KAMPUNI
ya Simba Motors imesema ina mpango wa kujenga kiwanda cha kuunganisha
magari aina ya pick-up ambacho kitaanza kuzalisha magari kabla ya
Desemba 30, mwaka huu.
Ahadi
hiyo imetolewa jana mchana (Jumatatu, Oktoba 10, 2016) na Mkurugenzi
Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Jitesh Ladwa mbele ya Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa katika mazungumzo yaliyofanyika ofisini kwake Magogoni, jijini
Dar es Salaam.
“Tumeamua
kuunda magari aina ya pick-up kwa sababu ya mahitaji makubwa yaliyopo
nchini. Takwimu zinaonyesha kuwa, kwa mwaka Tanzania inanunua magari ya
aina hii zaidi ya 4,000. Katika nchi za SADC mahitaji ni pick-up 35,000
kwa mwaka. Tutaanza na mtaji wa dola za Marekani milioni 200 na tumeomba
ekari 200 katika eneo la EPZ,” amesema.
“Eneo
la kiwanda cha kuunganisha magari peke yake linahitaji ekari 50, kwa
hiyo tukiweka na yadi za kupaki magari, eneo la viwanda vingine, eneo la
kushusha na kupakia makontena yatakayokuwa yakisafirishwa kwenda nchi
jirani, ni lazima tutahitaji eneo kubwa zaidi,” amesisitiza.
Amesema
mradi huo wa majaribio, utaanza kwa kutengeneza magari 20 kila mwezi na
kwamba kazi ya utengenezaji magari itaongezeka na kufikia 1,000 na
baadaye 5,000 kwa mwaka. “Tunataraji gari la kwanza litazinduliwa kabla
ya Krismasi, mwaka huu,” amesema.
Bw.
Ladwa amesema uundaji wa magari hayo aina ya Foton-Tunland utafanyika
kwa ubia baina ya kampuni yao, SUMA-JKT na kampuni Foton International
ya China kwa kutumia teknolojia ya Kichina na kwamba magari hayo
yanayotumia 4-Wheel Drive, yana uwezo wa kupita kwenye barabara za aina
zote.
Akizungumza
katika kikao hicho, Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Kampuni hiyo, Bw.
Aatish Ladwa, amesema mradi utakapoanza, mbali ya kutoa ajira kwa
Watanzania, utawezesha pia kujengwa kwa viwanda vingine
vitakavyotengeneza matairi ya magari, vioo, taa, bumpers, viti na
filters.
“Tunataraji
kujenga uwezo wa wahandisi wazawa, uhamishaji wa ujuzi kwa mafundi wa
Kitanzania (technology transfer), kupunguza bei kwa mlaji wa mwisho,
kupunguza gharama za uzalishaji, kutekeleza amza ya Serikali ya kuifanya
Tanzania kuwa ni nchi ya viwanda, kuongeza ajira kwa wanajeshi, na
kuwezesha upatikanaji wa vipuri vya magari kwa urahisi na kupunguza
uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.”
“Kiwanda
kitaajiri wafanyakazi 1,500 kwa kuanzia ambao watakuwemo mafundi na
watoa huduma mbalimbali, lakini katika kipindi cha miaka mitatu hadi
mitano, tunataraji kuongeza wafanyakazi wengine 5,000 wakati uzalishaji
ukiwa umepamba moto,” amesema.
Kwa
upande wake, akizungumza mara baada ya kulikagua gari la mfano aina ya
Foton-Tunland, Waziri Mkuu amesema anawakaribisha kwenye uwekezaji huo
hasa ikizingatiwa kuwa magari hayo yana uwezo wa kupita kwenye maeneo ya
vijijini ambako barabara zake siyo nzuri.
“Ofisi
za Serikali zinayahitaji zaidi haya magari, hospitali zetu za wilayani
nazo pia zinayahitaji haya magari ili yaweze kutoa huduma za chanjo kwa
watoto, huduma za UKIMWI, kampeni za kupambana na malaria, na huduma kwa
mama wajawazito huko vijijini,” amesema.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment