoni mwa makundi maalum na
yale yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa VVU yapo juu kulinganisha
na kiwango kilichopo kwa jamii kwa ujumla.
Kutokana
na mazingira yetu makundi maalum ni makundi yaliyo katika hatari zaidi
ya kuambukiza na kuambukizwa VVU, kwa kuzingatia takwimu za maambukizi
ya VVU kwa makundi haya kuwa juu, Serikali imeainisha makundi haya kama
ifuatavyo:-
Wasichana
walio katika umri wa balehe walio katika mazingira hatarishi, vijana
walio katika umri wa balehe, watoto yatima na watoto walio katika
mazingira hatarishi (yaani watoto wanaoishi mitaani), wanaume wanaofanya
ngono na wanaume wenzao, wanawake wanaofanya ngono kinyume na maumbile,
watu wanaotumia dawa za kulevya hasa wale wanaotumia dawa za kulevya
kwa njia ya kujidunga sindano, wanawake wanaofanya biashara ya ngono na
wateja wao, wafungwa, wakimbizi na wafanyakazi wanao hamahama hasa
madereva wa malori ya masafa marefu, wachimba madini na jamii zilizopo
katika maeneo ya migodi, wavuvi na jamii zilizopo katika maeneo ya
uvuvi, wafanyakazi wa kwenye mashamba makubwa, wajenzi wa barabara na
watu wenye ulemevu.
Kuna
ushahidi wa kipiedemilojia kwa programu za VVU na UKIMWI kulenga makundi
maalum. Katika nchi zilizo Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, vijana
balehe wenye umri wa miaka 15 hadi 24 wanachangia asilimia 35 ya
maambukizi mapya ya VVU. Aidha, kiwango kikubwa cha maambukizi ya VVU
nchini Tanzania, kinaonekana miongoni mwa makundi maalum (asilimia 26
miongoni mwa Wanawake wanaofanya Biashara ya Ngono, asilimia 36 miongoni
mwa wajidunga na asilimia 25 miongoni mwa wanaume wanaofanya ngono na
wanaume wenzao).
Serikali
ya Tanzania kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na
Watoto ilianza kutoa huduma za VVU na UKIMWI kwa makundi maalum na yale
yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa na kuambukiza VVU tangu mwaka
2010 baada ya kufanya tafiti na kugundua kuwa kiwango cha maambukizi ya
VVU kiko juu ikilinganishwa na makundi mengine kwenye jamii. Huduma
hizi zimekuwa zinatolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya katika
ngazi ya Jamii katika Mikoa mbalimbali nchini.
Hivi
karibuni kumekuwepo na taarifa kuwa Asasi za Kiraia (za hapa nchini na
za Kimataifa) zimekuwa zinapitia katika Afua ya kupambana na UKIMWI ili
kuhamasisha mapenzi ya jinsia moja, na hii imepelekea Waziri wa Katiba
na Sheria kutamka kupitia vyombo vya habari kuwa atavichukulia hatua za
kisheria asasi hizo ambazo zinakiuka taratibu na sheria zilizowekwa na
Serikali.
Napenda
kutamka kwamba, Wizara yangu halitalifumbia macho suala hili, na napenda
kuziasa asasi zote za kiraia za ndani na nje ya nchi kufanya kazi kwa
kufuata taratibu na sheria za nchi na kutoa afua zenye lengo la
kupambana na maambukizi mapya ya VVU katika makundi haya na jamii kwa
ujumla. Aidha nazitaka asasi hizo kutoa huduma bora zenye kiwango cha
kimataifa lakini pia huduma zinaoendana na utamaduni, mila na desturi za
Mtanzania huku zikizingatia sheria za nchi kama vile sheria ya kanuni
ya adhabu, sura ya 16 kama ilivyofanyiwa marakebisho mwaka 2002.
Tukumbuke
kwamba Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto ina jukumu la kutoa huduma za Afya na zile za kupambana
na UKIMWI bila ubaguzi, na vilevile bila kujali jinsi, kabila, dini,
hali ya kifedha, rangi au chama cha mtu yeyote.
Baada ya
kubaini changamoto katika utoaji wa huduma za Afya na zile za kupambana
na UKIMWI kwa asasi zisizo za Serikali, niliitisha kikao na wadau wa
maendeleo wanao fadhili na kutoa huduma za kupambana na UKIMWI katika
makundi haya maalum ili niweze kutoa ufafanuzi wa mambo kadhaa ya msingi
ikiwemo kuweka bayana suala la kutoa huduma za VVU kwa makundi haya
huku tukizingatia taratibu na sheria za nchi (Public Health Approach to
HIV programming to PK).
