Sunday, October 30, 2016

Tuliiga BRN, vipi uzazi wa mpango?

TAARIFA zilizopo zinaonesha kwamba nchi za Asia zikiwemo Malaysia na Singapore ambazo wakati tunapata uhuru kiwango cha maendeleo yao na sisi kilikuwa takribani sawa, zimepiga hatua kubwa ya maendeleo kutokana na kuwekeza vya kutosha katika elimu, afya, uzazi wa mpango na mageuzi ya kiuchumi.

Bila shaka tumeifanya Malaysia kama nchi tunayojifunza kwake, hususani suala zima la Matokeo Makubwa Sasa (BRN) hadi wataalamu wao walikuja nchini kutusaidia namna ya kunyanyua uchumi wetu kwa haraka kupitia njia hiyo. Lakini swali ambalo wengine wanajiuliza ni mbona hatukuwaiga pia suala zima la uzazi wa mpango ambao unatajwa kuwa moja ya kitu kilichowasaidia kupiga hatua?
Takwimu zinaonesha kwamba mwaka 1960 pato la taifa la Malaysia kwa mwaka lilikuwa Dola za Marekani 299 huku sisi likiwa 319. Lakini mwaka 2010, pato lao lilikuwa limefikia Dola 8,754 wakati letu likiwa Dola 514.

Takwimu pia zinaonesha kwamba mwaka 1960, wastani wa kuzaa kwa kila mwanamke wa Malaysia (fertility rate) ilikuwa watoto sita wakati sisi ikiwa watoto saba, lakini mwaka 2010 takwimu zinaonesha kwamba wao walikuwa na wastani wa kuzaa watoto wawili, sisi watoto 5.4 (sawa na sita).

Kadhalika mwaka 1960, kiwango cha kujiunga na shule za sekondari kwa Malaysia kilikuwa asilimia 35 wakati Tanzania kilikuwa 9, lakini mwaka 2010 kiwango chao kilikuwa asilimia 96 huku chetu kikiwa asilimia 27 tu.

Na kiwango cha wanafunzi kujiunga na vyuo (vikiwemo vyuo vikuu) kwa Malaysia mwaka 1960 kilikuwa asilimia 4, huku sisi kikiwa 0.5 lakini mwaka 2010 kiwango chao kilikuwa kimepanda hadi asilimia 37 wakati sisi kikiwa asilimia 3.9 tu.

Kwa mantiki hiyo, wakati tunapozungumzia kuelekea uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025 huku tukianza kufanya mageuzi ya kiuchumi, tunaweza tukafanikiwa haraka kama suala la uzazi wa mpango na elimu bora kwa watoto wetu tutalitilia maanani.

Faida za uzazi wa mpango Uzazi wa mpango una faida nyingi, kuanzia kupunguza vifo vya akina mama vinavyotokana na uzazi, kupunguza vifo vya watoto chini ya umri wa miaka mitano na kupunguza utoaji wa mimba usio salama (kienyeji) ambao pia huhatarisha sana maisha.

Lakini pia kuna faida nyingi za kiuchumi kutokana na uzazi wa mpango ikiwa ni pamoja na mama kuongezea fursa za kujishughulisha kiuchumi, familia kupata muda wa kutosha wa kuwekeza kwa watoto wao wachache lakini pia kuna faida kwa jamii kuendana na raslimali chache zilizopo.

Wanademografia wanasema jamii zote zilizopiga hatua ya maendeleo duniani, moja ya kitu kilichowasaidia kufika waliko leo ni kuhimiza uzazi wa mpango kwani una mchango mkubwa ikiwemo familia na taifa kwa ujumla kuwa na uwezo wa kuendeleza watoto kielimu.

Kwa mfano, hata kama tumehimiza vya kutosha suala la madawati mwaka huu, kama uzazi wa mpango hautazingatiwa, tutegemee kila mwaka kuwa na upungufu mkubwa wa madawati.

Hapo sijasemea matundu ya vyoo, vitabu, maabara, idadi ya waalimu na kadhalika! Njia za kisasa Njia za uzazi wa mpango za kisasa zimegawanyika katika makundi matatu, zipo za muda mfupi, muda mrefu na zile za kufunga kabisa kizazi baada ya wanandoa kukubaliana hivyo. Njia za muda mfupi kwa mujibu wa Dk Dismas Daniel wa Hospitali ya Marie Stopes ni matumizi ya sindano, vidonge na kondomu.

Anafafanua kwamba, kwanza kabla ya mama kupatiwa tiba hiyo, anafanyiwa uchunguzi na anapopewa, huwa imeshaaminika kwamba hatopata matatizo, na kama yapo ni madogo tu.

