Monday, October 17, 2016

MAONI YANGU KUHUSU MASUALA YA CHAKULA NCHINI

Mchambuzi wa Maswala mbalimbali nchini Tanzania Mathias Canal katika picha akiwa AFM Radio ya Mjini Dodoma kwa ajili ya mahojiano

Na Mathias Canal

Leo kuanzia majira ya saa 2:30 hadi 3:00 Asubuhi nilialikwa AFM Radio katika kipindi cha AMKA NA TOFAUTI kinachoongozwa na Elizabeth Kachenje, Victor Simion na Clement John lengo ilikuwa ni kupata maoni yangu kuhusu Maadhimisho ya siku ya Chakula Duniani yaliyoadhimishwa jana na kutazama namna bora ya uhifadhi wa chakula kwa nchi yetu ya Tanzania.

Kwanza mpaka sasa tumefika miaka 55 ya Uhuru na nchi yetu katika kipindi cha miaka 50 ya uhuru haijawahi kuwa na utoshelevu wa chakula mpaka tulipofika miaka 52 ya uhuru yaani kuanzia Mwaka 2013/2014 ndipo tukapata chakula cha kutosha hadi kufikia Asilimia 102 na 105.

Hii ni hatua nzuri sana lakini kwa kiasi kikubwa wananchi: hapa niwazungumzie vijana zaidi, wanalima mashamba makubwa na kupata mazao mengi lakini katika kulima kwao yaweza kuwa Mpunga, Mahindi, Mtama, Alizeti ama Pamba asilimia kubwa ya vijana hao wanalima mazao hayo wakiwa na lengo la kutatua matatizo ya familia zao sio kwa maendeleo ya kiuchumi ili kuondokana na Umasikini.

Waziri wa 67 wa Mambo ya nje nchini Marekani Hillary Rodham Clinton aliwahi kusema kuwa "Usalama wa chakula ni suala la kiusalama. Hapa Clinton alitaka kufikisha maana ya kwamba kulima na kuvuna mazao mengi pekee haitoshi bali kuna kila sababu ya kuhakikisha mazao hayo yanahifadhiwa vizuri kwa kuwekwa kwenye vihenge maalumu na kupuliza dawa.

Taifa linaweza kukitumia kilimo kama njia bora ya kumnufaisha mtanzania mkulima kuondokana na umasikini kwa kumuelimisha mbinu nzuri na bora ambazo zitamfanya akivuna mazao yake ajue kwamba anatakiwa kuyahifadhi vizuri lakini afahamu kuwa mkulima hatakiwi kulala na mazao ndani badala yake anapaswa kuyauza na kihifadhi fedha zake Bank mahala salama kwa matunzo ya fedha.

Mwaka juzi nikiwa Mkoani Iringa Mwandishi nguli nchini Maggid Mjengwa alifanya utafiti uliobaini kuwa Iringa ni miongoni mwa mikoa inayostawi sana mazao mbalimbali lakini ni mkoa ambao unashika nafasi ya tatu kwa Lishe Duni nchini na hii ilisababishwa na wazazi kujihusisha na unywaji pombe kwa kiasi kikubwa pasina kuhakikisha watoto wao wanapata mlo mzuri na wenye virutubishi hivyo watoto wengi wenye umri wa chini ya miaka mitano wakawa na Utapiamlo sababu ikiwa ni pamoja na wazazi kukwepa majukumu yao.
Kilimo ni moja ya sekta Muhimu katika uchumi na Maendeleo ya nchi yetu kwa kuwa inatoa ajira takribani asilimia 74% Kumbe kama kilimo kikitiliwa maanani maana yake tatizo kubwa la ajira huenda lisisikike kabisa.

Kwa mujibu wa Ofisi ya TAKWIMU Mwaka 2006 Katika Muongo wa Miaka 10 iliyopita zaidi ya watoto 600,000 wenye umri wa chini ya miaka mitano wanakufa kwa kukosa Lishe ya kutosha yaani hii ina maana kuwa kila baada ya dakika 12 mtoto mmoja anafariki hii ni hasara kubwa kwa Taifa kupoteza watoto wote hao ambapo ingeweza kufanya urutubishaji wa chakula kwa kutumia Bilioni 19 tu ambazo ndiyo uhitaji.

NINI USHAURI WANGU...!

1. Nimeshauri kituo cha Vyakula na Lishe TFNC kutokwepa majukumu yake iliyonayo ya kuongoza kuhusu Lishe ili kuwa na Taifa lenye watoto watakaokuwa kifikra kwani kila mwaka karibu Bilioni 700 zinatumika kugharamia virutubishi.

2. Kuachana na fikra za kuamini kuwa Shirika la Chakula na kilimo la umoja wa Mataifa (Food and Agriculture Organization of the United Nations FAO) ambalo lina lengo la kuboresha uzalishaji na ugawaji wa mazao na vyakula duniani kwa shabaha ya kuboresha hali ya watu Duniani bali tujue namna bora ya kupambana na ukata wa ajiri na kuwa na kilimo bora na chenye tija.

3. Kuacha kupuuza gharama za uchumi zinazotokana na Lishe duni ili kuboresha Lishe kwa watoto wa Tanzania katika mpangilio bora wa Mlo wa kila siku.

4. Serikali itoe elimu ya kutosha ya utunzaji wa chakula na kilimo bora ikiwemo maafisa kilimo kushiriki na wananchi kuwaelimisha katika hatua zote za kuandaa mashamba na kilimo chenye tija.
5. Wananchi kutambua kuwa wanapaswa kuuza ziada ya chakula wanachovuna ili kuhifadhi kwa umakini fedha zao na kuwa na matumizi mazuri ya fedha zao.

6. Kina mama wakubali kunyonyesha miezi sita bila kumchanganyia mtoto chakula kingine ili mtoto apate Lishe bora na imara kwa kipindi hicho kwani maziwa ya mama ni kinga na tiba tosha kwa mtoto.

Mwishi niipongeze AFM Radio kwa ufanisi wake na kwa kunialika katika mjadala huu mzuri na mpana kwa maslahi ya Taifa.

Bado nipo Mkoani Dodoma kwa majukumu ya siku nzima ya leo ambapo kesho nitaelekea katika majukumu mengine ya kikazi.

Wakati Mwema
Mathias Canal (Sauti ya Wanyonge)
0756413465
Dodoma


No comments:

Post a Comment