Friday, October 14, 2016

Miaka 17 Bila Nyerere: Mwinyi Asema Taifa Limepoteza Mwelekeo, Asikitishwa na Uwepo wa Panya Road


Wakati  Tanzania leo ikiadhimisha kumbukumbu ya miaka 17 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi amesema Taifa limepoteza mwelekeo  kwani halina tena uadilifu aliotujengea Mwalimu Nyerere.

Mwinyi aliyerithi mikoba ya urais kutoka kwa Mwalimu Nyerere mwaka 1985, alisema hayo jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua mdahalo wa kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na kuzindua kitabu cha 'Selective works of Mwalimu Nyerere', kilichotafsiriwa na wasomi kutoka China.

Mdahalo huo uliandaliwa na Taasisi ya Uongozi ikishirikiana na Ubalozi wa China na Asasi ya Urafiki kati ya Tanzania na China. Mwalimu Nyerere aliyeitawala Tanzania kwa takribani miaka 24, alifariki dunia Oktoba 14, 1999 kwenye Hospitali ya St Thomas jijini London nchini Uingereza ambako alikuwa akitibiwa maradhi ya saratani ya damu.

Aliiongoza Tanzania kwa uadilifu mkubwa akisimamia misingi ya haki, umoja, mshikamano, kupiga vita rushwa, kusisitiza kujitegemea na uzalendo kwa nchi.

“Kazi za kawaida kweli zinafanywa na zinaendelea, lakini sina uhakika hata kidogo kama uadilifu aliotuachia Mwalimu bado tunao, sijui nani wa kulaumiwa,” alisema Mwinyi maarufu kama Mzee Ruksa. Alisema kwa namna ambavyo mambo yanakwenda, ni kiashiria tosha kuwa nchi haina uadilifu tena.

“Mambo yanavyokwenda kama gari lililo katika usukani,” alieleza Mwinyi na kuongeza kuwa kuna kila sababu ya kutafakari hali ilivyo sasa ikilinganishwa na ile ambayo iliachwa na Baba wa Taifa miaka hiyo 17 toka kufa kwake.

Alisema nafasi hiyo ya mazungumzo katika mdahalo, inawapasa kukaa kutafakari namna ya kurudisha nchi kwenye reli ambayo iliachwa na Mwalimu Nyerere ambaye ndiye muasisi wa taifa hili katika misingi ya uongozi.

“Tuna utajiri wa machoni, lakini ndiyo aliyokusudia Mwalimu? Alitufundisha tuwe matajiri wa vitu au matajiri wa moyo? Tujali vitu au tujali utu?" Alihoji Rais huyo mstaafu.

Aidha, Mwinyi alisema Mwalimu Nyerere aliijenga nchi kwa misingi ya utu na kwamba alijitahidi sana kusaidia nchi nyingine za Afrika na hasa zile za Kusini mwa Afrika kujikomboa ili Afrika yote iwe huru. 
Alisema ukombozi huo usiwe wa kuingia msituni kupigana na kuwatisha akinamama na pia usiwe wa kuwaacha watoto kujilea wenyewe bila kujengewa misingi ya uadilifu.

“Siku hizi kuna panya road, wametoka wapi watoto hawa? Sisi wazee hatukuwepo? Au sisi wazee tumetengeneza mazingira kuwepo hao, mbona mwanzo hawakuwepo sasa wametoka wapi?" Alihoji tena Mwinyi.

Mwinyi alihoji pia kama mafunzo ya askari yamebadilika, iweje huko awali askari alikuwa ni mtu ambaye wananchi walikuwa wakimuona wanamkimbilia tofauti na sasa ambako wananchi wanamkimbia askari.

Aliongeza kuwa pia ni wakati sasa wa kutafakari kwa nini nchi pamoja na watu wake wamefikia walipo sasa kwani kuna tatizo pia la ubaguzi wa kikabila katika upatikanaji wa ajira mbalimbali pamoja na ubaguzi wa kidini.

Aidha, alisema kama yatabainika kuwepo mambo hayo, yasiachwe hivyo badala yake upatikane ufumbuzi ili kurudisha yale yote mema ambayo yaliachwa na Mwalimu Nyerere katika harakati zake za kuikomboa nchi, uongozi wake na pia usia wake.

"Baba wa Taifa kwangu alikuwa zaidi ya kiongozi, alikuwa kaka, rafiki na mtu aliyegeuza maisha yangu na kunifanya kuwa hivi nilivyo sasa, nimejifunza mambo mengi na nisipoyafuata itakuwa hasara kwangu,” alisema Mwinyi mmoja wa viongozi wastaafu wanaoheshimika na kupendwa na Watanzania. 
Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, Profesa Joseph Semboja alisema taasisi hiyo inaamini mdahalo huo utazaa maarifa na kuleta majibu ya changamoto ya karne ya 21.

“Mwalimu leo hii hayupo lakini mawazo na falsafa zake vinaishi na sisi hivyo ni vyema tuvitumie katika vizazi vijavyo,” alisema Profesa Semboja.

Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema Mwalimu Nyerere alitujengea misingi ya kujenga taifa katika msingi wa watu na tabia zao na sio vitu kama vile majengo, madaraja na mengineyo.

Alisema mdahalo ule haukuwa kwa ajili ya kutazama kifo cha Mwalimu Nyerere, bali kutazama mambo ya msingi ya kulisaidia taifa kusonga mbele.

Katibu Mkuu wa Asasi ya Urafiki China na Tanzania, Joseph Kahama alisema nchi mbalimbali za Afrika zimekuwa zikibadili katiba za nchi zao na viongozi kujiongezea muda wa utawala, lakini nchini mchakato wa Katiba umedorora kabisa.

No comments:

Post a Comment