VIGOGO watatu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA)
akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa mamlaka hiyo, Ephraim Mgawe (62)
wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam wakikabiliwa na mashitaka ya kujihusisha na rushwa ya Sh bilioni
nane.
Mbali na Mgawe, vigogo wengine katika kesi hiyo ni Mkurugenzi wa
zamani wa Uhandisi wa TPA, Bakari Kilo (59) na aliyekuwa Meneja wa
Mazingira wa TPA, Theophil Kimaro (54) pamoja na Mkurugenzi Mkuu
Mtendaji wa Kampuni ya DB Shapriya, Kishor Shapriya (60).
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani jana na kusomewa mashtaka
mawili na Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi mbele ya Hakimu Mkazi
Mkuu, Thomas Simba. Wakili Kishenyi alidai katika tarehe tofauti kati ya
mwaka 2009 na 2012, Mgawe, Kilo na Kimaro kwa kutumia nafasi zao,
waliomba rushwa ya Dola za Marekani milioni nne ikiwa ni zaidi ya Sh
bilioni nane.
Inadaiwa waliomba rushwa hiyo kutoka kwa Shapriya ili kumuwezesha
ashinde zabuni iliyokuwa ikishindaniwa yenye namba
AE/0116/2008-2009/10/59 kwa ajili ya ujenzi wa bomba la TPA katika RAS
ya Mjimwema.
Aidha, inadaiwa katika tarehe tofauti kati mwaka 2008 na 2009 akiwa
kama Mkurugenzi wa DB Shapriya alitoa rushwa ya Dola za Marekani milioni
nne kwa vigogo hao, kwa ajili ya kuiwezesha kampuni yake ishinde
zabuni. Baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa walikana kuhusika na
kutenda makosa hayo.
Wakili Kishenyi alisema upelelezi wa kesi bado unaendelea, pia hawana
pingamizi la dhamana endapo washtakiwa watatimiza masharti ya dhamana
yatakayotolewa na mahakama.
Vigogo hao waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya
dhamana yaliyowataka kuwa na wadhamini wawili waaminifu watakaosaini
hati ya dhamana ya Sh milioni 500 kwa kila mmoja.
No comments:
Post a Comment