Mkataba
wa Afrika wa Usalama wa Usafiri Baharini na Maendeleo (The African
Charter on Maritime Security, Safety and Development) umepitishwa katika
Mkutano wa Dharura wa Wakuu wa Nchi za Afrika (The AU Extraordinary
Summit) uliofanyika tarehe 15 Oktoba, 2016 Lome, Togo.
Kupitishwa kwa
Mkataba huu kumefuatia makubaliano yaliyofikiwa katika Mikutano ya
Kilele ya Wakuu wa Nchi za Afrika iliyofanyika Younde Juni, 2013 na
Visiwa vya Shelisheli Februari,2015
Tanzania
imewakilishwa katika Mkutano huo na Mhe. Balozi. Dkt. Augustine P.
Mahiga (MB), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
kwa niaba ya Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania ambaye hakuweza kuhudhuria Mkutano huu kwa
sababu ya Majukumu mengine ya Kitaifa.
Akihutubia
Mkutano huo Balozi Dkt. Mahiga alisema, Mkataba huo ni kati ya nyaraka
muhimu zitakazoelimisha kuhusu kutunza amani ya Dunia, usalama na
maendeleo katika karne hii ya 21.
Alisisitiza kwamba Bara la Afrika liko
kati ya bahari kuu mbili yaani Atlantic na Hindi ambazo ni kati ya
bahari zilizo na shughuli nyingi sana za usafirishaji duniani. Tanzania
ikiwa katika nusu ya ukanda wa pwani ya Mashariki na pwani ya Magharibi
ya Bahari ya Hindi yenye urefu wa Kilomita 1400, Mkataba huu ambao
Balozi Mahiga ametia sahihi kwa niaba ya Tanzania ni muhimu sana hivyo
amewasihi wanachama wengine kuhakikisha wanafanya hivyo.
Sambamba
na hilo Balozi Dkt. Mahiga amesema Mkataba huu si muhimu tu kwa Afrika
kulinda bahari na rasilimali zake bali ni muhimu kwa dunia nzima.
Balozi. Dkt. Mahiga ameomba Nchi zote na Mashirika ya Kimataifa kuunga
mkono utekelezaji wa mkataba huu. Kufuatia kupitishwa kwa mkataba huu
ameiomba Sekretariati ya Umoja wa Afrika kupeleka Mkataba huu kwenye
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na katika Jumuiya ya Kimataifa ili
kuweza kutambuliwa.
Aidha,
Balozi Mahiga amesisitiza kuwa bahari ni hadhina muhimu si tu ya samaki
na gesi bali rasilimali nyinine za thamani kama vile madini ambazo
zimekaa tu chini ya bahari hivyo ni jukumu la kila mwana Afrika
kuhakikisha analinda rasilimali muhimu tulizo nazo zikiwemo hizi ambazo
zinapatikana baharini.
Akimalizia
hotuba yake Balozi. Dkt. Mahiga alisisitiza “Hivi karibuni bahari hizi (
Atlantic na Hindi) zitakuwa chanzo muhimu cha nishati, hivyo kusaidia
jitihada za kuleta maendeleo kupitia rasilimali za bahari, naamini
mkataba huu utakuwa ni silaha muhimu katika kulinda rasilimali hizi za
bahari kwa ajili ya sasa na vizazi vijavyo”. Balozi. Dkt. Mahiga
ameusihi Umoja wa Afrika na Wanachama wote kuendelea kuuboresha Mkataba
huu na kupitisha viambasho muhimu na hatimaye kuharakisha kuuridhia
Mkataba huu ili utekelezaji wake uanze bila kuchelewa.
Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki
Dar es Salaam, 16 Oktoba, 2016.
No comments:
Post a Comment