Wednesday, October 5, 2016

MD UBUNGO AWATAKA WATUMISHI WA MANISPAA YA UBUNGO KUZINGATIA NIDHAMU NA UADILIFU KATIKA KAZI

Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi kayombo (Katikati) akisikiliza kwa makini maoni ya watumishi wa Manispaa hiyo wakati wa kikao cha pamoja na watumishi wa Manispaa hiyo

 Waratibu wa elimu wakisikiliza kwa makini maelekezo ya utendaji kazi kutoka kwa Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi kayombo


Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi kayombo akisisitiza jambo wakati wa kikao cha pamoja na waratibu wa elimu Kata wakati wa kikao cha Kazi


Watumishi wa Manispaa ya Ubungo wakimsikiliza kwa makini Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Lipesi kayombo wakati wa kikao cha kazi

Na Mathias Canal, Dar es salaam

Watumishi wote wanaofanya kazi katika Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo wametakiwa kufanya kazi katika hali ya ukweli, Uwazi, Ufanisi, Uadilifu, Kujituma na kuwa na nidhamu katika utendaji ili kukuza ufanisi wa Changamoto zinazowakabili wananchi mbalimbali.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam Ndg John L. Kayombo wakati wa kikao cha kazi na waratibu wa elimu kutoka kata 14 na wakuu wa shule za msingi zilizopo katika Manispaa hiyo mara baada ya ukaguzi wa shule za msingi Temboni Msigani.

Kayombo amezuru katika maeneo tofauti tofauti katika Halmashauri hiyo ikiwemo Shule ya Msingi Temboni ambapo alikutana na kamati ya shule sambamba na kufanya ukaguzi wa vyumba 8 vya madarasa utakaogharimu kiasi cha Shilingi milioni mia moja sitini (Mil 160) na matundu kumi ya choo ambayo yanataraji kugharimu kiasi cha shilingi milioni thelathini na mbili (Mil 32) ambapo pia ukarabati wa shule wenyewe utagharimu kiasi cha shilingi milioni kumi (Mil 10).

Kayombo alisema kuwa fedha hizo zimetolewa na serikali kuu kwa ajili ya kuboresha sekta ya elimu na kuhakikisha watoto wa masikini wanapata elimu bora katika mazingira rafiki.

Ziara ya kazi ya Mkurugenzi huyo wa Manispaa ya Ubungo John L. Kayombo kwa kukutana na waratibu wa elimu kutoka kata 14 za Halmashauri hiyo pamoja na wakuu wa shule za msingi imejikita zaidi katika kuamsha ari na ufanisi katika utendaji na kuwakumbusha watendaji wote majukumu yao ya kuwatumikia wananchi.

Ziara hiyo inatazamiwa kuwa kila mtumishi sasa atakumbuka majukumu yake katika utendaji na kuyafanya ipasavyo kwa mujibu wa kanuni, taratibu na sheria za muongozo wa watumishi wa umma.
Akizungumza na www.wazo-huru.blogspot.com MD Kayombo alisema kuwa watumishi wa serikali wanapaswa kutambua kuwa hawatakiwi kujiingiza na kufanya siasa zisizo na tija badala yake wanapaswa kuwajibika zaidi katika kuwatumikia watanzania na kuakisi kauli mbiu ya serikali ya awamu ya tano ya Hapa Kazi Tu chini ya Rais Dkt John Pombe Magufuli.

Kuzuru katika maeneo mbalimbali kukagua miradi na kujionea shughuli za maendeleo ni utaratibu ambao amejiwekea Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo John L. Kayombo ili kufahamu maeneo yake ya kiutendaji na kuamsha ari katika uwajibikaji na ufanisi wa kazi.

Baada ya ziara hiyo ya kukutana na waratibu Kata katika Manispaa ya Ubungo MD Kayombo hii leo amekutana tena na watumishi wote wa Manispaa kikiwa ni kikao chake cha kwanza kukutana na Watumishi wote kwa lengo la kutoa miongozi na maelekezo mbalimbali katika utekelezaji wa majukumu yao.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Manispaa ya ubungo Mkurugenzi huyo amesisitiza ufanyaji kazi kwa bidii, ushirikiano mahali pa kazi, upendo na uaminifu ili kuiwezesha ubungo kusonga mbele katika maendeleo na kuwafanya wananchi wa Ubungo kuimarika katika sekta ya uchumi.

MD Kayombo amewataka watumishi hao kuwa wabunifu katika utendaji kazi wao ili kuongeza mapato ya ya manispaa ya kurahisisha Manispaa hiyo katika ufanisi wa kazi na kuwahudumia wananchi kirahisi.

No comments:

Post a Comment