Tuesday, October 11, 2016

Adhabu ya Kunyongwa : Wafungwa 472 wasubiri hatma yao kutoka kwa Rais Magufuli

Watu 472 waliohukumiwa adhabu ya kifo kutokana na makosa mbalimbali, wanasubiri saini ya Rais Dk. John Magufuli ili kujua hatima ya utekelezaji wa adhabu zao ama laa.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa kati ya watu hao, wanaume ni 452 na wanawake ni 20.
Taarifa hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk. Hellen Kijo-Bisimba, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu adhabu ya kifo.

Bisimba alisema, watu hao walihukumiwa adhabu ya kifo kutokana na kutiwa hatiani na makakama kwa makosa ya uhaini na mauji.

Licha ya adhabu hiyo alisema hatua ya utekelezaji wake inakwenda kinyume na haki za binadamu kama inavyotafsiriwa katika matamko na mikataba mbalimbali ya kimataifa.

Kutokana na hali hiyo, Dk. Kijo-Bisimba, alisema hadi kufikia Desemba mwaka jana, jumla ya watu 472 walikuwa wamehukumiwa adhabu hiyo.

Alisema wakati watu hao wakisubiri adhabu hiyo, wengine 244 waliopo katika magereza mbalimbali bado wanasubiria maamuzi ya rufaa zao.

“Licha ya adhabu hii kutotekelezwa hapa nchini kwa takriban miaka 22 na miaka 24 ya kwanza ya uhuru, taarifa zinaonesha kuwa hadi sasa ni watu 72 tu ambao wameshanyongwa kutokana na adhabu hiyo,” alisema.

Dk. Kijo-Bisimba alitoa taarifa hiyo katika kipindi cha kuelekea maadhimisho ya siku ya kupinga adhabu ya vifo duniani, ambayo itafanyika katika nchi 70 na kaulimbiu ikiwa ni “Kuua ni Nyenzo ya Kigaidi, Acha Mnyororo wa Kigaidi,”.

“Leo ni miaka 14 tangu wanaharakati walivyoamua kuwepo kwa siku hii tusipokuwa na uhai hatuwezi kufanya kitu chochote hivyo adhabu hii haina maana kwani inaingilia haki ya uhai wa binadamu na kuona si kitu cha thamani,” alisema Bisimba.

Mkurugenzi huyo alisema, hadi sasa nchi 140 duniani zimeshafuta adhabu hiyo, ambapo kwa upande wa Afrika nchi 17 zimeshakubali kufuta adhabu hiyo.

Hata hivyo alisema ni wakati mwafaka kwa Serikali kuondoa adhabu hiyo, ili Tanzania iwe nchi ya 18 katika bara la Afrika kufuta adhabu hiyo, ambayo haina faida yoyote.

Mkurugenzi huyo wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, alisema kuwa adhabu hiyo inakabiliwa na upungufu mkubwa ikiwamo kuwapa marais ugumu kuweka saini kwa mtu kuuawa.

“Ni miaka 22 sasa nchi yetu haijawahi kutekeleza adhabu hiyo kwani Rais ndiye anayeruhusiwa kwa mujibu wa sheria lakini hata wao wanaogopa kufanya hivyo ili mtu mwingine afe badala yake wangetoa adhabu mbadala kwani wengine wanaofanya makosa hayo ni vichaa,” alisema.

Alisema adhabu hiyo ni ya kibaguzi na huwatia hatiani watu maskini wasiokuwa na uwezo wa kujitetea mahakamani au kuweka mawakili.

Dk. Bisimba, ameiomba Serikali isitunge tena sheria ya kifo na ikiwezekana ya sasa ikiwemo iliyoongezwa ya makosa ya ugaidi iondolewe na kutafutwa adhabu mbadala kwa mtu atakayetiwa hatiani.

“Adhabu ya kifo imeainishwa kwenye Sheria ya Kanuni ya Adhabu, sura ya 16 ‘Penal Code’ ambayo ililetwa na utawala wa kikoloni mwaka 1945. Hata baada ya Uhuru 1961 hukumu ya kifo imeendelea kuwa sehemu ya sheria licha ya marekebisho mbalimbali ya sheria hiyo ikiwemo marekebisho ya mwaka 2002.
 
“Adhabu ya kifo hutolewa kwenye makosa ya mauaji chini ya sheria hiyo kifungu 197 na kwenye hati ya kosa la uhaini chini ya kifungu cha 39 (3) (C).

“Pamoja na hayo mwaka huu Serikali imeongeza adhabu ya kifo kama mtu akikutwa na kosa la ugaidi chini ya sheria ya kudhibiti ugaidi ya mwaka 2002 kwenye mabadiliko madogo ya sheria, hii imeengeza makosa ambayo mtu anaweza kuhukumiwa kifo kufikia makosa matatu,” alisema Dk. Bisimba

Alisema kwa kuzingatia misingi ya haki za binadamu na mikataba mbalimbali ya kikanda na kimataifa ya haki za binadamu, zipo sababu za msingi za kupinga adhabu ya kifo.

“Tunapenda kuweka wazi kuwa hatufurahii watu kuua watu wengine na ndiyo maana hatungependa hata muuaji auawe kwa vile ni sawa na kumkubalia kuua. Adhabu ya kifo ni ya kinyama na isiyo na staha, inayotweza utu wa ubinadamu na hufanya Serikali ionekane pia kama mhalifu kwa kuua.

“Adhabu hii ikitolewa kwa mtu asiye na hatia kimakosa huwezi kuirekebisha kwani mfumo wa utoaji haki huwa pia na mianya ya makosa na hivyo maisha ya mtu yanweza kupotea bure na hakuna ushahidi kama adhabu hii inazuia watu wengine kutotenda makosa kama hayo,” alisema

Mbali na maadhimisho hayo kituo hicho kilizindua kitabu kinachoelezea adhabu ya kifo na ukiukwaji wa Haki za Binadamu cha mwaka 2015.

No comments:

Post a Comment