Baadhi ya wadau na Wanasayansi Watafiti wakifuatilia Kongamano hilo la 30 la NIMR mapema leo
Meza
kuu ikifuatilia tuko hilo la ufunguzi: Makamu wa Rais Mh. Mama Samia
Suluhu Hassan (Wa pili kulia) akifuatiwa na Naibu Waziri wa Afya,
Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi
Kigwangalla. Kushoto ni Dk. Honorati Masanja kutoka taasisi ya Utafiti ya Ifakara na kulia ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela
Tukio likiendelea
Makamu
wa Rais Mh. Mama Samia Suluhu Hassan akikabidhi ngao kwa mmoja wa
wadhamini wa kongamano hilo. Kushoto ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla na Kulia
ni Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela
Naibu
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk.
Hamisi Kigwangalla akizungumza na wanahabari (Hawapo pichani) muda mfupi
baada ya ufunguzi wa kongamano hilo
Mkurugenzi
Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela akizungumza na wanahabari (Hawapo
pichani) muda mfupi baada ya ufunguzi wa kongamano hilo.
Makamu wa Rais Mh. Mama Samia Suluhu Hassan amewahakikishia
Wanasayansi Watafiti waliopo nchini kuwa Serikali ya Tanzania inatambua mchango
wao na wataendelea na juhudi za
kuwalinda kwani ni nguzo muhimu ya kufikia malengo ya milenia katika Nyanja
mbalimbali ikiwemo Uchumi, Afya, Elimu na Maendeleo endelevu.
Makamu wa Rais ameyasema hayo mapema leo Jijini Dar es
Salaam wakati alipozindua rasmi Kongamano la 30 la Kimataifa la Wanasayansi
Watafiti lililoandaliwa na Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
(NIMR) ambalo ni la siku tatu kuanzia
Oktoba 4 hadi 6.2016.
Akiwahutubia Wanasayansi hao watafiti zaidi ya 300 kutoka
Tanzania na Mataifa ya Nje, amesema kuwa
Taifa bila watafiti hakuna maendeleoo hivyo uwepo wa watafiti hao ni kielelezo
tosha cha kufikia maendeleo hivyo anaamini kuwa baada ya mkutano huo, Wataalam
hao watakuwa chachu ya kichocheo cha uchumi kupitia tafiti zao.
Akiwaondoa hofu wanasayansi watafiti hao, Makamu wa Rais
Mama Samia Suluhu amebainisha kuwa, Serikali imesikitishwa na tukio lililotokea
hivi karibuni la kuchomwa moto baadhi ya watafiti huko Mkoani Dodoma kuwa ni la
kinyama na halivumiliki na sheria itachukua mkondo wake na wahusika wote
watafikishwa mikononi mwa sheria.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii,
Jinsia, Wazee na Watoto, Mh. Dk. Hamisi Kigwangalla katika mkutano huo
amebainisha kuwa, Wizara yake
inashirikiana bega kwa bega na wanasayansi na imekuwa ikiwatumia katika mikakati
mbalimbali ya kitaifa na hata kujenga sera za Afya na mambo mengine ya
kimaendeleo.
“Wanasayansi watafiti
kwa uzoefu wao tunautumia kwa kiwango kikubwa sana hapa nchini. Kwani wamekuwa
chachu kubwa sana na hata mfumo wa Kiserikali umekuwa ukitengeneza mfumo
mahususi wa kufanya kazi kwa pamoja kwani hata sera na mikakati ya nchi pia
tumekuwa tukiwatumia wanasayansi hao” amesema Dk. Kigwangalla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk. Mwele Malecela
amesema kongamano hilo linajumuisha nchi mbalimbali za Afrika, Ulaya na Amerika
ambapo washiriki zaidi ya 300 wanashiriki
huku mada zaidi ya 220 zitawasilishwa na kujadiliwa kwa pamoja na wataalam
hao.
“Jumla ya mada 220 zinawasilishwa kuanzia leo na kujadiliwa
katika Kongamano hili la Siku tatu ambalo pia litahusisha mkutano Mkuu wa mwaka
wa NIMR”. Amesema Dk. Mwele.
Katika kongamano la mwaka huu, linaongozwa na kauli mbiu ya
“Uwekezaji katika tafiti zenye ubunifu ili kufikia malengo endelevu ya dunia”.
Nchi ambazo zinashiriki kongamano hilo kuwa ni Afrika
Kusini, Kenya, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Australia, Denmark,
Ubeljiji, Uholanzi, Uingereza, Ujerumani, Uswis, Kanada, Sweden, Norway,
Marekani, Bangladesh, Thailand na wenyeji Tanzania.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment