WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na
Utawala Bora, Angella Kairuki amewataka watumishi wa umma na sekta
binafsi kuwahudumia wananchi kwa usawa na kutumia utawala wa sheria.
Aidha, ameitaka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kutekeleza
majukumu yake ya kulinda na kutetea misingi ya utawala bora na kulinda
haki za binadamu kwa mujibu wa Katiba na Sheria za nchi.
Kairuki aliyasema hayo Dar es Salaam katika maadhimisho ya Miaka 50
ya Tume ya Kudumu ya Uchunguzi na kueleza kuwa utawala wa sheria
unamtaka mtu binafsi, taasisi za umma, taasisi za kitaifa na sekta
binafsi kuheshimu misingi yote ya utawala bora.
Alisema umuhimu wa tume hiyo ni kuangalia haki katika utendaji wa
serikali, vyombo vya serikali na huduma, ndiyo maana Mwalimu Julius
Nyerere aliamua kuanzisha tume hiyo.
‘’Tume hii ilikuwa ni taswira ya utawala bora, kufanya maadili, haki
za binadamu masuala ya rushwa. Kupitia tume hii tumepata vyombo vitatu
ambayo ni Tume ya Haki za Binadamu, Sekretarieti ya Maadili na Taasisi
ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU),’’ alisema Kairuki.
Aliongeza kuwa, vyombo hivyo ni muhimu katika masuala ya uwajibikaji, uadilifu na kusimamia masuala ya sheria na utawala bora.
Aidha, alisema serikali inaendelea kushirikiana nao kuhakikisha
wanawajengea uwezo kifedha, miundombinu na kiufanisi ili kufanya kazi
nzuri zaidi.
Naye Mwenyekiti wa Tume hiyo, Bahame Nyanduga alisema katika
maadhimisho hayo vitu vikubwa wanavyovikumbuka ni kuanzishwa kwa tume
hiyo na kumuenzi Mwalimu Nyerere ambaye alikuwa muumini wa haki za
binadamu na utawala bora.
Alisema tume hiyo imetetea misingi iliyoanzishwa na Nyerere na wahusika wakuu wanaochunguzwa ni watendaji wa taasisi za umma.
Alisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inasimamia hayo ili
kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na maendeleo licha ya kwamba wapo watu
wanaokiuka haki za binadamu.
Naye, Jaji mstaafu na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC),
Damian Lubuva alisema Mwalimu Nyerere alianzisha tume hiyo ili kujenga
Taifa lenye uhuru, umoja na kuheshimiana, lakini pia kusimamia watendaji
wenye hulka tofauti na kusimamia tabia za wanaoendesha mamlaka kuu
ikiwemo Serikali, Bunge na Mahakama.
Maadhimisho hayo yaliwakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali
akiwemo Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, mawaziri wakuu
wastaafu, Jaji Joseph Warioba na Frederick Sumaye na viongozi wengine
wastaafu wa tume hiyo na serikali.
No comments:
Post a Comment