Anasema kinachofanywa na sindano au vidonge ni kuzuia yai lisipevuke na pia kuweka ute mzito kwenye njia ya kizazi, hatua inayozuia mbegu za kiume kutoingia kwenye mji wa mimba.

Anasema kutokana na mabadiliko hayo yanayotokana na homoni, baadhi ya watumiaji hupata madhara madogo, ikiwa ni pamoja kunenepa au baadaye kutokwa na damu, lakini kinachotakiwa ni kuwaona wataalamu na tatizo hushughulikiwa na kumalizwa.

Kuhusu kondomu anasema kuna watu ambao wanapata mzio (allergy) wakizitumia na hao ni wachache na wakiwaona madaktari watapata ushauri maridhawa. Njia za muda mrefu Dk Daniel anazitaka kuwa ni pamoja kitanzi na vijiti ambazo baadhi ya watu, hususani kitanzi, wamezipa pia sifa ambazo hazina.

"Kuna watu wanatoa madai kwamba mwanamke akiwekewa kitanzi, mara baba atakigusa, mara kinatembea mwilini na mengine ambayo hayana ukweli.

Kuna baba wakati wa tendo la ndoa na mkewe mjamzito alishamgusa mwanae?" Anahoji Dk Daniel.
Anafafanua kwamba kitanzi huwekwa kwenye mji wa mimba ambako si rahisi mwanamume kupagusa wala habari za kutanzi kutembea mwili hazina ukweli wowote.

Hata njia za kufunga kabisa kizazi kwa mwanamke na mwanaume, Dk Daniel anasema hazina madhara kama wengi 'wanavyobwabwaja' mitaani kwamba zinasababisha saratani, au kumfanya mhusika akose raha ya tendo la ndoa.

Mkutano wa FP 2020 Kuanzia leo, nchi yetu itakuwa mwenyeji wa mkutano wa Kimataifa kuhusu Uzazi wa Mpango maarufu kama FP 2020). FP 2020 ni mkutano unaojielekeza katika kutekeleza malengo ambayo dunia imejiwekea ifikapo mwaka 2020.

Mkakati huo ni wa ushirikiano wa kimataifa unaohamasisha haki za wanawake na wasichana za kuamua kwa uhuru ni wakati gani ambao ni mwafaka kwao kushika mimba na hivyo kuondokana na mimba wasizozitarajia.

Ni mpango unaoshirikisha serikali, asasi za kiraia, mashirika ya kimataifa, wafadhili, sekta binafsi, na watafiti wa maendeleo ya jamii katika kuwawezesha wanawake na wasichana zaidi ya milioni 120 kutumia njia za kiasa za uzazi wa mpango ifikiapo mwaka 2020.

Mkutano huo pia utashirikisha mpango wa kimataifa wa kusaidia kifedha juhudi za nchi mbalimbali katika kuimarisha afya ya wanawake, watoto na vijana wadogo, yaani Global Financing Facility (GFF).

Hadi mwaka 2013 wakati Tanzania inafanya mkutano wake wa Kitaifa wa Uzazi wa Mpango (FP), idadi ya watumiaji wa njia za kisasa za uzazi wa mpango ilikuwa asilimia 27 tu na lengo lilikuwa ni kufikia asilimia 60 hadi mwishoni mwa mwaka jana. Hata hivyo, takwimu zilizopo zinaonesha kwamba kasi siyo kubwa kwani ni asilimia 32 tu kwa sasa ndio wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Utafiti uliofanywa Zambia unaonesha kwamba kuwekeza dola moja katika uzazi wa mpango kunasaidia kuokoa dola nne katika masuala ya afya na maeneo mengine ya maendeleo, ikiwa ni pamoja na afya ya uzazi, chakula, malaria, elimu na huduma za maji. Wakati mkutano huu unafanyika nyumbani ni vyema tuzinduke na kujipanga katika kuongeza idadi kubwa zaidi ya matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango.

Ili hilo liwezekane tunatakiwa kuongeza elimu kuhusu faida za kupanga uzazi na kuongeza bidhaa za uzazi wa mpango na wataalamu hadi vijijini. Pia tunapaswa kuboresha sera na sheria zetu lakini kubwa kabisa ni kuongeza bajeti inayokwenda kwenye uzazi wa mpango, mintarafu suala zima la upatikanaji bidhaa zote za kupanga uzazi kisasa.

Bajeti iliyotengwa mwaka huu ni Sh bilioni 5, lakini mahitaji halisi ni Sh bilioni 20. Si vibaya tukaongeza hadi hata Sh bilioni 8, kiwango ambacho hatujawahi kufikia.

No comments:

Post a Comment