WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema amefurahishwa na uamuzi wa Kanisa Katoliki
na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) wa kutafuta viwanja Dodoma ili
wajenge ofisi za makao yao makuu pamoja na makazi ya viongozi wao wakuu.
Ametoa
kauli hiyo jana (Alhamisi, Oktoba 27, 2016) wakati akizungumza na
Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya wa Jimbo Katoliki la Dodoma pamoja na
Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC), Bw.
Peter Maduki ofisini kwake mtaa wa Railway, mjini Dodoma.
“Sina
shaka juu ya maombi yenu ya kupatiwa viwanja kwa ajili ya ujenzi wa
makao makuu pamoja na makazi ya viongozi wakuu. Sasa hivi Master Plan ya
Dodoma kama Makao Makuu ya nchi inapitiwa upya ili izingatie mahitaji
ya msingi sababu zamani ilikuwa haijapangwa kwa mazingira ya sasa ya
ujio wa Serikali,” alisema Waziri Mkuu.
Alisema
wiki tatu zilizopita alimwagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Ustawishaji Makao Makuu (CDA) ili atafute makampuni yenye uwezo wa
kupima viwanja kwa haraka. “Hii itatusaidia kutambua tuna eneo kiasi
gani na mahitaji halisi ni yapi na nani akija apewe eneo lipi kulingana
na mahitaji yake,” aliongeza.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu aliyashukuru makanisa kwa huduma za kijamii
zitolewazo katika sekta za elimu, afya na kilimo kama ambavyo
ameshuhudia katika baadhi ya maeneo alikopita hapa nchini.
Pia
aliwakubalia ombi lao la kuwa na kikao cha pamoja baina ya watendaji wa
Serikali na makanisa ambacho kitajadili namna ya kuimarisha ubia katika
utoaji wa huduma za kijamii hususan za afya na elimu.
“Kikao
hiki kitalenga kufanya mapitio ya huduma zinazotolewa baina ya Serikali
na Makanisa lakini pia kitatusaidia kupata mrejesho wa mambo
yanayofanyika kwenye hospitali na shule mnazomiliki katika maeneo
mbalimbali hapa nchini,” aliongeza.
Alisema
waharakishe kuleta mapendekezo yao ili kikao hicho kifanyike kabla ya
Desemba, mwaka huu kwani kitaisaidia Serikali kupata mrejesho wa
kuboresha baadhi ya maeneo katika mwaka mpya wa kielimu unaoanza Januari
kila mwaka.
Mapema,
Baba Askofu Mkuu Kinyaiya alimweleza Waziri Mkuu kwamba wanahitaji eneo
la kujenga ofisi za makao makuu na makazi kwa ajili ya kanisa hilo
pamoja na makanisa yaliyo chini ya CCT ambayo kwa pamoja yanaunda Tume
ya Kikristo ya Huduma za Kijamii (CSSC). Alisema wanahitaji eneo kwa
ajili ya ujenzi wa ofisi na makazi ya Balozi wa Baba Mtakatifu.
Alisema
walipowasilisha maombi yao CDA, waliahidiwa kupatiwa eneo la makazi tu
lakini bado wanahitaji eneo la ofisi. Pia alitumia fursa hiyo kumshukuru
Waziri Mkuu kwa jinsi alivyoiwakilisha Serikali kwenye mazishi ya
Mhashamu Askofu Mstaafu, Mathias Isuja wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la
Dodoma ambaye alifariki Aprili 13 na kuzikwa Aprili 20, mwaka huu.
Naye,
Mkurugenzi Mtendaji wa CSSC, Bw. Maduki alisema katika sekta ya afya
hadi kufikia Juni 2016, makanisa yalikuwa yanamiliki na kuendesha
hospitali 102, vituo vya afya 102 na zahanati 696. “Kati ya hospitali
102, mbili ni za rufaa za kanda na 38 ni za hospitali teule za
Halmashauri za Wilaya na hospitali nyingine 62 zinatoa huduma
halmashauri mbalimbali,” alisema.
Alisema
karibu asilimia 38 ya hospitali hapa nchini zinamilikiwa na makanisa na
nyingi ziko maeneo ya vijijini. Pia alisema kuna chuo kikuu kimoja,
vyuo vikuu vishiriki vitatu, na vyuo vya mafunzo ya kati 62 ambavyo
vinatoa kozi za uuguzi, maabara na ufamasia.
Kuhusu
sekta ya elimu, Bw. Maduki alisema makanisa yanatoa elimu kuanzia elimu
ya awali hadi chuo kikuu na kwamba hadi kufikia Juni, 2016, makanisa
yalikuwa na shuke za msingi 161, za sekondari 369, na vyuo vya ufundi
stadi 126. “Pia tuna vyuo vya ualimu 14, vyuo vikuu tisa, vyuo vikuu
vishiriki 17 na vituo vya vyuo vikuu saba,” alisema.
No comments:
Post a Comment