Yafuatayo ni matamko niliyoyatoa na ambayo wote tunapaswa kuyazingatia:
Serikali
itaendelea kutoa huduma za Afya na zile za kupambana na UKIMWI bila
ubaguzi wa jinsi, kabila, dini, hali ya kifedha, rangi au chama cha mtu
yeyote.
Kwa kuwa
maambukizi ya VVU kwa makundi maalum bado yapo juu ukilinganisha na
jamii kwa ujumla, Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii,
JInsia, Wazee na Watoto itaendelea kutoa kitita cha huduma kama
kitakavyopitiwa na kuainishwa na miongozo ya kutolea huduma za kupambana
na UKIMWI katika makundi maalum.
Makundi
Maalum kwa mantiki ya Tanzania itabaki kuwa ya kiujumla kama yalivyo
tajwa hapo juu ambayo yanaendana na mazingira ya Tanzania, hivyo maana
na tafsiri hiyo ifuatwe na kuzingatiwa katika huduma au afua
zinazotekelezwa na wadau wote wanao shirikiana na Serikali katika kutoa
huduma za VVU na UKIMWI nchini.
Kila mdau
wakati wote atoe huduma kwa mujibu na sheria na kanuni ya adhabu sura
ya 16 kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002 inayotaka mtu
kuchukuliwa sheria endapo atathibitika kufanya mapenzi na mtu wa jinsia
moja., na kama mdau ni shirika lisilo la Serikali pia ana wajibu wa
kuzingatia Sheria Na 24 ya Mwaka 2002 ya Asasi zisizo za Kiserikali, na
kufuata maadili ya kazi za NGO (NGO code of conduct).
Huduma za
Makundi maalum na yale yaliyo katika hatari zaidi ya kuambukizwa na
kuambukiza VVU zinazotolewa katika vituo vya kutolea huduma za afya
zitaendelea kwa makundi yote isipokuwa huduma za ngazi ya jamii kwa
wanaume wanaofanya ngono na wanaume wenzao, hizi zitasubiri mwongozo
mpya wa utoaji wa huduma ngazi ya jamii. Huduma mkoba zinazotolewa na
watoa huduma za afya toka vituoni zitaendelea kutolewa kwa mujibu wa
miongozo iliyopo. Wizara inaweka msisitizo mkubwa katika kuunganisha
huduma zinazofanana na utoaji wa rufaa katika vituo vya huduma za afya
kwa mwendelezo wa huduma. Taratibu za utekelezaji zitafafanuliwa na
Wizara ndani ya wiki moja.
Kutokana
na kuongezeka kwa idadi ya wadau wanaotaka kushirikiana na kuisaidia
Serikali katika kutoa huduma hizi, hasa kwa kuzingatia tabia ya kuhama
hama kwa makundi haya kutoka eneo moja hadi jingine, kumekuwa na
mwingiliano wa huduma zinazotolewa kwa makundi haya, mwingiliao huu
unahatarisha ubora wa huduma. Ili kuleta tija, uwajibikaji na uwazi,
Mganga Mkuu wa Serikali ataongoza zoezi la kupanga upya wadau katika
Mikoa watakayotoa huduma kwa nchi nzima.
Asasi
zote za kiraia za hapa nchini zinazotekeleza afua za VVU na UKIMWI
katika Halmashauri lazima ziidhinishwe na Halmashauri husika kabla
hazijaruhusiwa kufanya kazi na asasi zisizo za kiserikali za kimataifa.
Kwa maneno mengine, Asasi zisizo za kiserikali za kimataifa zitapewa
orodha ya asasi za kiraia zilizoidhinishwa kufanya kazi katika
Halmashauri au Wilaya husika. Kanuni za Msingi za Ushirikiano (MOU)
zitaandaliwa kati ya wadau watatu, yaani Asasi ya Kimataifa, Asasi ya
Kiraia ya hapa nchini na Halmashauri au Wilaya husika. Nakala ya Kanuni
za Msingi za Ushirikiano (MOU) ziwasilishwe Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara ya Maendeleo ya Jamii) na Tume ya
Taifa ya Kudhibiti UKIMWI.
No comments:
Post a Comment