Saturday, October 22, 2016

EU yapongeza mapambano dhidi ya rushwa


BALOZI wa Umoja wa Ulaya (EU) katikaTanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Roeland Van de Geer ameipongeza serikali ya awamu ya tano kwa kuonesha nia katika kushughulikia rushwa na kuleta maendeleo nchini.

De Geer alitoa pongezi hizo alipokutana na wadau wa habari, wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Alisema wanapongeza juhudi za serikali katika kuondoa umasikini, rushwa na kuleta maendeleo kwa wananchi. Balozi huyo pia alielezea dhamira ya Umoja wa Ulaya kuleta amani na utulivu katika Bara la Afrika.

“Usalama na amani Afrika siku zote vimekuwa ni kipaumbele cha Umoja wa Ulaya. Umoja huu umekuwa ukifadhili na kusaidia shughuli za walinda amani ili kurejesha amani na utulivu katika bara la Afrika,” alisema.

Aliongeza pia umoja huo umesaidia kwa asilimia kubwa, kutokomezwa kwa matukio ya kiuharamia baharini katika ukanda wa Afrika.

Akijibu swali la Mhariri Mtendaji wa Kampuni inayochapisha magazeti ya Daily News, HabariLeo na SpotiLeo (TSN), Dk Jim Yonazi aliyetaka kujua mtazamo wa EU juu ya kujitoa kwa nchi za Afrika kwenye Mahakama Kimataifa ya Uhalifu (ICC), balozi huyo alisema umoja huo siku zote unataka kuona kuna haki na usawa duniani kote, hivyo wanatarajia kulijadili suala hilo kwenye mkutano ujao.

Vile vile alishauri suala la Zanzibar, liangaliwe zaidi kwa kuwa muda bado upo.

“Kama marafiki, penye uzuri tunasifia, na kama kuna tatizo pia tunasema, hivyo tunaishauri Tanzania na suala la Zanzibar, tunadhani bado linabidi liangaliwe na muda bado upo,” alisema.

No comments:

Post a Comment